Heliamu ni fursa nyingine ya tanzania kuchochea mapinduzi kiuchumi

Muktasari:

Julai 4, 2016 wataalamu wa Kituo cha Utafiti wa Sayansi ya Anga (Nasa) cha nchini Marekani walishuhudia kifaa cha Juno kikitua katika sayari ya Jupita, safari  iliyotumia  miaka mitano  kutoka uso wa dunia  ilipozinduliwa  Agosti  5, 2011. 

Julai 4, 2016 wataalamu wa Kituo cha Utafiti wa Sayansi ya Anga (Nasa) cha nchini Marekani walishuhudia kifaa cha Juno kikitua katika sayari ya Jupita, safari  iliyotumia  miaka mitano  kutoka uso wa dunia  ilipozinduliwa  Agosti  5, 2011. Chombo hicho kimetua katika  sayari hiyo iliyozungukwa kwa wingi wa gesi mbili; heliamu na nitrojeni. Kifaa hicho kinatarajia kuizunguka  sayari hiyo kwa miezi 20 kukusanya taarifa mbalimbali hasa kujua kiasi cha wingi wa gesi ya heliamu na nitrojeni iliyopo.

Mei 27, 2016, hapa Tanzania  ilitangazwa kuwa imegundulika kuwa na gesi ya heliamu. Taarifa hizo  zilianza  kusikika  kupitia katika chaneli ya Mtandao wa Utangazaji wa Habari za  Biashara (CNBC), kupitia kipindi maalumu cha Global Heliamu cha nchini Australia.

Katika mahojiano hayo, Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa kampuni ya Heliamu One, Tom Abraham James ameitaja Tanzania kama nchi pekee inayoweza kushika  nafasi ya juu duniani kwa uzalishaji wa gesi ya heliamu kutokana na ugunduzi wa milimita za ujazo kiasi cha bilioni 54.2 (54.2 BCf) kupitia mradi wa Rukwa (Rukwa Heliamu Project). Kwa mujibu wa taarifa za mwaka kutoka taasisi ya jiolojia ya Marekani (USGS), takwimu zinaonyesha  mahitaji ya gesi ya heliamu katika soka la ndani la nchini humo katika kipindi cha miaka 14 iliyopita; mwaka 1990- 2008, kiasi cha  mita za ujazo za gesi safi ya heliamu milioni 500-2800 (500-2800MCf) zilihitajika  kwa matumizi mbalimbali kama vile kutumika katika mashine za  hospitali kujazwa katika mitungi ya MRI, katika kipindi hicho hicho kiasi cha mita za ujazo milioni 3,400-6,200 MCf kilihitajika kwa ajili ya  kutumiwa katika sekta ya viwanda, afya, usafiri na mawasiliano.

Kwa mujibu wa Profesa Chris Ballentine, mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Oxford na mtalaamu wa mambo ya gesi na jiokemia ambaye pia ni mmoja wa wagunduzi wa heliamu Tanzania, katika chapisho lake la kugundulika kwa heliamu nchini, alitamka: “Huge helium discovery, life-saving find.”

Anasema utafiti huu ulihusisha mchanganyiko wa sampuli mbili ambazo ni heliamu na nitrojeni katika kuchanganya na kutumia uelewa wetu wa heliamu, jiokemia na picha kamili ya mipasuko ya miamba katika bonde la ufa ikatoa kadirio la mita za ujazo bilioni 54.2 (54.2BCf) katika sehemu moja tu ya bonde la ufa.

Vipimo halisi vinaonyesha kuwa ugunduzi wa gesi hiyo kwa kiasi hicho kinaweza kujaza mitungi ya kifaa cha kupimia matibabu (MRI) zaidi ya milioni 1.2, na takwimu zinasema matumizi ya heliamu duniani kwa sasa ni milimita za ujazo bilioni nane kwa mwaka.

Takwimu kutoka katika kitengo maalumu cha kuhifadhi gesi safi ya heliamu nchini Marekani, ambao ndiyo wasambazaji wakubwa duniani wa heliamu, zinasema kuwa kwa sasa wanahifadhi ya milimita za ujazo bilioni 24.2 (24.2BCf). Hata hivyo takwimu za USGS zinaonyesha hifadhi ya heliamu safi na chafu ni milimita za ujazo bilioni 153 (153BCf).

Mtandao wa kampuni kongwe ya utafiti wa Heliamu One, unaonyesha kuwa Tanzania kuna miradi mbalimbali ya heliamu kama vile mradi wa Balangida na Eyasi yenye ukubwa wa kilomita za mraba 4,500 yakihodhiwa na leseni kubwa ya utafiti katika mradi wa Balangida uliopo Singida umeonyesha kuwapo kwa heliamu ya ujazo wa asilimia 10.5, kwa upande wa ziwa Eyasi na asilimia 4.3 kutoka katika chemchemi ya moto.

