Hatua za kufuata unapomfundisha mtoto kusoma -2

Muktasari:

  • Jambo hili linasisitizwa na matokeo ya utafiti mwingi unaochunguza mazingira ya ujifunzaji.

Mzazi ndiye mwalimu wa kwanza wa mtoto si tu kwa masuala yanayohusu maisha kwa ujumla, lakini pia kwa mambo yanayohusiana na masomo.

Jambo hili linasisitizwa na matokeo ya utafiti mwingi unaochunguza mazingira ya ujifunzaji.

Utafiti mathalani, unaonyesha kuwa mzazi, bila kujali kiwango chake cha elimu, anayo nafasi nzuri mara dufu ya kuhakikisha mwanawe anajenga uwezo wa kusoma na kuandika kuliko hata mwalimu wa darasani.

Maana yake ni kwamba mtoto anayekutana na mazingira duni ya kielimu nyumbani, ana uwezekano mdogo wa kuwa msomaji mzuri hata kama anafundishwa na mwalimu mzuri shuleni.

Msomaji mzuri anakwenda mbele ya uwezo wa kutambua maneno na sentensi, kama anavyoeleza Doris Lyimo, mhadhiri wa lugha, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU):

“Baada ya mtoto kujenga uwezo wa kutambua maneno yanayoleta maana, lazima mzazi atengeneze mkakati madhubuti wa kukuza uwezo wake wa kuelewa na kuchambua kile anachokisoma. Mara nyingi mkakati unaotumika kumfundisha mtoto kusoma unategemea lengo.”

Anaeleza malengo matatu ya kusoma. Kwanza, burudani. Hapa mtoto halengi kupata maarifa ya kina isipokuwa uelewa wa jumla. Pili, kusoma kwa lengo la kujenga ufahamu wa kina kwa jambo fulani. Tatu, kusoma kwa lengo la kuchambua ukweli au uhalisia wa kile anachokisoma.

Kusoma kwa burudani

Kwa mujibu wa Lyimo, si mara zote tunasoma kupata maarifa ya kina kuhusu suala tunalolisoma. Wakati mwingine tunasoma kwa lengo la kuburudika, kwa maana ya kufurahia kile tunachokisoma.

Aina hii ya usomaji inalenga kumkaribisha mtoto kupata ujumbe wa jumla tu na si kumtaka kupata undani wa kile anachokisoma.

Namna nzuri ya kukuza uwezo wa kusoma kwa njia hii ni kumpa mtoto vitabu vya watoto vyenye picha na simulizi fupi fupi.

“Kuna vitabu vya watoto vinakuwa na visa vya kutisha. Mfano simba anamvamia sungura na kumuua. Simulizi kama hizi ni muhimu katika kukuza maadili hata kama hazimsaidii sana mtoto kuelewa jambo kwa undani,” anasema.

Kusoma hadithi kama hizi kunamsaidia mtoto kutambua yale asiyotakiwa kuyafanya katika maisha halisi. Kupitia wahusika wanaochorwa wakifanya vitendo hivi vya kikatili, mtoto anajifunza kupambua mema na mabaya; anajifunza ujasiri na wakati mwingine uvumilivu.

Tunachokiona hapa ni kwamba mtoto anaposoma hadithi kama hizi, haitegemewi kuwa atajenga uelewa mpana wa jambo bali kujifunza kitu cha jumla kitakachomsaidia kwenye maisha yake.

Lyimo anashauri mzazi kumuuliza mtoto maswali mepesi kupima kile alichojifunza. Anasema: “Muulize mtoto kitabu alichosoma kinahusu nini. Unapofanya hivi unamsaidia kurejea kwenye ujumbe aliousoma kitabuni.”

Kusoma kwa undani

Katika aina ya pili ya usomaji, mtoto anasoma kwa minajili ya kulielewa jambo kwa kina. Hapa husomi ili kupata ujumbe wa juu juu pekee, bali kuelewa undani wake.

