HOJA BINAFSI-Ilivyo Tomasa ya Tomaso

Muktasari:

  • Anayefuata kauli badala ya kitendo ameshindwa kazi lakini bado wengi wanaendelea kufuata kitendo maana unachoona kina nguvu sana kuliko unachokisikia. Wajanja wanaangalia kwingine ili wasione vitendo ndiyo maana wanaweza kufuata maneno tu. Huwa tunatania kwamba huu ni mchezo wa viongozi wa dini (fanya nisemalo si nitendalo) au hata waelimishaji wa masuala ya Ukimwi. Asubuhi, anahubiria umuhimu wa kondomu, usiku … dah!

Katika warsha zetu, tunapenda kucheza michezo mingi ili watu wachangamke na kuelewa kwa undani zaidi. Mchezo mmoja ni kuwaambia watu watende kulingana na maneno yetu huku tukifanya vingine. Kwa mfano tunawaambia wanyanyue mguu huku tunanyanyua mkono. Anayefuata kauli badala ya kitendo ameshindwa kazi lakini bado wengi wanaendelea kufuata kitendo maana unachoona kina nguvu sana kuliko unachokisikia. Wajanja wanaangalia kwingine ili wasione vitendo ndiyo maana wanaweza kufuata maneno tu. Huwa tunatania kwamba huu ni mchezo wa viongozi wa dini (fanya nisemalo si nitendalo) au hata waelimishaji wa masuala ya Ukimwi. Asubuhi, anahubiria umuhimu wa kondomu, usiku … dah!

Lakini, ninaona siku hizi viko vikundi vingi zaidi ambavyo vinastahili kutajwa. Fanya nisemalo, si nitendalo. Au kwa maneno mengine, amini nisemalo, si nitendalo. Amini unachosikia, si unachoona. Mtu akisema anapenda amani huko akimtwanga mtu mwingine, tutaamini tutakachoona tu. Ndipo hapo tunaona umuhimu wa tomasa ya Tomaso. Alipoambiwa kwamba Yesu amefufuka, hakuamini.

‘Mpaka nione, niguse … ndipo nitakapoamini.’ Na kwa Imani ya Wakristo, Yesu akajitokeza tena na Tomaso aliona. Aliweza kugusa ndipo akaamini. Yesu alisema.

‘Wewe umeona ndiyo maana umeweza kuamini. Heri wasioona lakini bado wanaamini.’

Lakini, wengine tunaona kwamba Tomaso ndiye mwanasayansi wa kwanza. Huwezi kuamini kwa kuambiwa tu. Lazima ufanye majaribio, uthibitishe. Uwe na ushahidi wa wazi. Na wanasiasa wengi, na wanaodai kuleta maendeleo wanajaribu kufuata mfano wa Tomaso. Amini mimi bora kwa sababu nimejenga shule. Ona shule pale. Ona madawati. Ona walimu. Wanajenga uhalali wao kwa vitu vinavyoonekana. Tukigusa kwa mikono, tutaguswa moyoni pia. Na ni vivyo hivyo katika haki. Wahenga walisema, haitoshi kutenda haki, lazima watu waone kwamba kweli haki imetendeka. Mengine yakifichwa, hawawezi kuamini kwamba haki imetendeka hata watu wakisema kwa sauti za malaika, na kadiri yanavyofichwa imani inazidi kupungua.

Hayo yote nilikumbushwa na baba yangu nilipoenda kumtembelea. Usidharau wazee wetu ambao, si tu wamekula chumvi nyingi bali wameona na kuchambua mengi. Na baba yangu kwa maswali duh! Baada ya kunitoa jasho na maswali yake kuhusu hayo na maneno na vitendo, akaamua kunikumbusha hadithi aliyokuwa anapenda kutuambia wakati sisi ni wadogo.

Hapo zamani za kale, wanyama walikuwa wamezoea maisha chini ya ufalme wa simba na chama chake cha AU (Amani na Ulinzi). Walijua simba ni wakali, walijua kwamba simba wanalindwa na tembo ambao wana nguvu sana, walijua kwamba simba waliungwa mkono na chui, na duma, na fisi pia na mara mojamoja waliona wenzao wakikamatwa na kuliwa na wote hawa lakini hawakuwa na shida sana maana kila mmoja aliamini kwamba yeye ni mjanja kuliko mwenzie. Walijifariji kwa kusema kwamba wanaokamatwa ni uzembe wao tu. Na kwa kuwa wanyama walikuwa wengi sana, mmojammoja akipotea siyo shida sana. Aidha hawakuwa na shida sana na tembo maana, ingawa walikuwa na nguvu, waliitumia zaidi kuwalinda wanyama wadogowadogo badala ya kuwakanyaga.

