Guardiola: Muumini anayebadili rangi ya ngozi yake

Muktasari:

  • Mchana utakaokumbukwa zaidi katika klabu hiyo, siku ambayo kocha mpya asiyekuwa na uzoefu Pep Guardiola maarufu kama Pep alikuwa anatambulishwa kama kocha mpya wa klabu hiyo.

Mwaka 2008, klabu ya Barcelona chini ya Rais Joan Laporta na Mkurugenzi wa ufundi wa klabu hiyo, Txiki Begiristain ilikuwa inafanya uamuzi bora zaidi baada ya miaka 20.

Mchana utakaokumbukwa zaidi katika klabu hiyo, siku ambayo kocha mpya asiyekuwa na uzoefu Pep Guardiola maarufu kama Pep alikuwa anatambulishwa kama kocha mpya wa klabu hiyo.

Inawezekana ulikuwa uamuzi ambao ulinyanyua nyuso za watu wengi kwa sababu ya kocha aliyekuwa anaondoka, Frank Rijkaard, lakini kiuhalisia huu ndio uliokuwa uamuzi bora uliofanywa na Barcelona kwa kipindi cha miongo miwili tangu walipomteua kocha Johan Cruyff kuwa kocha wa klabu hiyo mwaka 1988.

Guardiola aliibadili Barcelona katika kile ambacho wengi hukisahau, na kushinda mataji 14 katika misimu minne tu huku pia akishinda kila fainali aliyofika isipokuwa moja tu ya Copa Del Rey iliyoamuliwa na bao la Cristiano Ronaldo.

Ni Pep huyu ambaye alishinda mataji 14 kati ya mara 19 alizoshiriki katika michuano yoyote ile kwa maana akikosa mara tano tu kati ya 19.

Huyu ambaye aligeuka kuwa kocha ambaye alifanikiwa zaidi katika historia ya Barcelona na kufunika hata nyota ya mkufunzi wake Johan Cruyff.

Inawezekana kabisa rekodi zote hizi zikawa matusi ya “nguoni” kwa kocha Jose Mourinho kwani kabla ya uteuzi wa Guardiola, Rais Laporta pamoja na mkurugenzi wake wa ufundi Begiristain walishazungumza na Mourinho na kumuahidi kuwa nafasi ya Rijkaard ingekuwa yake, uamuzi ambao usingeweza kushangaza wengi.

Lakini waliamua kucheza “kamari” kutokana na ushauri wa Johan Cryuff ambayo iliwalipa, waliweka mkeka ambao ulikuwa “jackpot” na pengine ambao unaweza usitokee tena katika kipindi ambacho kizazi cha sasa kitaendelea kupumua.

Ni ngumu kupata akili ya Guardiola, hasa kutokana na ukweli kuwa aliishi miaka yote akijaribu kuhitimu na kufaulu masomo ya Johan Cryuff na kuleta somo lake jipya kwenye soka.

Medulla Oblongata ya Guardiola ni aina ya kina Albert Einstein ambaye aliishi akiamini kuwa “tafakuri ni bora kuliko maarifa, kwa sababu maarifa yana ukomo au mwisho lakini tafakari inaizunguka dunia.”

Pep Guardiola alifahamu kuwa alifundishwa falsafa ya “Total Football” tangu akiwa mdogo na Johan Cryuff, falsafa ambayo Cryuff aliweza kuifahamu kupitia mbabe wa zama hizo Rinus Michel.

Kwa Guardiola, falsafa hii haikuwa na nguvu tena kwa sababu iliishi miaka takribani 40 tayari, hivyo wakati wake ukifika alitakiwa kuwa na kitu tofauti na ambacho kingeweza kumfanya aiweke dunia katika mabega yake na atoe amri ni wapi aitue ili afanye mengine.

Ndipo hapa ambapo kichwa chake kinachokiuka yaliyosemwa na wahenga kuwa akili ni nywele, kikauboresha mfumo na kulifanya jina la Tik-Taka kuwa maarufu kupindukia.

Guardiola alileta ladha tofauti na waliyofanya wengine na kusababisha dunia kuungana kutafuta majibu dhidi ya mitihani aliyoweka mbele yake ikiwemo mfumo maarufu wa Jose Mourinho wa “Park The Bus” ambao mara kadhaa uliwahi kujaribu kuwa jawabu la baadhi ya maswali ikiwemo ile Inter Milan iliyotikisa msimu wa 2009/2010.