Jarida la kila mwezi la kampuni ya Heliamu One, limeonyesha kuwa gesi ya heliamu katika soko la dunia imekuwa ikiongezeka kwa asilimia 7.5 kila mwaka, likitolea mfano kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita mahitaji yaliongezeka kwa asilimia 100.

Hivi karibuni kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2011-2013, soko la heliamu liliyumba kutokana na uzalishaji kuwa mdogo uliosababishwa na taarifa ya utafiti iliyosema kuwa gesi ya heliamu ipo mbioni kupotea duniani, lakini baada ya miaka ya miwili kukajitokeza usambazaji mkubwa katika soko la dunia kutokana na kufunguliwa kwa mtambo wa pili wa uzalishaji nchini Qatar (Qatar II) na kuwezesha mwaka 2016 soko la heliamu kuwa sawa na imara.

Taarifa ya hali ya sasa ya soko la heliamu duniani inatarajiwa kuongezeka na kufikia kiasi cha dola za Marekani bilioni sita ($ 6BN) kwa mwaka 2016, nchi ya Marekani ndiyo msambazaji mkubwa duniani ikiwa na asilimia 60 kwa mwaka 2015 ikifuatiwa na Qatar yenye asilimia 24. Wasambazaji wengine ni Algeria, Australia, Canada, Poland na Russia.

Jarida la taarifa za Geoscience la Afrika katika utafiti juu ya bonde la ufa na mfumo wake, unaelezea hali ya eneo la ziwa Rukwa kuwa liko katika bonde la ufa ambalo ni moja ya mipasuko mikubwa duniani.

Jarida hilo linaendelea kueleza kuwa kuwapo kwa mipasuko hai kunawezesha kuwapo kwa chemchemi za majimoto. Mazingira haya ya kijiolojia ni viashiria vya uwapo wa gesi hiyo.

Nchini Tanzania utafiti wa jiofizikia kuainisha viashiria vya uwapo wa madini au gesi ya heliamu ulifanyika miaka ya 1980 hadi 1990 na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), akijibu swali la mbunge wa Kwela katika mkutano wa Bunge la 11 juu ya kuwapo kwa taarifa za ugunduzi wa gesi ya heliamu katika mitandao ya kijamii, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema utafiti wa jiofizikia nchini ulifanyika miaka ya 1980 mpaka 1990 katika ziwa Rukwa kwa ushirikiano wa Chuo Kikuu cha Oxford na Durham.

Alisema wamegundua viashiria vya gesi ya heliamu, na utafiti ulioendelezwa na kampuni ya Heliamu one ya Australia umegundua kiasi cha mita za ujazo wa gesi hiyo bilioni 54.2.

Katika chapisho la kitabu cha madini cha GST mwaka 2011, juu ya madini yapatikanayo Tanzania kimebainisha kuwa gesi ya heliamu yanapatikana katika mkoa wa Mara, wilaya ya Rorya, kijiji cha Nyamusi.

Kwa upande wa chapisho la ramani ya Tanzania ya malighafi zinazotolewa ardhini cha mwaka 2015 kilichoandaliwa na GST kwa ushirikiano na Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo kikuu cha ufundi cha Bergakademie Freiberg na kituo cha Madini kusini Mashariki mwa Afrika katika kiambatanisho cha chati zinazoonyesha uwapo wa viashiria vya heliamu katika maeneo mbalimbali kwa mfano chemchemi ya Hika, Minyere, Mponde, maji moto Musoma, Manaka, Kusini ya Nyamosi, kaskazini ya Nyamosi, Tagwa na Ivuna.

Heliamu inapatikana katika kina kifupi na ina matumizi mbalimbali kama vile, hutumika katika vifaa vya umeme kama redio, teknolojia ya mawasiliano ya baluni angani (Baloon Air Space), urushaji wa helikopta (chopa), inatumika pia kupunguza uzito wa mafuta ya ndege, utengenezaji wa taa mfano tubelight na kuendesha mashine za kupiga picha hospitalini za MRI.

Historia inaonesha kuwa gesi ya heliamu iligundulika mwaka 1895 na Sir William Ramsay, kwa kushirikiana na Per Teodor Cleve na Nil Abraham Langlet jijini London nchini Uingereza, asili ya jina heliamu linatokana na lugha ya Kigiriki “Helios” likiwa na maana ya jua.

 

Yameandikwa kwa utashi wa mwandishi, hayana uhusiano wowote na anapofanyia kazi. Wasiliana naye kwa simu 0756638393 au baruapepe [email protected]