Wednesday, October 11, 2017

Hatari ya ukada katika utumishi wa umma

 

By Kelvin Matandiko, Mwananchi kmatandiko@mwananchi.co.tz

Wakati baadhi ya watumishi wa umma wakiwamo wakuu wa mikoa, wilaya na katibu tawala (DED), wameshinda uongozi ndani ya CCM. Chama hicho kimesema kitendo hicho ni kinyume na maelekezo yake.

Mbali na watumishi hao kukiuka maelekezo ya CCM, pia wametajwa kukiuka Kanuni za utumishi wa umma za 2014 zinazokataza watumishi kujihusisha na siasa.

“Kama kuna mtumishi wa Serikali amepenya kwenye nafasi yoyote ni vyema akachagua kuacha kazi serikalini na kubaki kuwa mjumbe au kiongozi kwenye chama. Tulishatoa maelekezo lakini baadhi ya watendaji hawakulisimamia vyema suala hilo hivyo ni vyema makada hao wakajitoa wenyewe,” ni kauli ya Makamu Mwenyekiti wa CCM, Taifa, Philipo Manguli alipozungumzia taratibu za uchaguzi ndani ya chama hicho.

Mangula alitoa kauli hiyo hivi karibuni alipozungumza na gazeti moja la kila siku nchini kuhusiana na uchaguzi ndani ya CCM.

Anasema zipo taarifa za watumishi wa Serikali waliogombea na kushinda kwenye uchaguzi wa CCM na jumuiya zake, jambo ambalo ni kinyume na maelekezo ya chama.

Pamoja na agizo hilo, Katiba ya Nchi, sheria na kanuni waraka katika Utumishi wa Umma zinapiga marufuku kwa mtumishi yeyote wa umma kujihusisha na siasa. Zuio hilo linatajwa kuanza miaka ya 1961 baada ya kupata uhuru.

Hata hivyo, matokeo ya uchaguzi wa viongozi ndani ya CCM yaliyotangazwa siku chache zilizopita yameibua mjadala baada ya baadhi ya wakuu wa mikoa, wilaya, katibu tawala na maofisa wengine wa taasisi za Serikali kushinda nafasi za ujumbe wa mkutano mkuu.

Watumishi wa umma walioshinda CCM

Waliotangazwa kushinda ujumbe wa mkutano mkuu wa CCM ni wakuu wa mikoa, Halima Dendego (Mtwara) na Dk Kebwe Stephen (Morogoro).

Wakuu wa wilaya waliogombea uongozi ndani ya CCM na kushinda ni Simon Odunga (Chemba), Christina Mndeme (Dodoma) na Elizabeth Kitundu (Bahi) wote hawa ni Mkoa wa Dodoma. Mkoani Morogoro wakuu wa wilaya waliongombea na kushinda ni Alhaji Mohamed Utaly (Mvomero) na Seriel Nchembe (Gairo).

Wakuu wa wilaya wengine walioshinda ni Raymond Mushi (Babati) mkoani Manyara, Herman Kapufi (Geita) mkoani Geita, Katibu Tarafa wa Makuyuni mkoani Arusha, Paul Kiteleki na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha Alexander Mnyeti. Katibu Tawala wa Wilaya ya Nanyumbu (DAS), Salum Palango naye alishinda nafasi ya ujumbe wa mkutano mkuu taifa.

Wengine ni mtumishi Idara ya Elimu Halmashauri ya wilaya Mvomero, Salvatory Richrd amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi wilaya hiyo. Dereva wa hospitali ya mkoa wa Morogoro amechaguliwa kuwa mjumbe wa halmashauri kuu ya wilaya Mvomero.

Wajumbe wengine waliochaguliwa Arumeru ni Mkurugenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), Elishilia Kaaya na Dk Daniel Mirisho.

Athari zake kiutumishi

Samweli Ruhuza, kada na Katibu Mkuu mstaafu wa NCCR Mageuzi anasema kama Rais John Magufuli anakubaliana na hali hii ya katibu tawala kuingia katika siasa, kuna hatari ya kudhoofisha maendeleo ya wananchi ngazi ya chini.

“RAS au DAS ni mtumishi wa umma, anaweza kutumikia Serikali yeyote itakayoingia madarakani, CCM ikiondoka anaweza kuendelea na nafasi hiyo kwa chama kingine kilichoingia madarakani, hii ni hatari sana, ni sawa na mwanajeshi asiyetakiwa kuingia kwenye uteuzi wa nafasi za kisiasa,” anasema Ruhuza.

Anasema uamuzi wa DAS aliyejitambulisha mjumbe wa CCM unaweka mipaka ya kutumikia wananchi kwa tofauti zao za kivyama.

“Kwa DC na RC tulikuwa tunakutana na kesi za upendeleo wa huduma, kwa mfano kama utakuwa na kikundi cha wajasilimali wenye kadi za CCM watapata mikopo kabla ya wale ambao hawatakuwa na kadi za vyama na katibu tawala hatakiwi kuangalia tofauti hizo,” anasema Ruhuza.

Pili anasema athari zilizopo kwa sasa zitaongezeka zaidi baada ya kuongezeka kada wa CCM ndani ya utendaji wa Serikali.

