Haya yanakatazwa kabla na wakati wa uchaguzi

Wednesday February 7 2018

Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi Tanzania (NEC)

Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi Tanzania (NEC) Jaji SemistoclesKaijage akizungumza wakati wa mkutano na vyama vya siasa . 

Kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge katika majimbo mawili ya Kinondoni na Siha na katika kata tisa zimepamba moto kutokana na wagombea wa nafasi hizo na wafuasi wao kuwa katika hekaheka za kujinadi.

Ni katika kampeni hizo, Watanzania wameshuhudia lugha kadhaa zikitolewa na wafuasi wa vyama vya siasa ambao wanapanda kwenye majukwaa kwa ajili ya kunadi wagombea wao ili kuwaleta ushawishi kwa wapigakura.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeona ni wakati bayana wa kuwakumbusha wadau wa uchaguzi maadili ya uchaguzi yanayowaongoza katika kampeni za ubunge na udiwani ambayo vyama vyote vinavyoshiriki kwenye uchaguzi huo viliyasaini katika uchaguzi uliofanyika Novemba 2015.

Haya ni maadili yaliyowekwa na pande tatu ambao ndio wadau wakuu katika uchaguzi ambao ni vyama vya siasa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Serikali ambao kwa pamoja wamekubaliana kuwa na uchaguzi huru, wa haki na uwazi na wa kuaminika.

Haya ni maadili ambayo lengo lake ni kulinda amani, ustawi wa nchi, usalama wa raia, uhuru wa vyama vya siasa, utii wa sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi kwamba ndio msingi wa uchaguzi ulio huru, haki na wenye kuzingatia ushiriki wa makundi yote ya jamii katika uchaguzi.

Vyama vya Siasa

Katika maadili hayo viongozi wa vyama vya siasa, wagombea wao hawatakiwi kufanya fujo au kusababisha vurugu ya aina yoyote katika mkutano wa chama kingine. Pia, hawatakiwi kutumia lugha ya matusi, kashfa, kejeli, udhalilishaji na vitisho au lugha inayochochea uvunjaji wa amani au kuashiria ubaguzi wa kijinsia, ulemavu au maumbile kwenye mikutano ya kampeni.

Maadili yanakataza mtu yeyote kuwa na silaha yoyote ikiwa ni pamoja na silaha za jadi au zana yoyote inayoweza kumdhuru mtu katika mkutano wa kampeni au mkusanyiko wowote wa kisiasa.

Hairuhusiwi pia kubeba sanamu, kinyago au kitu chochote ambacho kinaonesha kudhalilisha, kukebehi au kufedhehesha chama kingine cha siasa au kiongozi wake au Serikali katika mkutano au mkusanyiko wowote wa kisiasa.

Ni katika maadili hayo viongozi wa vyama vya siasa na wafuasi wao hawaruhusiwi kutumia vipaza sauti vya aina yoyote ile kwa shughuli za kisiasa nyakati zote za usiku kuanzia saa mbili usiku hadi saa 12 asubuhi. Hairuhusiwi pia kuchafua, kubandua au kuharibu matangazo ya kampeni ya vyama vingine vya siasa, matangazo ya uchaguzi yanayotolewa na NEC.

Vyama vya siasa pia vinakatazwa visibandike mabango ya kampeni, matangazo au mchoro wowote kwenye nyumba, majengo au vyombo vya usafiri vya watu binafsi au taasisi mbalimbali bila idhini ya wamiliki husika.

Katika maadili hayo wapiga kampeni wanaelekezwa kuwa kukosoana kati ya vyama na wagombea kunapofanyika ni lazima kujikita katika sera, programu na kazi zao walizofanya. Ukosoaji wa vyama vingine au wagombea wengine kwa tuhuma zisizothibitishwa ni lazima uepekwe.

Wakati wa kampeni pia inakatazwa wagombewa kuomba kura kwa msingi ya udini, ukabila, jinsia au rangi. Wahusika pia wanaaswa kuepuka kutumia rushwa au shukrani ili kumshawishi mtu kusimama kama mgombea au kujitoa ugombea wake. Vyama pia vinatakiwa visiwazuie watu kuhudhuria mikutano ya hadhara ya vyama vingine.

Serikali na watendaji wake

Katika maadili hayo viongozi wa Serikali wanatakiwa wasiingilie au kuzuia isivyo halali mikutano ya vyama vya siasa au wagombea iliyoitishwa kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi. Serikali pia inakatazwa isifanye kitendo chochote cha kuwakandamiza wafanyakazi wake kwa sababu za uanachama wao au imani yao katika chama chochote cha siasa.

Vyombo vya ulinzi na usalama vimekatazwa visitumie madaraka yao kukandamiza wagombea, wafuasi wa chama chochote cha siasa na visitumie nguvu za ziada.

“Serikali haitamhamisha mtumishi yeyote wa Serikali anayehusika na shughuli za uchaguzi mpaka mchakato wa uchaguzi umemalizika. Endapo Serikali itaona kuna ulazima wa kumhamisha ni lazima ishauriane na NEC,” yanasema maadili hayo.

Maadili yanasisitiza kuwa mawaziri, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wasichanganye ziara za kikazi na shughuli za kiuchaguzi na wasitumie vyombo au watendaji wa Serikali katika shughuli za uchaguzi kwa manufaa yao.

Inasisitizwa kuwa kuanzia kipindi cha kampeni za uchaguzi mpaka kutangazwa kwa matokeo, mawaziri, watendaji na mamlaka zingine za Serikali hazitakiwi kutangaza katika vyombo vya habari au kwa namna yoyote misaada au ahadi ya aina yoyote.

Mawaziri pia wamekazwa kutoa ahadi za shughuli za maendeleo ya jamii kwa mfano, kujenga barabara, kusambaza maji na mambo mengine hayo. Maadili yanatamka kuwa waziri akipanda kwenye jukwaa akatoa ahadi hizo kwa wapigakura kwa lengo la kumpigia debe mgombea wake ni makosa.

Serikali pia ihakikishe kwamba viongozi na watumishi wa umma hawatumii madaraka au rasilimali za Serikali kwa shughuli za kampeni za uchaguzi kwa manufaa ya chama chochote au mgombea yeyote.

“Pale ambapo Serikali inakodisha vyombo vya usafiri basi itoe fursa sawa kwa vyama vyote na wagombea wote na kuwe na uthibitisho kuonyesha kuwa wahusika wamekodishiwa vyombo hivyo na wamelipia.”

Katika maadili hayo inasisitizwa kuwa hakuna waziri au ofisa mwandamizi wa Serikali yeyote atakayemwita msimamizi wa uchaguzi kwa lengo la kujadili masuala ya uchaguzi kuanzia kipindi cha kampeni mpaka kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi.

“Mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na viongozi wengine wa Serikali hawaruhusiwi kuingia katika vituo vya kupigia kura isipokuwa kama ni wapiga kura kwa madhumuni ya kupiga kura, Aidha hawaruhusiwi kuingia katika vituo vya kuhesabia au kujumlisha kura,” yanasisitiza maadili.

Mwandishi wa Makala hii ni Afisa Habari Mwandamizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Anapatikana kwa namba 0788 014 648

Advertisement