Fursa zilizopo kwenye uyoga zimemwezesha kujenga, kuajiri wengine

Muktasari:

  • Mbali na kujihusisha na kilimo hicho, Upendo anajihusisha na utengenezaji wa mbegu za Uyoga ambazo huziuza mikoani.

Hakuna njia rahisi ya kufanikiwa kama utaamua kujiajiri anasema Upendo Mhapa ambaye ni mkulima wa kilimo cha uyoga.

Mbali na kujihusisha na kilimo hicho, Upendo anajihusisha na utengenezaji wa mbegu za Uyoga ambazo huziuza mikoani.

“Sisemi ukiajiriwa hautapata mafanikio laa hashaa! lakini kwa upande wangu naona nikijiajiri ndio nitapata mafanikio yale ambayo nayataka kwa sababu itanifanya nisimamie biashara yangu kwa hali na mali” anasema Upendo.

Upendo, mama wa mtoto mmoja anasema yeye hakukata tamaa ndio maana safari yake haikuwa ngumu katika safari yangu ya kufikia malengo kupitia kilimo cha uyoga, nilichoanza kulima mwaka 2008” anasema.

Anabainisha kuwa “Niliona biashara ya uyoga inalipa na ndio sababu niliamua kupata mafunzo na hatimaye nikaingia rasmi katika kujiajiri kwa kulima na kutengeneza mbegu za Uyoga na kusafirisha mikoani” anasema.

“Shemeji yangu, alikuwa anafundisha jinsi ya kulima uyoga, ikabidi na mimi nijifunze kwa sababu nilikuwa nakaa kwake, hivyo namshukuru sana shemeji yangu maana alinionyesha njia na hatimaye nimefanikiwa kujiajiri mwenyewe kupitia uyoga” anasema Upendo.

Licha ya kujihususha na kilimo hicho, pia anafundisha wajasiriamali kuhusu kilimo hicho katika mikoa ya Mbeya, Arusha, Songea na Dar Es Salam na kwamba tangu mwaka 2014 hadi sasa ameshatoa mafunzo kwa vikundi vya wajasiliamali zaidi ya 50.

Usichokijua kuhusu uyoga

Anasema uyoga una tabia ya kuvuta harufu kama mtu amejipulizia pafyumu hatakiwi kuingia katika banda kwa ajili ya kuvuna uyoga kwa sababu uyoga utavuta harufu yake.

Vipi kuhusu soko la uyoga:

Soko la uyoga ni kubwa kwa sababu anauuza katika hoteli mbalimbali, maofisini na hata katika Supermaketi lakini wateja wake wakubwa pia ni wafanyakazi na wanafunzi wa Chuo Kikuuu cha Dar Es Salaa(UDSM), ambapo wananunua sana baada ya kupata mwamko kuwa uyoga ni tiba lishe.

“Nalima mifuko 1,000 na kuvuna kilo 10 hadi 15 kwa siku kwa muda wa miezi miwili hadi mitatu na kilo moja ya uyoga anauza Sh7,000 kwa bei ya jumla na rejareja ni Sh 10,000,” anasema.

Pia, hushiriki katika maonyesho mbalimbali ya biashara lakini kwa mwaka huu hakufanikiwa kwenda kwenye maonyesho ya nanenane kutoka na kuwa oda nyingi za kutengeneza mbegu walizokuwa wanataka wateja wake.

Anasema mara nyingi hupata oda ya kutengeneza chupa 1000 za mbegu za uyoga kwa muda wa wiki mbili, ambazo anasema sio kazi rahisi , kwa sababu “Unakuta mtu mmoja anataka mbegu za uyoga chupa 100 mwingine chupa 200 mwingine 500 kwa hiyo ukijumlisha unakuta ni oda nyingi ambazo zinatakiwa kwa wakati mmoja”anafafanua.

Anasema chupa hizo za mbegu humwingizia faida kwa sababu chupa moja ya mbegu ya uyoja huuza Sh 1800, hivyo kwa chupa 1000 anapata Sh 1.8milioni ndani ya kipindi cha wiki mbili na pia mbegu hizo zinauwezo wa kukaa kwa muda wa miezi miwili bila kuharibika zikiwa katika chupa.

Kwa upande wa kuuza uyoga, Upendo anasema ukipanda banda la uyoga lenye mifuko 1000, utavuna kilo 10 hadi 15 kwa siku katika kipindi cha miezi miwili hadi mitatu.

“Kwa hiyo hapo unapiga mahesabu kwamba kilo 10 kila siku kwa muda wa miezi mitatu, ni pesa ndefu, hivyo nawashauri wanawake wenzangu hata kama wanakazi nzuri, waende wakapate mafunzo ya namna ya kulima uyoga ili na wao waweze kujikwamua kiuchumi” anasema

Anafafanua kuwa , ukifika wakati wa mavuno, kila siku mkulima anauwezo wa kuvuna kilo saba mpaka kumi za uyoga kwa siku, kwa sababu ”kila wakati unapoingia bandani unakutana na uyoga umechuputa hivyo unauvuna.

Faida za uyoga katika mwili

Uyoga una chanzo kizuri cha madini ya chuma na shaba yanayohusika katika uwezeshaji wa usambaza wa hewa ya oksijeni mwilini, lakini Vitamini B2 inayopatikana kwenye uyoga, ni tiba kwa watu wanaosumbuliwa na ugonjwa wa kuumwa kichwa unaojulikana kama ‘kipanda uso’.

Kwa kula kiasi uyoga utajiweka kwenye nafasi ya kuwa na hali nzuri hususani kwa wale wagonjwa wa kipanda uso, lakini Vitamini B iliyopo katika uyoga, ina uwezo wa kuzuia uchovu wa mwili na akili hasa wakati wa kazi nyingi, huku Vitamin B3 husaidia kupunguza kiwango cha lehemu mwilini, wakati Vitamini B6 huondoa hatari ya mtu kupatwa na kiharusi au shambulio la moyo.

Pia, una madini ya zinki yanayoimarisha kinga ya mwili pia husaidia kuponya haraka vidonda si hivyo tu faida nyingine husaidia ukuaji mzuri wa seli za mwili, huimarisha kiwango cha sukari mwilini na kukufanya usikie ladha , harufu ya vyakula na vitu vingine ipasavyo. Hata hivyo wataalamu wa masuala ya lishe wanashauri badala ya watu kutumia nyama, wanatakiwa kutumia uyoga.

Aina za uyoga

Anasema kuna zaidi ya aina 13000 ya uyoga, lakini sio wote unaofaa kwa kuliwa ua kwa matumizi ya binadamu, lakini kwake yeye anazijua aina tatu za uyoga ambazo ni uyoga rangi ya pinki, kijivu (sajokajo) na nyeupe.

“Mimi nizalisha mbegu ya uyoga rangi nyeupe ambayo ndio unakubalika sokoni na wakulima wengi wanaipenda hivyo ninatenegeza kitu ambacho wakulima wanapenda” anasema

Changamoto

Uandaaji wa vimeng’enyo ndio changamoto lakini napambana kukabiliana na nalo.

Pia zamani alikuwa analazimika kupika uyoga na kisha kuwapelelekea watu waonje ndio watoe oda ya kununua , lakini kwa sasa anapeleka uyoga alioufungasha kwa wateja wao bila tatizo baada ya kuaminika na kujulikana.

Mafanikio

Kwa sasa amejenga nyumba, anamiliki viwanja vitano na amenunua shamba lenye ukubwa wa heka 10 ambalo amepanda miti.