Hatima ya ushindi wa Kenyatta kesho

Muktasari:

  • Huku mioyo ikigonga kwa sauti na wafuasi wake wakiingiwa na wasiwasi kwamba ushindi huo unaweza kutupiliwa mbali, Rais Kenyatta anaamini wakati huu atashinda kesi na kuendelea na mipango ya kuapishwa kwake Novemba 28.

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya anasubiri uamuzi wa mahakama kuhusu kesi tatu zilizowasilishwa kwenye Mahakama ya Juu ya nchi hiyo kupinga ushindi wake wa Oktoba 26.

Hii ni mara ya pili ushindi wa Kenyatta kupingwa ndani ya miezi mitatu tu.

Huku mioyo ikigonga kwa sauti na wafuasi wake wakiingiwa na wasiwasi kwamba ushindi huo unaweza kutupiliwa mbali, Rais Kenyatta anaamini wakati huu atashinda kesi na kuendelea na mipango ya kuapishwa kwake Novemba 28.

Mawakili wa Kenyatta walizikejeli kesi hizo wakisema hazina msingi wowote ule unaoweza kuhakikisha anarejeshwa nyumbani.

Mawakili hao Fred Ngatia na Ahmednassir Abdulahi walipuuza kesi hizo ingawa uchunguzi uliofanywa katika fomu namba 34A na 34B za matokeo zilizowasilishwa mahakamani zilibainisha makosa yanayodhihirisha kuwa uchaguzi wa Oktoba 26 haukuzingatia sheria za kuigia kura na Katiba.

Mawakili wa Jubilee na wa walalamikaji walimaliza hoja zao kuhusiana na kesi hizo. Sasa, majaji wa mahakama hiyo wameanza kuandika maamuzi yao ili wayasome kesho Jumatatu katika mahakama hiyo.

Mahakama hiyo ina majaji sita; Jaji Mkuu David Maraga, Naibu wake, Philomena Mwilu na Smokin Wanjala. Wengine ni Njoki Ndung’u, Jackton Ojwang’ na Isaac Lenaola.

Kupitia kwa wakili wake, Kenyatta alifaulu katika kupinga kuhusishwa kwa uchunguzi uliopatikana katika fomu 34A na 34B kwenye kesi hizo, wakisema hiyo itamaanisha kwamba kesi hiyo inawasilishwa upya kortini.

Kulingana na wakili wa walalamikaji, Donald Deya, fomu 15 kutoka majimbo matatu zilikuwa na mabadiliko yaliyoonyesha kuwa hesabu za kura zilibadilishwa baada. Majimbo hayo ni Kakamega, Samburu na Garissa.

Si hayo tu. Uchunguzi huo ulionyesha pia kuwa Rais Kenyatta aliongezewa kura zaidi kuliko zile alizopata. “ Tumegundua kwamba Kenyatta aliongozewa kura kwa mfumo maalumu wa kuongeza matokeo kwa 100, 200 na 300,” Deya akafichua.

Mmoja wa maofisa wakuu wa chama cha Jubilee, Winnie Guchu alisema fomu walizopokea awali zilikuwa zimepigwa muhuri lakini baadaye, fomu zingine za kughushi zililetwa zikiwa na matokeo tofauti.

Awali, mawakili wa Kenyatta ambaye ni mshtakiwa wa tatu, walikuwa wameomba mahakama watupilie mbali kesi hizo kwa sababu walalamikaji hawakupiga kura kwa hiari yao wenyewe na kwa hivyo hawana haki ya kuhoji ama kupinga matokeo yake.

“Walalamikaji wanataka kutumbukiza nchi hii kwenye mashaka na maafa na kuhujumu uchumi,” walisema.

Walalamikaji ni mwanasiasa Harun Mwau, mtetezi wa haki za kibinadamu Njonjo Mue na Khalef Khalif.

Mawakili wa Kenyatta wanasema mahakama haiwezi kutupilia mbali ushindi wake kwa sababu hakuna ushahidi kwamba uchaguzi haukufuata sheria.

Miongoni mwa sababu walalamikaji, wanataka ushindi wa Kenyatta uharamishwe ni Tume ya Uchaguzi (IEBC) kushindwa kuwateua upya wawaniaji wa urais kama inayohitajika kisheria.

Lakini mawakili wa Rais walisema kuwa zoezi hilo la kuwateua upya wawaniaji wa urais halingefanyika kwa sababu, msingi wa kura ya Oktoba 26 ni maamuzi ya Mahakama ya Juu ambayo ilitoa maamuzi yake Septemba Mosi.

Majaji wanapoendelea kutayarisha maamuzi yao, ni muhimu kufahamu kwamba kuna masuala makuu na mazito ambayo yataongoza hatua zao.

Mbali na IEBC kukosa kuwateua upya wawaniaji wa urais, kujiondoa kwa mwaniaji wa urais wa muungano wa Nasa, Raila Odinga kutoka katika kinyang’anyiro hicho, pia utakuwa msingi na muuhimu kwa maamuzi ya majaji.

Mbali na hayo, IEBC ilikosa kuandaa uchaguzi kwa majimbo 25 ya ubunge ilhali Katiba inasema kuwa uchaguzi wa urais lazima ufanyike katika maeneo Bunge yote (290) ya Kenya la sivyo, uchaguzi si halali.

Pia, kulingana na takwimu za IEBC, asilimia ndogo ya wapiga kura walijitokeza Oktoba 26 kupiga kura jambo linaloweka doa kwa ushindi wa Kenyatta.