Maisha hayakuwahi kuwa magumu kwenye moyo wa Guardiola, alikuwa na kikosi ambacho kila kocha alikitamani, alikuwa na kikosi ambacho kilikuwa na wachezaji watatu ambao ungeweza kuwapa uchezaji bora duniani wakati wowote na hakuna ambaye angelalamika, wakiwa ni Lionel Messi, Andres Iniesta na Xavi Hernandez.

Barcelona hii ambayo baada ya kumtetemesha Sir. Alex Fergusson pale Wembley na kisha yeye mwenyewe kukiri kuwa ni timu pekee aliyowahi kukutana nayo na “ikawaweka mafichoni” kwa wakati wote wa mchezo, ilikuwa imesajili wachezaji 14 tu mpaka Guardiola anaacha kuifundisha mwaka 2012.

Guardiola akiwa mwanafunzi bora wa Cryuff na akiwa ametokea kwenye timu ya vijana aliamini kuwa hakukuwa na ubora ambao angeweza kuutengeneza kwa kutumia wachezaji wa nje, yaani waliokuzwa kwa tamaduni tofauti.

Kwenye akili ya Guardiola, alikuwa anakumbuka namna Cruyff alivyotengeneza kikosi kilichoitwa “Dream Team” huku yeye akiwa miongoni mwa vijana waliopandishwa.

Guardiola alinunua wachezaji 14 peke yake, huku akipandisha wachezaji 22 katika kikosi cha kwanza ambao walimpa kila alichotaka. Vijana ambao angewaambia kuwa nimewafundisha soka bora zaidi duniani na wao wakatii.

Miaka ikaondoka zake, kama ilivyo ada, wakati huondoka na zama zake.

Guardola tangu hapo ameamua kutafuta maisha kwingineko akipita Bayern Munich ambako wengi wanaweza kupaita hakuna ushindani, na sasa yupo England panapoitwa Jehanamu kutokana na tabia ambayo klabu ya Burnley inaweza kufungua msimu kwa kuifunga Chelsea inavyotaka, kitu ambacho ni nadra kukikuta La Liga.

Guardiola aliamua kuja kuiaminisha dunia kuwa hakuna jangwa ambalo hawezi kuishi kwa sababu nundu yake ni imara.

Kwenye moyo wake hakutaka kubadili imani yake ya ngozi kutokubadilika, kwake aliamini angeweza kutumia vijana na maisha yakasogea.

Aliamini kila kitu kinawezekana na hakuna sababu ambayo Kelechi Ihenacho akashindwa kufanya kile ambacho Aguero anafanya kama akimfundisha.

Wazungu wanasema “too bad” wakati anafika, ndicho kipindi pia ambacho ligi kuu ya England ilikuwa inawapokea kikamilifu, Antonio Conte pale darajani na Chelsea, Jurgen Klopp akileta kumbatio lake Liverpool pamoja na Jose Mourinho katika klabu ya Manchester United.

Hawa wote ni washindi na hawa wote walitolea macho kile alichokitamani pia.

Wakati akiamini kuwa rangi ya ngozi haibadiliki, kikosi chake kilikuwa na wastani wa umri unaokaribia miaka 30 huku safu yake ya Ulinzi ikiwa imezidi umri huo. Hakuwa na vijana, na pamoja na kuwa falsafa zake zilianza vyema, baada ya muda misuli ya “wachezaji wake wa makamo” haikuweza tena kuhimili vishindo na maisha yakawa magumu.

Hao ndipo kengele ya kumbukumbu ilipogonga kichwani kwake, hapo ndipo alipogundua moto anaojaribu kuuzima na ni wakati huu alipopata majibu juu ya namna ambayo watu wengi bado wanamjaribu.

Akitizama mfumo wa klabu ya Manchester City iliyopo chini ya usimamizi wa ufundi Txiki Begiristain, mtu ambaye alimleta Barcelona, haufanani na Barcelona na hakuna vijana wengi wenye vipaji.

Medulla yake inayofanya kazi kwa kasi ya kipekee ikampa jibu moja tu, kuwa kwa sasa Kaisari kaachiwa ulimwengu wa soka autawale na kuwa watoto hawana nafasi kubwa kwa sababu fedha alizozisema Ben R Mtobwa, zinanuka harufu kali kweli.

Maisha mafupi, akayatafutia njia ya mkato, akaamua kubadili rangi ya ngozi, akasahau wazo la kupandisha vijana na kuamua kusajili kwa kiasi cha paundi milioni 220.

Sasa ameweka swali jipya na gumu zaidi, wakati timu inapambana na akili ya Guardiola ambayo inafanya kazi kwa kasi ya kipekee, unakuwa unapambana na fedha zilizokuwa nyuma yake pia. Maisha yamebadilika na Guardiola kabadili rangi ya ngozi yake.