Hatua za kuchukua unapoamua kuacha kazi -2

Muktasari:

Mtu mtulivu anayejitambua hafanyi maamuzi yanayoongozwa na hasira au hata furaha isiyo na kiasi.

Katika makala yaliyopita tuliona sababu za watu kuacha kazi na hatua za awali za kuchukuliwa na mtu anayefikiria kufanya maamuzi ya kuacha kazi. Tuliona ni muhimu kuwa na utulivu unapofanya maamuzi mazito.

Mtu mtulivu anayejitambua hafanyi maamuzi yanayoongozwa na hasira au hata furaha isiyo na kiasi.

Hutafuta ushauri wa kitaalamu ili kufikia maamuzi yanayotokana na uelewa sahihi wa mambo.

Kuna faida ya kuacha kazi kwa kufuata taratibu rasmi. Kwanza, inakusaidia kudai haki zako unazostahili kwa mujibu wa sheria.

Ili uweze kupata haki zako, ikiwa ni pamoja na mafao yoyote unayostahili kwa mujibu wa mkataba wa kazi, zitahitajika nyaraka rasmi kuthibitisha uliacha kazi.

Aidha, kuheshimu mkataba kunakuepusha na uwezekano wa kujiingiza kwenye matatizo baada ya kuondoka kazini.

Unapoondoka kienyeji kazini kwa sababu yoyote ile, mwajiri mkorofi anaweza kukuhesabu kuwa mtoro kazini na kukubebesha tuhuma za kuiba mali za ofisi zilizokuwa chini ya uangalizi wako.

Wapo wafanyakazi ambao, mara baada tu ya kupata kazi nzuri, waliondoka kwa mbwembwe na dharau kwa waajiri wao.

Wengine waliacha kazi kwa notisi ya saa 24 kwa kuamini hawana cha kupoteza tena. Haikuwa kama walivyofikiri.

Ondoka kazini kwa namna inayolinda uhusiano wako wa kikazi na mwajiri. Unaweza usione faida hiyo leo lakini baadaye uhusiano mbaya unaweza kukugharimu.

Mwajiri mpya anaweza kuwasiliana na mwajiri wako wa zamani kujiridhisha kama ni kweli uliacha kazi.

Kama hukuondoka kwa utaratibu, unaweza kujikuta ukipoteza kazi uliyofurahia kuipata.

Katika makala haya tunapendekeza namna nzuri ya kutoa taarifa ya kuacha kazi kwa mwajiri wako wa sasa na wafanyakazi wenzako.

Kutoa taarifa rasmi kwa mwajiri

Baada ya kujiridhisha kuwa umezingatia taratibu za kuacha kazi kwa mujibu wa mkataba, hatua inayofuata ni kufanya mawasiliano rasmi na mwajiri kuwa sasa unaacha kazi.

Siyo waajiri wengi wanaweza kufurahia kukutana na tetesi za mfanyakazi kuacha kazi kwenye vikao vya chai. Epuka kueneza taarifa hizo kabla hujawasiliana rasmi na mwajiri.

Taarifa rasmi ya kuacha kazi ni muhimu, kama inawezekana, itanguliwe na mazungumzo ya ana kwa ana na mwajiri.

Katika mazungumzo hayo, mwajiri wako anapata nafasi ya kuzipokea habari mbaya katika mazingira yasiyo rasmi kabla hajasoma barua rasmi.

Katika kuandika barua ya kuacha kazi, yapo mambo kadhaa ya kuzingatia. Mosi, ni kuweka wazi kuwa nia yako kuwa unaacha kazi.

Kwa mfano, barua yako inaweza kuwa na kichwa cha habari kinachosema;

‘YAH: KUACHA KAZI’.

Maneno kama, ‘Kuhama kazi’, ‘Kuchoka na mazingira ya kazi’ ‘Kubadili kazi’ yanaweza kuwa na tafsiri nyingi. Epuka maneno yenye tafsiri nyingi.

Baada ya kuainisha lengo la barua yako, andika sentensi inayotaja tarehe ya mwisho ya kufanya kazi na mwajiri wako.

Kwa mfano, ‘Ninakuarifu kuwa baada ya kutafakari kwa kina, kwa hiari yangu, nimeamua kufanya maamuzi ya kuacha kazi ili kupata fursa ya kujiendeleza kimasomo. Siku ya mwisho kufanya kazi inategemewa kuwa Ijumaa ya tarehe 31/3/2017.’

Baada ya kutaja siku ya mwisho kufanya kazi, shukuru kwa kutambua mchango wa mwajiri wako katika kuboresha ujuzi wako.

Taja kwa ufupi fursa ulizopata tangu umeanza kazi unazoamini zilizokujenga kiuweledi na kiuzoefu.

Inawezekana kweli kuna mambo hukuyapenda katika kampuni/taasisi unayoondoka. Labda ulikuwa na mgogoro na mkubwa wako wa kazi.

Huu si wakati wa kulalamika wala kukumbushia maumivu yaliyopita. Tumia lugha chanya isiyoonyesha hisia hasi.

Sambamba na hilo, epuka kumtaja mwajiri wako mpya wala unakokusudia kwenda. Mwajiri haitaji kujua mipango yako baada ya kuachana nae.

Malizia barua yako kwa kuomba kujulishwa taratibu zozote za makabidhiano ya ofisi.

Malizia barua yako kwa kuomba kujulishwa taratibu zozote za makabidhiano ya ofisi.

Unaweza pia kuonyesha uko tayari kwa usaili wa kuacha kazi kumpa fursa mwajiri kukudadisi sababu zilizokufanya uondoke; namna utakavyopewa haki zako; utaratibu wa makabidhiano ya ofisi; utayari wako katika kumsaidia mtu mpya atakayepatikana kuchukua nafasi yako na mambo mengineyo.

Kuwajulisha wafanyakazi wenzako

Baada ya makubaliano rasmi na mwajiri wako kwamba sasa unaacha kazi, kinachofuata ni kuwajulisha wafanyakazi wenzako.

Taarifa kuwa sasa unaondoka zinaweza kuibua hisia za wivu. Unapowajulisha, heshimu hisia zao.

Ni kweli umeacha kazi na unakwenda mahali bora zaidi. Pengine hata wafanyakazi wenzako wangependa kwenda huko unakokwenda wewe.

Usiwafanye wajione hawana mahali pa kwenda kwa kuendelea kubaki na mwajiri unayeachana naye.

Huna sababu ya kufanya majigambo ya maneno na vitendo kabla na baada ya kuondoka kwenye kituo cha kazi.

Hakuna sababu ya msingi kueleza kwa nini umeondoka na kwamba unakokwenda kuna maslahi zaidi.

Pia, usihatarishe uhusiano wako na mwajiri unayemwacha kwa kumsema vibaya kwa wafanyakazi unaowaacha. Hata kama ni kweli ana upungufu wake; hata kama mazingira ya kazi unayoyaacha hayafai; huna sababu ya kuyaeleza hayo kwa wafanyakazi unaowaacha.

Sema maneno chanya. Toa sababu za kawaida kwa nini unaondoka. Ondoka kwa namna ambayo itakufanya uendelee kuwa na uhusiano mzuri na hao unaowaacha. Kumbuka kuna kesho!

Mwandishi ni mhadhiri wa saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge. 0754 870 815