Itakumbukwa kuwa Bunge la Kitaifa lilipitisha sheria mpya za uchaguzi siku chache kabla ya uchaguzi kufanyika Oktoba 26.

Hata hivyo, haitakuwa rahisi kwa majaji hao kutoa uamuzi wao kwa msingi wa sheria hizo.

Mawakili wa Rais Kenyatta, IEBC waliunga mkono sheria hizo huku wale wa walalamishi wakizipinga.

Mawakili wa Mue na Khalif wanasema sheria hizo ni haramu na zinaenda kinyume cha Katiba na pia haziwezi kutekelezwa na kutumika kwenye kesi yao kwa sababu zilianza kutumika Novemba 2, 2017 baada ya uchaguzi wa Oktoba 26.

Baadhi ya vipengee vya sheria hiyo mpya vinasema kwamba, Mahakama haina mamlaka ya kutoa uamuzi dhidi ya ushindi wa urais.

“Sheria hiyo ililetwa na Bunge makusudi ili izuie mahakama kutekeleza wajibu wake wa kuamua kesi za uchaguzi,” walilalamika.

Waliomba korti hiyo ipuuze sheria hiyo kwa msingi kwamba zinakinzana na Katiba ya nchi.

Lakini hayo yalipingwa na Mwanasheria Mkuu, Githu Muigai ambaye alisema sheria hizo ndizo zitakuwa vigezo vya kuamua kesi hizo dhidi ya ushindi wa Kwanza kabisa, Bunge la Kitaifa lilipitisha sheria mpya za uchaguzi siku chache kabla ya uchaguzi kufanyika Oktoba 26.

Haitakuwa rahisi kwa majaji hao kutoa uamuzi wao kwa msingi wa sheria hizo.

Kulingana na sheria hiyo kifungu cha 9, Mahakama hiyo haina mamlaka ya kutupilia mbali uchaguzi wowote kwa msingi kwamba haukuzingatia kanuni zozote zile ikiwa ni wazi kwamba zoezi hilo lilitekelezwa kikatiba.

Inaendelea kusema kuwa, ikiwa uchaguzi haukuzingatia Katiba, matokeo yake hayatatupwa ikiwa kwa kukosa kufanya hivyo, hakungeathiri matokeo.

Majaji wataangazia athari za Raila na mgombea mwenza Kalonzo Musyoka kujiondoa kwenye kivumbi hicho cha Oktoba 26 na ikiwa IEBC ingeahirisha zoezi hilo.

Mawakili wa Kenyatta na wa IEBC walisema viongozi hao wawili hawakujiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho bali walikisusia.

Wakati wa kusikiza kesi hiyo, majaji walikuwa wametofautiana na mawakili wa Kenyatta na IEBC wakisema kwamba, wakati Raila na Kalonzo walipojiondoa kulikuwa na wagombea wawili tu kwenye orodha ya wawaniaji wa kiti cha urais.

Walisema, wakati huo wagombea wengine (Ekuru Aukot na Cyrus Jirongo) hawakuwa wamewekwa kwenye orodha hiyo na hivyo kumwacha Rais Uhuru pekee kama mgombea.

Majina ya Aukot na Jirongo yaliwekwa katika orodha baada ya Raila kujiondoa. Wakili Mue anasema Raila alijiondoa Oktoba 10 wakati kulikuwa na majina mawili (Raila na Uhuru) kwenye orodha ya wagombeaji wa urais.

“IEBC ingefanya mpango wa kuwateua wagombea wapya wakati huo lakini hawakufanya hivyo,” akateta.

Huku Wakenya wakisubiri maamuzi ya mahakama, wafuasi wa Nasa wanaendelea kujitayarisha kufanya lolote wanaloambiwa na viongozi wao katika mazingara haya ambayo yamegubikwa na siasa za ukabila, chuki na wito wa kugawa Kenya.

Juzi Novemba 17 hali ilichafuka jijini Nairobi wakati wa mapokezi ya Odinga aliyerejea nchini Kenya kutoka safari ya siku 10 Marekani na Uingereza.

Licha ya kikosi cha polisi kuwazuia wafuasi wake kumlaki katika Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), wafuasi hao sugu wa kiongozi huyo walifurika eneo hilo na kumpokea kiongozi wao na kusababisha kutawanya kwa taabu kwa mabomu ya machozi na maji ya kuwasha.

Kulikuwa na mchezo wa kuwindana kati ya polisi na wafuasi hao katikati Jiji la Nairobi huku maduka na biashara nyingine zikifungwa kwa muda mfupi.

Nasa inasema imefanya mipango kabambe ya ‘kukomboa’ Kenya kutoka kwa minyororo ya Jubilee. Tayari kuna kundi linalotaka Keya igawanywe kulingana na makabila yanayomuunga mkono Kenyatta na lile la lodinga. Kwenye ramani isiyo rasmi iliyochorwa hivi punde, kabila la Rais Kenyatta (Kikuyu) limetengwa kutoka kwa sehemu nyingine mwa nchi hiyo mpya inayoitwa Jamhuri ya Watu wa Kenya.

Eneo la Pwani la Kenya tayari limeapa kuwa lazima litajitenga hata kama itachukua miaka 40.

Lakini pamoja na hayo, Kenya haiwezi kupasuka. Viongozi wanafahamu kuwa njia pekee ya nchi hii kujiendeleza ni kukuza haki na utangamano. Kwa hivyo, hawatakuwa na chaguo lingine ila kuketi pamoja na kujadili jinsi ya kuishi pamoja na kutenda haki kwa Wakenya.