JICHO LA MWALIMU : Haiba ya mwalimu inavyochochea ujifunzaji

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa kamusi mbalimbali za Kiswahili, haiba ni tabia nzuri, mwenendo wa kupendeza; haiba ni hali katika mtu inayofanya wengine wavutike naye ama mvuto wa heshima.
  •  Pia, haiba ni zile tabia zote za mtu ambazo huweza kumfananisha au kumtofautisha na mwingine.

Watu wengi wamekuwa wakichukulia haiba kuwa ni ule mwonekano wa kimavazi wa mtu.
Kwa mujibu wa kamusi mbalimbali za Kiswahili, haiba ni tabia nzuri, mwenendo wa kupendeza; haiba ni hali katika mtu inayofanya wengine wavutike naye ama mvuto wa heshima.
 Pia, haiba ni zile tabia zote za mtu ambazo huweza kumfananisha au kumtofautisha na mwingine.
Mtaalamu wa saikolojia, Christian Bwaya anaeleza kuwa haiba ni jumla ya tabia za mtu zinazotokana na kile anachofikiri, anachopenda, anavyojichukulia yeye mwenyewe, anavyowachukulia watu wengine na kadhalika.
Haya yote hujenga mwonekano wa mtu unaopimika (tabia) kama vile anavyoongea na watu, anavyodhibiti hasira zake, anavyovaa, anavyofanya maamuzi, anavyoweza kuwa mwaminifu, anavyoweza kutunza siri moyoni, anavyoweza kukabiliana na changamoto.
Kwa muktadha huo, haiba hujumuisha zaidi ya mwonekano wa nje; haiba ni mwonekano wa mtu kitabia, kimatendo, kimavazi na kimaongezi.  
Haiba huweza kubadilika kutokana na umri, mazingira na jinsi ambavyo mtu alilelewa na makuzi yake. Kuna mambo ambayo hufanya watu wakafanana haiba zao kama kuishi pamoja, mila na desturi, uhusiano wa familia na hata kusoma pamoja.
Pia, yapo mambo ambayo huweza kutengeneza haiba tofauti kama motisha anayopata mtu, mtazamo, uwezo wa akili wa kutafakari.
Haiba na ufundishaji
Mwalimu ana nafasi kubwa ya kuambukiza haiba yake kwa wanafunzi wake. Hivyo, haiba ya mwalimu huweza kuathiri tendo la ufundishaji na ujifunzaji darasani. Mwalimu anapokuwa na sifa zinazowavutia wanafunzi kama umahiri katika kufundisha somo lake, husababisha wanafunzi kupenda hilo somo na hivyo kulifanya vizuri katika mitihani.
Mwalimu mwenye utulivu wa mawazo na mwonekano mzuri, huzalisha wanafunzi wenye usawazo. Kinyume chake huambukiza na kuzalisha wanafunzi wasio na utulivu wa kifikra na mtazamo. Mojawapo ya kazi ya mwalimu ni kuhamasisha haiba zinazokubalika katika jamii kwa wanafunzi wake.
Tabia hujenga haiba ya mtu. Kwa mfano, mwalimu anayenyoa kiduku au anayevalia suruali kwa staili ya ‘mlegezo’ mbele ya wanafunzi wake huweza kuambukiza tabia hiyo kwa wanafunzi wake, ambao pia wakiunganisha na mbwembwe zao hali ya uvaaji shuleni na mitaani huwa tete zaidi. Pia, mwalimu anapotumia lugha ya staha huambukiza wanafunzi wake tabia inayofaa.
Kuna makundi mbalimbali katika jamii yanayopishana juu ya dhana ya umuhimu wa haiba katika taaluma ya ualimu.
Mathalani, wapo wanaodhani kwamba haiba haina umuhimu kama mwalimu anatekeleza tu jukumu lake la kuingia darasani na kufundisha na kuondoka. Tabia yake na mavazi yake hayana umuhimu.