“Mkuu wa wilaya ni mjumbe wa Kamati ya siasa, huyu DAS naye anakuwa mjumbe wa mkutano mkuu wa chama ngazi hiyo, wakipewa maagizo ya kudhoofisha wapinzani lazima watekeleze kwa sababu nao wameshakuwa sehemu ya maslahi hayo,” anasema.

Anasema kiini cha kujitokeza kwa hali hii kunasababishwa na CCM kutokuwa tayari kukubaliana na mabadiliko ya mfumo wa vyama vingi vya siasa kwani utaratibu huo ulikubalika enzi ya chama kimoja.

Ruhuza anasema kitachotakiwa kufanyika ni kuhakikisha wananchi wanakemea ukiukwaji wa katiba na sheria za nchi,

NAENDELEA UK.18

INATOKA UK.15

kwa kuwa inaathiri kasi ya maendeleo ya watu. Anasema wananchi wengi maeneo ya vijijini hawafahamu ukiukwaji huo na matokeo yake wamekuwa wakiathiriwa wakati wa utafutaji wa huduma.

Hatari inayojitengeneza

Mkurugenzi wa Mipango na Utafiti kutoka Taasisi ya utafiti ya Repoa, Dk Abel Kinyondo anasema kuna uwezekano mkubwa wa watumishi wengi kuendelea kujihusisha na siasa kupitia mgongo wa utumishi.

“Kuna watumishi wengine watatumia nafasi zao kama stepping stone, kwa kufanya mambo fulani yanayoweza kuvutia chama bila kujali athari zake kwa umma. Tunafanya ‘time bombing’ na hatari kubwa itaonekana uchaguzi mkuu 2020 kwa wakuu wa wilaya, wakurugenzi na makatibu tawala wa wilaya kuwa sehemu ya makada na wakati huo huo kuwa wasimamizi wa uchaguzi,” anasema.

Dk Kinyondo anasema hali hiyo itaondoa imani kwa wagombea wa vyama vingine vya upinzani, hata kama watashindwa katika uchaguzi kuanzia ngazi za serikali za mitaa hadi Uchaguzi Mkuu wa madiwani, wabunge na urais.

Anasema tahadhari hii iliwahi kutolewa na Mwalimu Julius Nyerere baada ya kupiga marufuku kuchanganya siasa na shughuli nyingine za utumishi wa umma na biashara.

Dk Kinyondo anasema kwa hali itakayojitokeza kwa sasa, ni kuibuka kwa mivutano kati ya viongozi wa vyama vingine vya upinzani na watumishi wa umma wanaotumikia halmashauri moja.

Anatoa mfano wa halmashauri inayoongozwa na katibu tawala wa CCM huku ikiwa na uwakilishi wa Chadema katika ngazi ya jimbo na baraza la madiwani.

“Sasa hawa baraza la madiwani wakishajua DC, DED na DAS wote ni CCM, nini kitatokea?, ni vurugu na miradi mingi itakwamishwa kwa masilahi ya kisiasa, DAS atakuwa ameingia kwenye kundi hilo na kupoteza imani ya Serikali, hawezi kuaminiwa tena kama mtumishi wa umma,” anasema.

Katibu Tawala Wilaya ya Kilombero, Robert Selasela anasema kwa maoni yake kuna changamoto kwa mtumishi yeyote atakayefanya siasa katika mipaka ya halmashauri anayotumikia wananchi.

Selasela anasema Ofisi ya Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya, mamlaka yote yanakuwa kwa katibu tawala ikiwamo kufanya uhamisho, kushughulikia madai na kusimamia likizo. Anasema watumishi hao ndiyo washauri wakuu wa wakuu wa wilaya au mikoa.

“Mkuu wa wilaya au mkoa ni sawa kuchaguliwa CCM kwa sababu, Mkuu wa Mkoa ni mjumbe wa kamati ya siasa ndani ya mkoa na Mkuu wa wilaya ni mjumbe kamati ya siasa ya wilaya, siyo watumishi ila viongozi, hawana mamlaka ila wana madaraka tu lakini kwa katibu tawala kwa maoni yangu kutakuwa na shida akiingia katika chama ndani ya eneo la mipaka yake ya utumishi,” anasema Selasela.

Selasela ambaye amewahi kuwa diwani Morogoro vijijini anasema changamoto anayoiona ni katika mgongano wa masilahi ya utumishi wake na nafasi ndani ya chama. Anasema kwa mujibu wa kanuni na miongozo ya utumishi, katibu tawala ni mwenyekiti wa kamati ya rufaa katika uchaguzi ndani ya eneo lake husika.

Kwa maoni yake anasema licha ya Katiba ya nchi kutoa uhuru wa kila Mtanzania kuwa mwanachama wa chama chochote, katibu tawala atachaguliwa tu kuwa mjumbe nje ya mipaka ya halmashauri yake anayofanyia kazi na hakutakuwa na kizuizi ndani ya chama.

“Kwa mfano, Profesa Kitila Mkumbo alikuwa mtumishi wa umma lakini alikuwa Chadema, Katibu tawala wa wilaya ya Iringa ni mjumbe wa Nec ya CCM Taifa, Katibu tawala wa Wilaya ya Rombo, Abubakar Asenga ni mjumbe wa baraza la Umoja wa Vijana Taifa, mimi pia nilikuwa diwani Morogoro Vijijini, lakini nilikuwa mwalimu wa sekondari Mvomero hapo hakuna mgongano wa maslahi katika majukumu,” anasema.     

-->