Hili la Diamond na Kamanda Mpinga linafikirisha

Muktasari:

  • Nani asiyependa heshima? Kila mtu duniani angependa kuheshimiwa hasa na watu wenye hadhi na madaraka.

Wakati wengine wanatafuta fedha waende kwenye muziki kuburudika, msanii anaburudika huku akiingiza fedha. Hakika hii ni kazi nzuri.

Zaidi ya yote anapata umaarufu ambao katika dunia ni chambo cha kupata huduma nyingine kwa urahisi tofauti na yule asiyefahamika. Umaarufu unamfanya aheshimike hata na viongozi wa Serikali.

Mfano mzuri ni kilichotokea wiki hii kati ya mwanamuziki Diamond na Kamanda wa  Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga.

Kila mtu angependa kuitwa ofisini kwa kamanda na baada ya kulipa faini apige naye picha.

Nani asiyependa heshima? Kila mtu duniani angependa kuheshimiwa hasa na watu wenye hadhi na madaraka.

Hebu fikiria, Umemaliza chuo ukiwa na matumaini tele ya kuipata kazi ya ndoto yako. Baada ya kuzunguka na bahasha kwa miaka miwili unaanza kufikiria  kufanya kazi nyingine. Ukiangalia huku na kule mara imetokea kazi unajisemea moyoni  wacha nijishikize.

Huu ni mwaka wa 10 umejishikiza kwenye kazi hiyo na pengine ndoto za kufanya kazi uliyoitamani enzi za utoto wako na kuisomea zinaanza kufifia. Waangalie watu waliokuzunguka na waulize kama wakifanyacho sasa kilikuwa katika mipango yao enzi za utoto.

Jibu ni kwamba wengi waliamua kufanya kazi walizopata na kujikuta wamelowea huko.

Kwa maana hii unajikuta unafanya kitu ambacho moyo wako haukipendi kwa dhati, unafanya ukiamini kuwa umejishikiza lakini siku zinayoyoma hivyo.

Huwa naamini wanamuziki ndiyo watu wanaofurahia maisha yao na wana nafasi ya kufanya vizuri siku zote za maisha yao.

Hebu fikiria unaupenda muziki halafu inakuwa kazi yako. Kila unachofanya kinasindikizwa na muziki. Ofisi yako haikulazimishi kuvaa suti na tai, kwa mwanamke anaweza kuvaa nguo ya ndani tu na kuingia kazini.

Yote kwa yote inabidi kupenda unachokifanya kwa namna yoyote  ile kwa sababu ndicho kinachopeleka chakula mezani kwako na kulipia bili zote.

Ubora wa kazi  yako taratibu utakufanya uipende kwa sababu kama ni bidhaa au huduma itapendwa na bila kujua unaweza kujikuta umeangukia kwenye mapenzi na kazi au wateja unaowahudumia.

Wanamuziki wana bahati kwa kuwa kazi yao inaburudisha, inatoa heshima na kuingiza fedha nyingi.

Mwanamuziki anaweza kuingiza Sh1 milioni kwa onyesho la nusu saa, wakati mfanyakazi wa kawaida anaisotea Sh300,000 mwezi mzima.

 [email protected] Sms 0744 053 111