Fursa za kujiendeleza kwa waliofanya vibaya kidato cha nne

Muktasari:

  • Ieleweke kufeli kidato cha nne si ishara mbaya maishani na wala haijawa sababu ya kuanza kuamini kuwa umeshafeli kimaisha.
  • Kwa kuzingatia ukweli kuwa wapo baadhi ya wanafunzi waliofanya vibaya katika matokeo hayo, lakini wanatamani kuendelea na masomo, makala haya yanaangazia fursa mbalimbali wanazoweza kutumia ili kutimiza ndoto zao.

Wiki iliyopita Baraza la Mitihani Taifa (Necta), lilitangaza matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha nne wa mwaka 2016 na kueleza karibu asilimia 30 ya wahitimu wamefeli.

Ieleweke kufeli kidato cha nne si ishara mbaya maishani na wala haijawa sababu ya kuanza kuamini kuwa umeshafeli kimaisha.

Kwa kuzingatia ukweli kuwa wapo baadhi ya wanafunzi waliofanya vibaya katika matokeo hayo, lakini wanatamani kuendelea na masomo, makala haya yanaangazia fursa mbalimbali wanazoweza kutumia ili kutimiza ndoto zao.

Rudia mitihani

Njia mojawapo rahisi ya kurudisha matumaini ya ndoto zako za kusoma inawezekana kwa wewe kuamua kurudia mitihani yako kwa mara nyingine. Mfumo wetu wa elimu unatoa fursa hiyo ya kurudia mitihani na ndio maana kuna utaratibu wa watahiniwa binafsi.

Rudi tena darasani kusoma. Mathalani kuna shule nyingi za sekondari zenye programu maalumu kwa ajili ya watu wanaorudia mitihani ya kidato cha nne tena kwa bei rahisi. Zitafute shule hizi ila kuwa makini na vituo vinavyoitwa kwa Kingereza kama ‘Tuition Centers’ ambavyo vingi vinajali masilahi kuliko ubora wa elimu.

Kuna mtindo wa wanafunzi wanaofeli kidato cha nne na kuamua kuingia kidato cha tano huku wakirudia mitihani yao.

Hawa wanalazimika kusoma masomo ya mitihani wanayorudia huku wakisoma pia masomo mapya ya kidato cha tano.

Huku ni kujidanganya kwa mtindo huu, mwanafunzi mhusika hawezi kusoma kwa undani masomo ya kidato cha tano badala yake atakuwa anasoma kimtego mtego ili afaulu tu mitihani ya ndani.

Kibaya zaidi ni pale baadhi yao wanapofikia hatua ya kuzungumza na walimu wao wasiwape mitihani ya kidato cha tano kwa sababu tu wanakabiliwa na mitihani ya kurudia.

Soma ngazi ya cheti

Fursa nyingine iliyopo kujiendeleza ni kusoma fani mbalimbali zinazoanza kwa ngazi ya cheti. Ikumbukwe baadhi ya fani elimu ya cheti inatosha kuwa kipimo cha mtu kupata ajira.

Kwa mtu mwenye ndoto ya kusoma zaidi, kipato cha ajira kinaweza kutumika kama nyenzo ya kukuwezesha kuendelea na masomo ya juu.

Kwa mujibu wa mfumo wa elimu nchini, kuna vyuo vingi vya kada ya kati vinavyotoa elimu mbalimbali za astashahada ya msingi, ngazi ambayo ni maalumu kwa wahitimu wa kidato cha nne na cha sita.

Kutoka astashahada au cheti cha msingi, mwanafunzi anaweza kuendelea hadi ngazi ya cheti cha juu (advanced certificate), stashahada na hatimaye kupata fursa ya kusoma elimu ya chuo kikuu.

Hii inaweza kuwa safari yenye mzunguko mkubwa, lakini usishau msemo wa wahenga: mvumilivu hula mbivu. Wapo waliovumilia ujanani, lakini wakiwa ukubwani wanaburudika na matunda ya safari ndefu ya elimu waliyopitia. Hawa ni pamoja na wasomi na wataalamu mbalimbali waliopo serikalini na sekta binafsi.

Kwa walio makini mlolongo huu wa kusomea astashahada na stashahda unaweza kuwafikisha mbali. Wanaweza kufika chuo kikuu kwa kutumia njia hii ya kusoma. Vipo vyuo vikuu vinavyowakubali wanafunzi waliopitia mfumo huu. Vyuo hivi vina ithibati ya Baraza la Usimamizi wa Elimu ya Ufundi (Nacte).

Hata hivyo, ni vyema kutoa angalizo na vyuo vinavyotoa mafunzo kwa ngazi za cheti, kwani baadhi yao havina sifa na havitambuliki na Nacte. Kabla ya kujiunga na chuo chochote, tafuta taarifa zake katika baraza hilo, ikiwamo kupitia wavuti wao wa www.nacte.go.tz

Jiunge na Veta

Fursa nyingine inayotumiwa na baadhi ya wanafunzi wanaoishia kidato cha nne, ni kusoma masomo ya ufundi katika vyuo vinavyosimamiwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta).

Wengi wamekuwa na mtazamo hasi na vyuo vya Veta wanasahau kuwa vyuo hivi vina msaada mkubwa kiajira na hata kujiendeleza zaidi kielimu. Zaidi ya yote wigo wa mafunzo ya Veta umekua na kuhusisha mambo mengi ya kiufundi ya kisasa na yanayolipa kiajira iwe ajira binafsi au ajira rasmi. Hivi sasa Veta inaendesha kozi kama masomo ya madini, utalii, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Teknohama) na mengineyo muhimu katika zama za sasa.

Hakuna sababu ya kukata tamaa ikiwa bado una nafasi na fursa kedekede za kujiendeleza kielimu. Kama una ndoto ya kufanikiwa kielimu, fuata kilichosemwa katika makala haya utafanikiwa.

Elimu masafa

Uzoefu unaonyesha hapa nchini kuna watu wengi baadhi yao leo ni maprofesa maarufu waliowahi kufeli katika madaraja fulani ya kielimu siku za nyuma, lakini kwa kuwa tu walikuwa na dhamira ya dhati waliweza kujiendeleza na kufika kiwango hicho cha elimu kinachotamaniwa na kila mtu.

Watu hawa pamoja na wengine kuamua kuanza maisha ya familia au kikazi, bado walijiendeleza kupitia mfumo usio rasmi. Hawakukaa darasani bali walisoma kwa kutumia njia ya posta ambayo zamani ilikuwa maarufu.

Hii ndiyo inayoitwa elimu masafa inayotumiwa kwa kiwango kikubwa na watu wasiopata fursa ya kukaa darasani ama kwa kubanwa na kazi au kwa kuwa na majukumu mengine.

Elimu masafa ni mfano mmoja wa fursa za kielimu kati ya fursa nyingi wanazoweza kutumia wanafunzi waliofeli kidato cha nne, lakini bado wana ndoto za kujiendeleza kielimu, hasa ikizingatiwa kuwa elimu haina mwisho.

Kwa sasa taasisi maarufu za elimu masafa nchini ni pamoja na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) na Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT).

Kupitia vituo vya taasisi hizi vilivyosambaa kila kona ya nchi, uwezekano wa kujiendeleza ni mkubwa na hatimaye mtu anaweza akaifikia ndoto yake ya kupata elimu.