Haja ya kuwa na kalenda ya siasa kwa mwaka

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana akizungumza katika mkutano wa hadhara. Picha ya Maktaba

Muktasari:

Kalenda hiyo ibainishe pamoja na mambo mengineyo idadi ya mikutano ya lazima na muhimu ambayo vyama vya siasa inaweza kuendesha kwa mwaka

Kipindi cha miaka mitano ni kifupi katika uhai wa Taifa. Vyama vya siasa vilikuwapo, vipo, vitakuwapo, vitakuja na vitaondoka katika ramani ya ushindani wa kisiasa nchini, lakini Taifa la Tanzania litakuwepo na litaendelea kuwapo milele.

Katika siku za karibuni, Taifa letu limeshuhudia sintofahamu ya kisiasa kati ya Serikali inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Sintofahamu hii, inaashiria hali mbaya kwa mustakabali wa nchi yetu.

Migongano baina ya vyama vya siasa nchini visipewe nafasi katika kuifinyanga Katiba ya nchi na sheria zake kwa masilahi ya Taifa.

Katika kipindi hichi ambacho tumekuwa tukishuhudia majibizano ya tofauti za mawazo, misimamo na kiitikadi baina ya vyama vya siasa kuhusu hili na lile

Kila aina ya busara na ustahimilivu mkubwa vitahitajika kutoka kwa kila Mtanzania wa rika, jinsia na imani zote katika kuhakikisha Taifa letu linashikamana zaidi katika hali ya upendo, amani na utulivu.

Tuzidi kuwaombea viongozi wetu watangulize mbele maslahi mapana ya Taifa, wapate ujasiri mkubwa wa kustahimili tofauti za mawazo na wakubali kukosolewa kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.

Mwenyezi Mungu awajaze hofu yake na awape uwezo wa kuona mbali; wawe wepesi na tayari kusikiliza na kupokea maoni na mawazo ya Watanzania wenye kuitakia mema nchi yetu, bila kujali Mtanzania huyo katoka kambi gani ya mawazo na mitazamo ya kisiasa.

Ili kuondokana na purukushani za migongano hii ya tofauti za mawazo, misimamo ya kisiasa na tafsiri za Katiba na sheria za nchi ambazo zimekuwa zikiendelea kwa muda sasa, njia mojawapo inayoweza kututoa katika mkwamo huu wa kushindwa kuvumiliana kimawazo na kimsimamo, ni kwa vyama vyote vya siasa nchini kukubaliana.

Vyama vyote vya siasa nchini vikubaliane kwamba, ili nchi yetu iweze kuendesha ‘siasa za kistaarabu’, na kuipa Serikali iliyopo madarakani nafasi tulivu ya kutekeleza kile ilicho waahidi Watanzania wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita, upo umuhimu wa kuwapo kwa kalenda ya mwaka ya kitaifa ya shughuli zote muhimu za kisiasa za vyama vyote vya siasa nchini.

Ni kweli, Katiba ya nchi na sheria ya vyama vya siasa nchini imeeleza kwa uwazi na undani na umakini mkubwa nini kinachopaswa kufanywa na kila chama cha siasa katika kuendesha shughuli zake za kisiasa hapa nchini, bila kuvunja sheria za nchi, na bila kusubiri “hisani” ya mtu nje ya matakwa ya kikatiba na sheria za nchi.

Pamoja na kuwapo kwa maelekezo ya kikatiba na sheria, ninaamini kwa umuhimu wa kuwapo kwa kalenda ya mwaka ya kitaifa ya shughuli za vyama vya siasa nchini ili kuepusha misuguano na migongano isiyo na tija kwa Taifa, hatimaye kila chama cha siasa kione kinatendewa haki kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.

Hii ni pamoja na kuvipa vyama vya siasa nafasi ya kustawi na kujiimarisha katika ngazi za matawi kwa kuzingatia misingi ya demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini.

Kila chama cha siasa nchini lengo lake kubwa ni kuongeza idadi ya wanachama na wafuasi wake.

Wanachama wapya watapatikana kwa kukutana nao na kuwajengea ushawishi ili waridhie itikadi, sera na malengo ya chama husika.

Kazi hii haiwezi kufanyika bila ya kufanya mikutano ya lazima na walengwa au wanachama wapya watarajiwa.

Vyama vya siasa vitalazimika kuuza sera zake kwa walengwa au wanachama wapya.

Hii ni shughuli mojawapo muhimu ya kisiasa ambayo ni endelevu, lakini ni muhimu ikawekewa utaratibu maalum ili kuepusha migongano isiyo na tija kwa Taifa.

Nini kiwe kwenye kalenda?

Nitataja mambo machache yanayoweza kuwamo katika kalenda ya kazi za kisiasa kitaifa.

Katika harakati za kuhimiza maendeleo ya nchi ambayo hayawezi kufanywa na chama tawala peke yake na katika kujiimarisha kwa wafuasi wake katika dhana ya umoja wa kitaifa, kwa ridhaa ya pamoja, vyama vyote vya siasa vinaweza kuweka utaratibu wa kuendesha mikutano ya hadhara muhimu kwa uhai wa chama na masilahi ya nchi.

Kalenda inaweza kubainisha idadi ya mikutano ya hadhara inayoweza kufanywa na kila chama cha siasa katika mwaka; mikutano hiyo itafanyika wapi na nyakati zipi na kwa malengo gani.

Polisi na vyombo vingine vya usalama vitapata fursa ya kurekodi yote yatakayo hutubiwa katika mikutano hiyo, ili baadaye vyombo hivyo vya usalama vijiridhishe iwapo kilichotamkwa katika mikutano hiyo hakikuvunja sheria za nchi.

Mikutano hiyo itakuwa ile ya muhimu. Hatutarajii kuona mikutano ya hadhara ikiitishwa au kufanyika katika misimu ya kilimo au kila kukicha ni mikutano tu, hapana.

Mikutano inapaswa kufanywa, lakini je ni ile yenye tija kwa vyama husika na hata nchi kwa jumla?

Hofu ya wengi ni kuwa tusifanye mikutano na maandamano, kwa sababu tu wakubwa wa vyama wanataka hayo.

Lazima busara zitawale miongoni mwa vyama vya siasa. Mikutano mingine siyo lazima iwe ya hadhara.

Katika ulimwengu huu wa Tehama, vyama vya siasa vinaweza kufikisha ujumbe wake kwa wafuasi kupitia vyombo vya habari kama runinga au televisheni, redio, magazeti na njia nyinginezo.

Ridhaa hiyo ya pamoja ikipatikana, kila chama cha siasa kitawajibika kuzingatia taratibu zake bila kusababisha misuguano na migongano isiyo na tija kwa Taifa.