Hata hivyo, huwezi kuwa na jamii ambamo wote waliridhika hivyo mara akajitokeza kobe, mara nyati, mara swala mmojammoja na kuuliza kwa nini sisi wanyama tunakubali mfumo unaoruhusu wenzetu kuliwa bila hata hatia, ili wengine wanenepe tu. Kwa nini hatuwakemei hawa tembo wanapotukanyaga bila sababu? Kuna maana gani kutegemea makucha makali ya simba na wenzake dhidi ya maadui wa nje huku makucha hayahaya makali hutumika kuwararua na wao. Walithubutu hata kugeuza jina la chama cha simba liwe ni UA badala ya AU. Wanyama walio wengi waliwachukia hawa wabishi ambao wanathubutu hata kumhoji mfalme na kumsumbua wakati wanategemea atawaletea maendeleo, na ukweli ni kwamba hawa wabishi mara nyingi walikuwa wa kwanza kupotea bila kujulikana walipo au kuliwa hadharani lakini wabishi ni wabishi, wakazidi kuongezeka na walipoanza kuwa wengi mwisho waliweza kuunda umoja wao dhidi ya simba na wenzake. Kilikuwa ni chama hasa ya wanyama wala majani (WAWAMA)

Kumbe ni kweli zimwi likujualo, angalau katika maoni ya watu. Simba walizidi kutamba kwamba ni wao wameleta amani na maendeleo na hawa wengine wanataka kuvuruga. Tena walisisitiza kwamba wanapenda wanyama wala majani kuliko wanyama wala majani wenzao. Ndiyo maana wanyama wengine walizidi kuwaunga mkono, eti bora wachache kuliwa na simba kuliko wengi kupata njaa kutokana na umoja huu feki ya walafi wa majani wenye nia ya kujimilikisha majani yote tu. Sijui walipata wazo kwamba WAWAMA watakula majani yote, lakini ndivyo walivyoamini hivyo simba na wafuasi wao walizidi kuneemeka bila noma. Kuliwa si hoja ili mradi wanaona kwamba wanaweza kula majani vizuri.

Mambo yakaendelea hivyo huku, licha na vitisho na maneno mengi sana, WAWAMA ikazidi kupata wafuasi wengi walioamini kwamba dunia bila kuliwa inawezekana. Hata simba wengine walivutiwa na kutangaza rasmi kwamba wanajiunga na WAWAMA na kuacha ulaji wa wanyama wenzao kabisa. Hivyo kundi la wanyama wakali wakaona kwamba ni muhimu kumchagua kiongozi mwingine, simba mwenye msimamo mkali badala ya kuwaendekeza hawa wadai majani zaidi. Akachaguliwa hata na wala majani wengi kwa misingi kwamba atawakomesha simba wanaozidi kuwala na pia atahakikisha kwamba majani yataongezeka mara dufu ili kila mtu ashibe na kushibaga.

Na kweli alifanya hivyo na wanyama wote wakaanza kushangilia na kubeza WAWAMA kwamba hawana lolote. Hata wengine wa WAWAMA wakahama na kuonekana wanakula majani maalum kwa niaba ya wenzao. Wengi sana waliamini kwamba kweli, nchi ya ahadi ilikuwa imetimia.

Kilichowashangaza lakini ni kwamba ghafla, wakati simba wanajipongeza kwamba wanazidi kuleta maendeleo, wakati huohuo, wakaona kwamba maadui wa ndani wanazidi kuongezeka. Kwa kuwa wamedhamiria kuongeza majani, yeyote anayepinga au kuleta mawazo mbadala kuhusu njia bora ya kuongeza majani ni adui. Huko nyuma, wanyama walijua kwamba maadui wa ndani ni wale ambao wanazidi ulaji na kutafuna wanyama wenzao bila huruma lakini hali ya hewa sasa ikabadilika. Mara swala waliambiwa nyati ni maadui maana ni wahamiaji, mara nyati wakaambiwa kwama swala hawana maadili maana rukaruka yao haifai inaharibu maadili ya nchi yao, maana katika kurukaruka wanaonesha mambo ambayo hayatakiwi kuonekana. Mara kobe walishtumiwa kula majani mengi usiku na kukusanya wanyama wengine kuwaelezea kuhusu maisha ya huko nyuma. Mara lawama, mara shutuma, kisha ikaonekana wabishi walianza kuwindwa waziwazi. Kila WAWAMA wakijaribu kusimama, tembo wakaingia na kuwakanyagakanyaga na wengine kuwavunja. Na wale waliojaribu kuendelea wakawindwa na kundi la mafisi, hadi wengine waliliwa hadharani kabisa. Idadi ya wanyama waliopotea ikaongezeka mara dufu.

Hapo ndipo nchi ya wanyama ikaingia kwenye taharuki kubwa sana. Huko nyuma waliwalaumu wenzao kwa kuchokoza simba na kukosa mbinu za kujihami lakini sasa hofu ikatanda, kila kundi likijiuliza kama litapona. Katika hali hiyo, hata majani waliyokuwa wanakula yalipoteza ladha na wanyama walianza kukonda kwa wingi. Simba wakazidi kuwa wakali na kusema hata kukonda kwao ni ubishi kwa mfalme. Lazima wanenepe ili waoneshe shukrani kwa simba wao. Wakikonda sana hata ladha ya kuliwa inapotea.

‘Unakumbuka mwisho wa hadithi mwanangu?’

‘Hapana baba.’

Hata mimi lakini nakumbuka hadithi ilipotapakaa, wale viongozi wetu wa kijiji walibadilika maana walitambua kwamba maendeleo ya vitu bila watu kujisikia huru na salama hufanya maisha yapoteze ladha kabisa na kwamba kiongozi akitenda mema hana haja ya kuogopa mawazo mbadala. Badala yake ni changamoto ya kufanya vizuri zaidi.