HEKAYA YA MLEVI : Unajua hadi vumbi linauzwa?

Muktasari:

  • Tulipata madafu laini kama tulivyoagiza hadi mgeni alishangaa. Na mimi nikajigamba kuwa Mswahili hasahau asili. Alilifurahia lile dafu kiasi mchana ulipoingia aliomba chakula cha asili. Nilimpeleka kwa mama lishe na kumuagizia dona kwa perege chukuchuku, miksa kisamvu na kauzu.

Niliwahi kuulizwa na rafiki wa Kijerumani: “kinywaji chenu asilia ni kipi?” Nikamjibu “viko vingi: togwa, kosha, dafu…” Nilipomtupia jicho nikamwona naye ashanitupia la kwake. Haraka nilimuita muuza madafu. “Kata mawili laini, maji mengi”. Muuza dafu alitomasa madafu, akayatikisa na kukata.

Tulipata madafu laini kama tulivyoagiza hadi mgeni alishangaa. Na mimi nikajigamba kuwa Mswahili hasahau asili. Alilifurahia lile dafu kiasi mchana ulipoingia aliomba chakula cha asili. Nilimpeleka kwa mama lishe na kumuagizia dona kwa perege chukuchuku, miksa kisamvu na kauzu.

Alisuuzika kwelikweli. Lakini baada ya msosi alitaka kushushia soda ya kikwao iliyoitwa “Schweppes”. Nikamwambia kuwa hapa hiyo ni picha ya Kilatino. Labda tusogee pale Motel Agip ndo watamwelewa. Tulikwenda na tukaipata.

Nikamsoma vizuri Mdachi huyu. Alipiga vazi la “lederhosen”, gari yake ilikuwa “Volkswagen Audi”, alipoteremka akachomoa pakiti ya sigara ya “Reemtsma Imperior” na kibiriti cha “Erdgas”. Kila kitu kilitengenezwa nchini mwao. Bila shaka huyu mtu alikuwa akitembea na Taifa lake.

Wakati wote alikuwa akiusifu urafiki wa Ujerumani na Tanzania. Alisema kuwa huu ni mfano wa kuigwa kwa sababu marafiki wote wamekaza kwenye mapinduzi ya viwanda. Akatoa mifano ya jinsi Schweppes ilivyoendelezwa kutoka togwa hadi kinywaji cha biashara kimataifa.

Kwa upande mmoja yalikuwa madongo mazito kwangu. Sikujua nami ningeanzaje kujigamba jinsi tulivyoendeleza bidhaa asilia kwenye uwanja wa biashara. Ni kweli tulishawahi kusindika machicha ya nazi tukapata mafuta ya nywele, vifuu vya nazi kuwa sumu ya mbu na miti kuwa karatasi. Lakini ni lini?

Sikukubali kiurahisi. Pale Hotelini niliagiza soda ya Fahari. Hiyo ingetosha kufagilia kinywaji cha ridhaa cha maji ya machungwa kwenda kibiashara. Mhudumu aliniangalia mara mbili, kisha kwa kuwa niliambatana na mzungu alikwenda kumuuliza meneja. Nikajua mambo yashaharibika.

Aliporudi kunieleza kuwa hata yeye hakuwahi kukijua kinywaji hicho, niliagiza Schweppes kwa madai ya kuonja ladha asilia za wenzetu. Hata yeye si kaonjeshwa dona kwa kisamvu? Ngoma droo!

Lakini nilipigia mstari jambo hili; Moja ya njia za uhakika za kulipa kodi ni matumizi ya bidhaa mnazozalisha. Na hakuna nchi iliyoendelea bila uzalishaji. Na huwezi kuzalisha bila viwanda. Hata mzalishe tani trilioni za chakula, mafuta na madini, mkiuza ghafi ni kazi bure. Mkiuza ufuta bado mtalazimika kununua mafuta ya kula kulekule kwa bei ya kutisha pamoja na kodi.

Kwa hiyo mkigundua gesi nchini kwenu, harakisheni ujenzi wa viwanda vya gesi. Mtakapoiingiza mtamboni kuichuja mtaipata ikiwa na madaraja yake yote. Kwenye uchafu wa gesi mtavuna petroli, kisha mafuta ya taa, halafu dizeli. Bado utamu unakuja: baada ya dizeli mnapata oili, grisi na lami. Hadi uchafu unauzwa. La kwanza mtatumia mazao yenu kwa gharama nafuu sana. Ebu fikiria longolongo ya mafuta yanayotoka Arabuni kuuzwa bei nafuu Zambia kuliko hapa. Mafuta haya yanashukia kwenye bandari yetu na tunayasafirisha wenyewe kwa bomba la TAZAMA. Nina maana kuwa bidhaa mnayozalisha wenyewe hainaga longolongo.

La pili mtauza kila kitu kitokacho kwenye zao hilo. Mtakuwa na pato la uhakika kutoka kwenye kila kitu kama kilivyo. Kila zao linaposindikwa kunatoka kitu na kunabakia kitu. Hamtakimbizana na makirikiri… sijui nini… Unapokoboa mahindi unabaki na pumba ambayo ni malighafi katika kutengeneza Kangara. Upo hapo?

La tatu mtakuwa kwenye chati ya walalao hai kwa sababu ajira zitakuwa wazi kwa watu wenu. Mtafikia mahala hadi mtatangaza zawadi nono kwa wanaosapoti rasilimali watu. Tuzo kwa wazaao watoto zaidi ya kumi na tano, tofauti na hivi sasa ukizaa nane tu unaonekana mwanga!

Kutokea hapo Mtanzania ataweza kuota analishwa doriyani na watumishi bora kumi na wawili. Zile ndoto za kuzungukwa na mapaka meusi yenye macho mekundu zitatoweka. Hutayaota tena mazombi wanaokudai wakija na misumeno kugawana maini yako.

Mwendo wa kutoka kwenye kununua embe hadi kufika kwenye kuzalisha maembe si mwepesi. Lakini kama wewe ni mlaji haukosi kuwa na kokwa. Badala ya gharama za kutafuta na kununua kokwa, unaweza kupambana na jitihada tu na ukafanikisha.

Hivi sasa tunao wajasiriamali kwenye kila kona nchini. Kuna wauza lishe, sabuni, juisi, vipodozi na mahitaji mengi sana ambayo pale mwanzoni tuliagiza Ulaya. Lakini leo wauzaji hawa wanapata bidhaa hizi kutoka kwa wajasiriamali wanaozalisha bila mitaji mikubwa.

Serikali, wadau na taasisi za fedha wanaunga mkono jitihada hizi. Lakini kwa mshangao wanawapa mikopo midogo yenye riba kubwa kiasi cha kuwafanya kuwa watumishi wao. Hadithi kubwa ni rejesho: Umekopeshwa milioni mbili urejeshe laki tano kila mwezi kwa miezi minane! Sasa huu ni mkopo au mauaji?

Kama kweli tunataka Tanzania ya viwanda tuanze na hawa. Badala ya kuwakopesha fedha kiduchu kwa riba kibwena, tuwakopeshe viwanda vidogo na vitendea kazi bila riba. Kwani riba kitu gani bwana? Tunataka nchi iendelee au tunapenda kuhesabu vifaranga wakati koo angali mtamizi?

Kwa hili Serikali inaweza. Basi tu.