Kuna namna mbili za kupata undani wa jambo kama anavyoeleza Lyimo: “Namna ya kwanza ni kumfanya mtoto atumie uzoefu alionao kujaribu kuelewa kile anachokisoma. Lengo ni kuoanisha yale anayokutana nayo kwenye maisha yake na maandishi anayoyasoma.”

“Namna ya pili ni kujifunza vitu vidogo vidogo vinavyohusiana na lugha ambavyo hatimaye vitamsaidia kuelewa ujumbe wa kisa anachokisoma.’’

Mtoto anaweza kuulizwa misamiati na misemo iliyotumika kwenye hadithi anayoisoma na hiyo inamsaidia kuelewa ujumbe mkuu.”

Mbinu zinazopendekezwa kumsaidia mtoto kuelewa jambo kwa undani, ni kumwekea mazingira ya kujenga motisha ya kusoma kwa kuhusianisha uzoefu alionao kama anavyoeleza tena Lyimo:

“Unaweza kuanza kwa kumuuliza mtoto kitabu anachokwenda kusoma kinahusiana na nini. Lengo ni kujua ana uelewa gani kabla hajasoma hadithi husika. Baada ya hapo unaweza kumpa maswali yanayomuongoza katika usomaji.”

“Kinachofuata unamwacha asome. Akishasoma unamtaka ajibu maswali yale ya awali. Hapa ni muhimu na wewe mzazi uwe kweli umesoma kile unachotaka asome, ili ubaini wapi hajaweza kujibu sawa sawa na umsaidie kufanyia kazi yale ambayo hakuweza kuyajibu.”

Sambamba na kukuza uwezo wa kuelewa jambo kwa undani, kasi ya kusoma nayo ni muhimu. Lyimo anashauri wazazi tuwape watoto kazi za kusoma kwa muda fulani.

“Mpe dakika kadhaa asome hadithi halafu apate muda wa kuja kuhadithia kile alichokisoma,” anasema. Tunachojifunza hapa ni umuhimu wa mzazi kuwa mfano katika usomaji.

Huwezi kumpa mtoto kazi ambayo wewe mwenyewe huifanyi. Ili uwe mfuatiliaji wa karibu unayeweza kujenga tabia ya usomaji wa kina, lazima kwanza wewe mwenyewe uonekane kweli ni mfuatiliaji wa mambo.

Kusoma kwa kujenga udadisi

Haitoshi kuelewa jambo kwa kina. Ni muhimu mtoto ajenge uwezo wa kutathmini kile anachokielewa.

“Si kila kilichoandikwa huwa ni sahihi. Kuna wakati hadithi zinakuwa na visa vyenye utata na mtoto anahitaji kuwa na uwezo wa kubaini uongo na ukweli, uhalisia na mambo ya kufikirika yasiyokuwepo katika maisha ya kila siku,” anaeleza.

Tafsiri yake ni kuwa msomaji mzuri haishii kukubali kila kilichoandikwa. Lazima awe na uwezo wa kuhoji ambao kimsingi ndio unazalisha tabia ya udadisi ndani ya mtoto. Udadisi, ndio msingi wa uwezo wa kuchambua mambo kwa kina.

Unachoweza kukifanya kama mzazi ni kumtafutia mtoto hadithi zisizo na majibu ya moja kwa moja kama anavyoshauri Lyimo;

“Msaidie mtoto awe na taarifa zinazohusiana na maisha tunayoyaishi. Taarifa hizi zinajenga uelewa wake na zitamsaidia kufanya maamuzi ya kile anachokisoma.”

Anaongeza: “Mpe hadithi zisizo na jibu moja. Tafuta hadithi zenye wahusika wenye mwenendo unaofanya iwe vigumu kuamua ikiwa walichofanya ni sahihi ama la. Lengo kubwa la kufanya hivi ni kumsaidia mtoto atafakari kisa kwa kina na kuelewa pande mbili za jambo.”