Hakimiliki kwa wasanii itainua uchumi na Pato la Taifa

Muktasari:

Hakimiliki ni sheria ambayo inampa msanii haki ya kumiliki kitu alichotengeneza au kubuni. Kitu hicho kinaweza kuwa kwenye mfumo au muonekano wa mchoro, picha, shairi au kitabu. Kwa kuwa kimetengenezwa au kumebuniwa, hakimiliki inampa msanii haki ya kuwa chake.

Msanii ni mtu yeyote anayefanya kazi za sanaa ikiwamo uigizaji, muziki au uimbaji, uchoraji, uandishi, utunzi na ubunifu tofauti.

Hakimiliki ni sheria ambayo inampa msanii haki ya kumiliki kitu alichotengeneza au kubuni. Kitu hicho kinaweza kuwa kwenye mfumo au muonekano wa mchoro, picha, shairi au kitabu. Kwa kuwa kimetengenezwa au kumebuniwa, hakimiliki inampa msanii haki ya kuwa chake.

Sheria hii inampa msanii haki ya kuzalisha, kuandaa, kusambaza, kutangaza na kuonyesha ubunifu wake kwa jamii. Hizi ni haki za msanii na ni zake peke yake.

Kwa ridhaa yake msanii anaweza kuhamisha au kuuza haki au sehemu ya haki kwa mtu au watu wengine. Bila kufanya hivyo, ni kosa kisheria kwa mtu au watu wengine kutumia kazi iliyobuniwa au kuzalishwa bila ridhaa ya aliyeibuni.

Sanaa kama zilivyo kazi zingine zinatoa elimu na burudani na hutatua changamoto ya ajira, huzalisha na kisha kuchangia uchumi wa nchi.

Shirika la Hakimili Duniani (Wipo), Chama cha Hakilimili Marekani (IIPA) na washirika wengine kwa kushirikiana na Serikali ya Marekani walianza kazi ya kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa sheria ya hakimiliki kwa wasanii wa nchi hiyo tangu mwaka 1984.

Mafanikio ya kazi yao yameendelea kuonekana. Ripoti ya IIPA ya mwaka 2016 inaonyesha kuwa mchango wa hakimiliki kwa uchumi wa Marekani umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka.

Mwaka 2015 hakimiliki zimechangia zaidi ya Dola 1.2 trilioni sawa na asilimia 6.88 ya Pato la Taifa (GDP). Katika upande wa ajira hakimiliki imechangia watu kupata kazi zenye hadhi na zinazolipa vizuri.

Zaidi ya watu milioni 5.5 wameajiriwa katika sekta ya sanaa sawa na asilimia 3.87 ya ajira zote nchini humo. Kuanzia mwaka 2012 mpaka 2015 sekta hiyo imekuwa ikikua kwa wastani wa asimilia 4.81 wakati uchumi wa Marekani ukikua kwa asilimia 2.11.

Mauzo ya hakimiliki za wasanii wa Marekani nje ya nchi yao yalifikia Dola 177 bilioni mwaka 2015. Mauzo hayo yanajumuisha muziki, filamu, tamthilia, haki za masafa ya runinga na video, vitabu, majarida pamoja na software za aina zote.

Mchango huo ni mkubwa kuliko mauzo ya bidhaa za kilimo ambazo ziliwaingizia Dola 62.9 bilioni na dawa zilizoingiza Dola 58.3 bilioni. Kwa mwaka 2015, mapato ya sanaa hasa kutokana na hakimiliki yalichangia Dola 2.1 trilioni sawa na asilimia 11.69 kwenye uchumi wa Marekani.

Ukiona takwimu hizo utapenda kufahamu hali ilivyo hapa nchini. Tanzania ina sheria ya hakimiliki kwa kazi za sanaa, lakini malalamiko makubwa yamekuwa ni namna sheria hiyo isivyo na makali kwa wezi wa kazi za sanaa. Kuwapo kwa sheria ni jambo moja na usimamizi wake ni suala jingine.

Ni vyema Serikali ikatambua kuwa hakimiliki kwa kazi za sanaa ni chanzo cha uhakika cha mapato. Marekani ni mfano mzuri wa mchango wa sanaa kwenye uchumi wa nchi, endapo kutakuwa na mifumo na mazingira mazuri.

Mwaka 2012 Wipo ilifanya utafiti juu ya hakimiliki nchini humo, lakini ripoti yake haifahamiki ilipo huenda ni Serikali pekee ndiyo inafahamu. Wengi wa wasanii wa Tanzania wana majina makubwa na hufanya kazi nzuri, lakini ajira zao na kipato kinachotokana nazo ni vitu viwili tofauti.

Ni wasanii wachache Tanzania wanaoweza kumudu kuendesha maisha yao ya kila siku kwa kutumia sanaa wanayoifanya pekee.

Aliwahi kuimba msanii mmoja kuwa, ‘sanaa isiwe daraja la kutengeneza maskini wenye majina makubwa.’

Ni wakati kwa Serikali kupitia na kuangalia upya mifumo yote inayotumiwa na wasanii kuanzia kubuni, kuzalisha, kutangaza na kusambaza kazi zao na kuziba mianya ya upotevu wa mapato.

Itengenezwe sheria mpya ya hakimiliki za kazi za sanaa ambayo itakuwa dawa na uponyaji kwa sanaa ya Tanzania. Siyo jambo la kufurahia kupata elimu na burudani kutoka kwa wasanii maskini ambao wangestahili kuwa matajiri na kuchangia mapato ya Serikali.

Hakuna utafiti uliofanyika kuthibitisha, lakini inakisiwa kuwa moja ya sababu za wasanii kujiingiza katika utumiaji wa dawa za kulevya ni msongo wa mawazo unaotokana na ugumu wa maisha wakati huo kazi zao zikiwatajirisha wengine.

Kwa kuanzia, tununue kazi za sanaa zilizo halali ili wasanii wapate kipato na Serikali ikusanye kodi. Pia, Serikali itunge sheria yenye makali kwani faida zitakuwa pande zote kwa msanii na Serikali.

Kukiwa na usimamizi makini kwenye kazi za wasanii ambao utazuia wizi wa haki zao, ajira zitaongezeka hasa kwa vijana na kuongeza uwezo wao wa kujitegemea.

Licha ya kuongeza ajira, ubora wa kazi pia utaimarika na kukidhi viwango vya kimataifa, hivyo kuitangaza Tanzania nje ya mipaka na kuongeza mapato ya fedha za kigeni kutokana na mialiko au mikataba itakayopatikana.

Changamoto kubwa ninayoiona ni kuchibiti uvujaji wa kazi hizo kwenye usambazaji.

Hili likishughulikiwa bila shaka mafanikio yatapatikana na kundi hili litaneemeka na kazi za mikono yake.