Pia, lipo kundi la watu wengine ambao huona siyo vema kwa mwalimu kukosa haiba ya kiualimu. Hii ni kwa sababu haiba ya mwalimu husababisha mabadiliko chanya katika tabia ya mwanafunzi ambayo ndiyo lengo kuu la kujifunza.
Hivyo, ni vema walimu wakawa na tabia njema za kuigwa kuanzia wanavyoongea, wanavyotembea, wanavyowajibika na namna wanavyovaa yaani ule mwonekano wao wa nje.  Ikumbukwe kuwa  wapo wanafunzi ambao hujifunza hekima na utulivu wa akili kutokana na kile wanachokiona, kukigusa na kukisikia.
Umuhimu wa haiba ya mwalimu unabaki kuwa  muhimu bila kujali anafundisha ngazi ipi ya elimu. Kwa mfano, kuliwahi kutokea mhadhiri mmoja wa kike katika chuo kikuu kimoja ambapo mavazi yake hayakuwa ya staha kwa maadili ya Kitanzania na chuo kikuu hicho kiasi cha kusababisha hata wahadhiri wenzake kulalamika kuhusu mavazi yake.
 Cha ajabu alipoitwa na mkuu wa chuo na kuonywa kuhusu uvaaji wake huo, alimjibu kwamba yeye alikuwa ameingia mkataba na chuo wa kufundisha na si kumuamulia mavazi gani avae au asivae. Hili lilisababisha chuo  kuongeza kipengele cha haiba katika mkataba wao wa ajira.
Baadhi ya walimu wanaeleza kuwa baadhi ya changamoto wanazokutana nazo na kufanya kazi hiyo ionekane ngumu kwao na kutokuwa na mvuto, ni mazingira magumu na duni ya kufanyia kazi na idadi kubwa ya wanafunzi darasani.
Pia kuna tatizo la baadhi ya watu wasio na sifa ya ualimu kusomea fani hiyo, hawa wakisukumwa zaidi na sababu za kiajira.
Haiba pia huendana na  mtu kujitambua. Kujitambua ni hali halisi ya kuelewa kuwa mtu anaishi kama mtu binafsi na tofauti na mtu mwingine.
Kujitambua kunahitaji ukweli na uthubutu kuhusu mtu anavyofikiri, anavyohisi na kukubali ukweli anaouona kuhusu yeye.
Mwanzo wa kujitambua ni mtu kuelewa kuwa yeye ni mtu binafsi na tofauti, na kufahamu jinsi anavyohusiana na watu wengine pamoja na mazingira yake.
Kujitambua hutegemea jinsi mtu anavyojibu kwa uhakika maswali kama, “Mimi ni nani, niko wapi na  ninataka kwenda wapi maishani?”
Majibu sahihi na ya wazi kwa maswali hayo humwezesha mtu kupanga kwa urahisi mwelekeo wa maisha yake na kutambua uwezo alionao. Ni mtaji wa kumfikisha mtu katika mafanikio yake.
Mwanafunzi aliyejitambua hufahamu mwelekeo wa maisha yake na kuwa na dira ya kufikia malengo yake.  Hawi mtu dhaifu, na asiye na thamani. Hujitunza, hujiheshimu na kuheshimu wengine. Kutojitambua husababisha mtu kutokuwa na msimamo.
Hivyo, ni wajibu wa mzazi na mwalimu kumsaidia mwanafunzi ili ajitambue yeye ni nani, ameumbwa kwa makusudi gani na ana thamani gani?
Atambue kwamba yeye ni mtu wa pekee na wa thamani  machoni mwa Mungu; na hakuna binadamu aliyeumbwa kwa bahati mbaya, wala aliyelazimisha azaliwe na wazazi waliomzaa.
 Kitaaluma, mwalimu anawajibika kukuza haiba za wanafunzi wake kwa kuwajali na kukuza uhusiano mkubwa baina yake na wanafunzi, wazazi, familia, jamii na kada nyingine.