Ghassani: Nilianza kutunga mashairi darasa la nne

Mohammed Ghassani (kushoto) akipokea tuzo aliyoshinda mwaka 2015. Na Mpigapicha Wetu

Muktasari:

``Nyumbani oo nyumbani, kwetu ninakukumbuka

Gizani humu gizani, machozi yamiminika

Kwa nini hivi kwa nini, kwetu miye nikauka? ``

       Ulikuwa ni usiku mmoja, katikati ya giza na baridi kali, akaamka katika kijichumba chake, akalia peke yake na huku akijiuliza maswali yasiyo na majibu. Kisha akaketi na kuchukua kalamu, na kuanza kuandika ubeti huu wa shairi.

``Nyumbani oo nyumbani, kwetu ninakukumbuka

Gizani humu gizani, machozi yamiminika

Kwa nini hivi kwa nini, kwetu miye nikauka? ``

Hiyo ni sehemu ya ubeti wa shairi la Mohammed Ghassani, katika kitabu chake cha ´Nna Kwetu: Sauti ya Mgeni ugenini´

Ghassani, ni Mtanzania na mtunzi wa mashairi, mkazi wa Bonn, Ujerumani, ambaye mapenzi yake katika utunzi wa mashairi yamempa mafanikio hadi kupata tuzo ya kimataifa ya kazi za Fasihi ya Kiafrika iitwayo Mabati Cornell.

Alishinda tuzo hiyo mwaka 2015 baada ya kupeleka shairi lake la ´Nna Kwetu´ lililozungumzia maisha yake ugenini. Tuzo hiyo iliambatana na zawadi nono ya dola za Marekani 5000.

Alivyoanza ushairi

Safari yake ya upenzi wa ushairi hadi kupata tuzo ya kimataifa ilianzia visiwani Pemba, Zanzibar miaka zaidi ya 20 iliyopita. Anasema alianza kuyanakili na kuyasoma akiwa mwanafunzi wa darasa la nne.

``Nilikuwa nayasoma mashairi yaliyokuwa yanachapishwa katika magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Mfanyakazi,`` anasema

Alipofika darasa la nne, akaanza kuandika mashairi yeye mwenyewe, akifuatilia na kusoma kazi za washairi nguli kama Juma Balo, Zuhura Salehe na wengineo.

Kabla ya kushinda tuzo hii aliwahi kuwa mshairi bora wa Wilaya ya Wete Kaskazini Pemba, baada ya kutunga shairi bora zaidi katika mashindano ya kiwilaya.

Ghassani, ambaye kwa sasa ni mtangazaji na mhariri wa Idhaa ya Kiswahili ya DW, anasema mapenzi yake katika ushairi yalitokana na kupenda lugha.

``Nilijifunza Kiswahili, Kiarabu na Kiingereza, na zaidi hasa napenda kujisomea riwaya za Kiswahili na ninapenda kutafsiri,``anasema na kuongeza:

``Jambo lolote likitokea na nikahisi napaswa kutuma ujumbe wangu au kutoa maoni yangu, naweza kuyatoa kwa njia ya ushairi na si lazima nichapishe kama kitabu, lakini naweza hata kuweka katika mitandao ya kijamii, ndicho ninachopenda.``

Mpaka sasa Ghassani ameandika mashairi zaidi ya 3000, lakini yaliyochapishwa na kuwekwa katika vitabu ni matano likiwamo lililompa tuz, Nna Kwetu, Andamo, Siwachi Kusema na Kalamu ya Mapinduzi lililozungumzia uchaguzi wa Zanzibar wa mwaka 2015.

Mashairi yake mengi ni ya kimapinduzi, siasa na kwa uchache masuala ya kijamii.

Anasema maudhui yake yanalenga kubadili fikra za watu katika siasa, kwa mfano Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

``Ushairi wangu natamani kuwasilisha fikra zangu ili ziwe na maana katika jamii lakini isiwe kwa ubaya. Fikra zangu zidumu na ziache alama, `` anasema.

Diwani ya N’na Kwetu

Ukiisoma Diwani ya N´na Kwetu, utagundua kuwa Ghassani, ametumia Kiswahili fasaha. Licha ya kuwa baadhi ya misamiati ni migumu, lakini ameitafsiri,

Maudhui makuu katika diwani hiyo, ni maisha ya ukiwa ugenini lakini pia imeangazia safari yake kutoka Uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere hadi Ujerumani. Maisha yake Ujerumani na hata simanzi aliyokuwa nayo kwa kuiacha familia yake.

Kwa mfano katika shairi hili anasema;

``Khadhira hii safari, leo hii niendayo,

Usidhani nahajiri, naselemeya machweyo,

Sienendi hiyari, nendea makadirio,

Basi kiri pendo kiri, niuke nina radhiyo.``

Wanaomjua Ghassani, akiwamo Faraji Said, aliyesoma naye Chuo Kikuu cha Tumaini, hawashangazwi na tuzo hiyo.

Saidi, anasema alikutana naye kwa mara ya kwanza chuoni, mwaka 2006.

``Hatukuwa wanafunzi wengi katika darasa letu ilikuwa rahisi kufahamiana kwa haraka. Wakati tunazoeana na huyu bwana niligundua anaongea Kiswahili kwa ufasaha mkubwa, ikiwamo kutumia msamiati mzito. Kuna wakati niliwahi kumtania na kumwambia anapaswa kutunga nyimbo au mashairi, `` anasema Saidi

Anasema, katika kipindi alichofahamiana na Ghasani, hakuwahi kujua kama ni mshairi.

``Kwa kweli anastahili tuzo,kwanza anajua lugha vizuri ya Kiswahili, pili ni msomi na mtafiti mzuri, tatu ni mtu mwenye fikra na uwezo mpana wa kuchambua na kudadavua mambo mbalimbali,`` anasema

Anaongeza: ``Naamini kwa kuchanganya kipawa na uwezo alionao, vimemsaidia kuwa mtunzi bora wa mashairi. Akiendelea kutunga basi ataendelea kupata tuzo nyingi siku zijazo.``

Akizungumzia utunzi wa mashairi au kazi za fasihi kwa ujumla, Saidi anasema utamaduni wa mashairi umekufa na kumekuwa na mwamko mdogo kwa vijana kuandika au kusoma mashairi.

Wasifu wake

Ghassani alisoma Shule ya Msingi Pandani, Pemba. Akajiunga na shule ya sekondari ya Utaani, baadaye akahamia shule ya Fidel Castro, hapo hapo Pemba. Alipata diploma ya lugha katika Taasisi ya Lugha, akijikita katika Kijerumani, Kiswahili na Kiingereza.

Baadaye, akapata shahada ya Sanaa ya Uandishi wa Habari.