Gesi itaongeza umuhimu wa Tanzania duniani siku zijazo

Muktasari:

  • Ongezeko hili la watu linapandisha matumizi ya nishati pia hivyo kuwalazimu wavumbuzi kukuna vichwa wakitafuta nishati iliyo bora zaidi kwa matumizi; ambayo haina madhara makubwa kwa binadamu na mazingira.

Idadi ya watu inazidi kuongezeka duniani kila siku siku. Mpaka Desemba mwaka jana, dunia ilikuwa inakadiliwa kuwa watu bilioni 7.6 huku idadi ikitarajiwa kuwa zaidi ya bilioni 11.8 mwaka 2100.

Ongezeko hili la watu linapandisha matumizi ya nishati pia hivyo kuwalazimu wavumbuzi kukuna vichwa wakitafuta nishati iliyo bora zaidi kwa matumizi; ambayo haina madhara makubwa kwa binadamu na mazingira.

Zamani, kabla ya kugundulika na kuanza kutumika kwa mafuta, makaa ya mawe yalikuwa yanapewa nafasi kubwa zaidi kwenye mitambu mikubwa. Lakini maoni ya wadau yanasema yanachochea uchafuzi wa mazingira hivyo teknolojia mpya kuhitajika.

Sasa hivi, kampuni kubwa za uundaji magari zinatengeneza modeli ambazo hazitumii kabisa mafuta. Mataifa makubwa kama Uingereza, yameshatangaza, kutoruhusu magari yanayotumia mafuta kuanzia mwaka 2040.

Kampuni kubwa zinajielekeza kwenye matumizi ya gesi iliyosindikwa (LNG), Tanzania ina hazina kubwa ya gesi asilia inayoizalisha.

Tangu uvumbuzi wa gesi hiyo ulipoanza mwaka 1974 katika Kitalu cha Songosongo, sasa kuna zaidi ya futi trilioni 57.25 za ujazo zilizopo hivi sasa.

Wadau wa nishati wanatafuta nishatiendelevu na nafuu. Kwa bahati nzuri, njia mbadala zipo. LNG, imedhihirisha kuwa mbadala kwani ni chaguo bora zaidi la nishati.

Tanzania inawajibu mkubwa wa kuendeleza uwekezaji katika miradi ya nishati kutokana na ukweli kwamba vyanzo vya asili kama vile makaa ya mawe na mafuta vinapungua.

Maana ya LNG

Japokuwa imekuwa ni sehemu kubwa ya mchanganyiko wa nishati mbalimbali kwa zaidi ya nusu karne sasa, gesi iliyosindikwa, yaani LNG si maarufu sana kama ilivyo mafuta, gesi asilia au makaa ya mawe. Hata hivyo, umuhimu wake unazidi kuongezeka siku hadi siku kama chanzo cha nishati duniani.

LNG ni kimiminika angavu, kisicho na rangi na ambacho sio sumu. Ni safi kwa kiwango cha juu sana kuliko nishati nyingine zitokanazo na visukuku au mabaki ya wanyama na mimea.

Kutokana na maendeleo ya teknolojia ya hivi karibuni kufanikisha uhifadhi na usafirishaji, nishati hii imeendelea kuwa chanzo cha uhakika duniani hata kwa nchi ambazo hazina visima vya gesi asilia.

Maendeleo ya teknolojia ya LNG yamefungua fursa kwa nchi zenye uwezo wa kusafirisha gesi hiyo sehemu mbalimbali duniani. Kwa nchi zilizojaaliwa hazina ya kubwa ya gesi asilia kama Tanzania, uwezekano wa muda mrefu wa kufanya biashara ni mkubwa.

Uhakika, usalama

Siku za nyuma, gesi asilia, inayopatikana kina kirefu chini ya ardhi, ilikuwa inatumika kwenye maeneo ilipogundulika na kuchimbwa ikiwa katika hali ya asili kabla ya kuchakatwa.

Njia pekee ya kusafirisha gesi hiyo iliyokuwa inafahamika ilikuwa ni mabomba, yaani kutandaza kutoka inapochimbwa mpaka itakakotumika. Kwa sababu hiyo, usafirishaji wake ulikuwa ni changamoto hivyo kupunguza uhitaji wake ikilinganishwa na mafuta au makaa ya mawe.

Kutokana na kutokuwa na visima vya kuchimba rasilimali hiyo, nchi nyingi zilikosa nia ya kuendeleza miundombinu inayotakiwa.

Hata hivyo, mwaka 1964, wanasayansi walipata ufumbuzi baada ya kugundua namna ya kuigeuza gesi hiyo kuwa kimiminika kwa kuipoza hivyo kuwezekana kuisafirisha kwenda mahali popote duniani.

Gesi asilia inapopoozwa hadi nyuzijoto sentigredi -162 hugeuka kuwa kimiminika ambacho hakishiki moto kwa urahisi, sifa inayofaa zaidi kwa usafirishaji wa masafa marefu. Ni rahisi kuihifadhi na hatari ya kutokea moto ni ndogo.

Pamoja na usalama wakati wa kuisafirisha, kupoza hupunguza ujazo wa gesi takriban mara 600, hupunguza gharama pia.

Ulikuwa ni ugunduzi mkubwa, kufanikisha matumizi ya gesi duniani kote. Yalikuwa mabadiliko ya haraka mno.

Maendeleo

Kiwanda cha kwanza cha LNG kibiashara kilijengwa Arzew nchini Algeria. ilikuwa mwaka 1964. Hii inamaanisha Afrika ni kitovu cha maendeleo ya LNG tangu mwanzo wa ugunduzi wa nishati hii.

Miaka 50 iliyofuata, pamekuwapo maendeleo makubwa ya LNG. Mwaka 2009 kwa mfano, Kampuni ya Shell ilianzisha Mradi wa Sakhalin LNG huko mashariki mwa Urusi ambako gesi iligunduliwa baharini karibu na Kisiwa cha Sakhalin wakati wa utawala wa Soviet.

Tangu ulipoanzishwa, Mradi wa Sakhalin umesambaza gesi inayohitajika katika soko la ndani hata kusafirisha nje kwa usalama na uhakika.

Kupanuka soko

Soko la LNG linakua na bila shaka mwenendo huu utaendelea kadri nchi nyingi zaidi zinavyoamua kutumia vyanzo vya nishati rafiki kwa mazingira. Makisio yanaonyesha, uhitaji wa gesi asilia duniani utaongezeka maradufu mwaka 2040.

Visima vipya vinahitaji kukidhi mahitaji jambo litakalopeleka neema nchi kama Tanzania. Maendeleo ya LNG yataambatana na uwepo wa gesi ya kutosha na ya gharama nafuu itakayoendesha mitambo ya kufua nishati na kuendesha viwanda nchini na nje ya Tanzania.

Mwandishi ni mchumi na mtaalamu wa masuala ya gesi asilia.