Hillary Clinton alivyoweka historia Marekani

Hillary Clinton

Muktasari:

Uteuzi huo aliupata katika mji wa Philadelphia ambao mwaka 1776 mahala hapohapo ndipo palipotolewa tangazo la uhuru wa Marekani.

Hillary Clinton, ameweka historia. Mwanasiasa huyo wa Chama cha Democratic, ni mwanamke wa kwanza kuteuliwa na chama kikubwa kugombea urais.

Uteuzi huo aliupata katika mji wa Philadelphia ambao mwaka 1776 mahala hapohapo ndipo palipotolewa tangazo la uhuru wa Marekani.

Hillary, aliyewahi kuwa waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, katika mkutano mkuu wa chama chake wiki hii, alinyakua zaidi ya kura 2,383 za wajumbe, zaidi ya nusu, na hivyo kuwa na wingi ulio wazi.

Ni miaka 100 sasa tangu pale wanawake walipopata haki kamili ya kupiga kura nchini humo.

Mpinzani wa Clinton katika kampeni za mchujo ndani ya chama, Bernie Sanders, seneta wa Mkoa wa Vermont, mwishowe aliwaomba wajumbe wa mkutano mkuu wamuunge mkono Hillary, hivyo kuhakikisha ushindi wa bibi huyo.

Pia hapo awali, Michelle Obama, mke wa rais wa sasa, Barack Obama, alimpigia debe Bibi Clinton. Mumewe Hillary, rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton alisimama katika ukumbi wa mkutano na kumsifu mkewe kwamba ana uwezo wa kubeba dhamana kubwa ya urais na ataweza kuiletea nchi hiyo mabadiliko na kukabiliana na hatari zilizoko mbele ya taifa hilo kubwa duniani.

Licha ya hayo, wafuasi wa Sanders katika mkutano mkuu hawakujizuia kuelezea masikitiko yao kushindwa mtu wao na wakaulaumu uongozi wa chama cha Democratic kwa kuendesha vitimbi vya kumpendelea Hillary Clinton wakati wa kampeni za mchujo ndani ya chama.

Baada ya kutangazwa ushindi wake, Hillary katika risala yake kwa njia ya video aliwaambia wafuasi wake kes kusema:” Kwa kweli huo ni ushindi wenu, huu ni usiku wenu.”

Hillary atashindana na mgombea wa Chama cha Republican, Donald Trump katika uchaguzi wa urais Novemba 8. Trump, tajiri mkubwa wa biashara ya ujenzi wa majumba na ambaye hapo kabla alikuwa hatajiki katika mambo ya siasa, wiki iliopita alichaguliwa na mkutano mkuu wa chama chake huko Cleveland kuwania nafasi ya urais wa nchi.

Mchuano katika kampeni zijazo baina ya Clinton na Trump hautakuwa rahisi, japokuwa wahakiki wanatia dau kwamba Hilary atashinda.

Ukiiangalia historia ya Hillary ni kwamba maishani mwake amekuwa akipigania mambo muhimu, mfano maslahi ya walemavu badala ya kuwabeza. Amewatetea watu weusi wanaokabiliwa mara nyingi na nguvu za polisi katika miji mkubwa ya Marekani.

Hillary Clinton ameukubali na kuusemea ule ukweli ambao watu wengi sana wa rangi nyeupe hawajaribu kuutaja kwa sauti kubwa kwamba “maisha ya mtu mweusi yana thamani pia.

Tangu alipokuwa wakili kijana, Hillary amekuwa akitetea haki za watoto na amepigania kuwapo kwa bima ya afya kwa Wamarekani wote. Aliwatemebelea hospitalini watu waliojeruhiwa katika mashambulio ya kigaidi ya Septemba 11, 2001, na anapigania kuwapo kwa marekebisho katika kanuni zinazohusu namna wafungwa wanavotendewa katika magereza.

Amewahi kupinga sheria za Marekani zenye kurahisisha raia kumiliki silaha. Clinton ameshikilia kuwapo kwa kiwango cha chini cha mshahara ambapo familia haitaishi katika umaskini.

Ni kutokana na hayo ndio maana mkutano mkuu wa Democratic umemkabidhi Clinton apeperushe bendera ya chama hicho katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu wa Novemba.

Wahakiki wengi wanasema inabidi Hillary ashinde uchaguzi huu, ama sivyo mambo hayatakuwa mazuri kwa Marekani yenyewe, kwa Ulaya na kwa nchi nyingine za kidemokrasia duniani. Pindi atashindwa itakuwa balaa.

Kuchaguliwa Trump kutazusha hali ya wasiwasi katika nchi za kidemokrasia za Magharibi, ikiwa ni kabla ya kufanyika uchaguzi wa urais nchini Ufaransa na miezi 10 kabla ya Ujerumani kuwa na uchaguzi wake mkuu. Kuchaguliwa Trump hakutatoa ishara nzuri.

Marekani imekuwa na marais 44 kabla, na wengi wao wamekuwa na ‘ndevu’. Lakini Hillary Clinton atakapochaguliwa Novemba 8 atakuwa si tu hana ndevu, lakini atakuwa mwanamke wa kwanza katika historia ya nchi hiyo kubwa.

Tamko lake la mwanzo baada ya kuteuliwa kuwa mgombea lilikuwa fupi. Aliushukuru mkutano mkuu wa chama chake kwa imani waliyoionyesha kwake na aliwaahidi wanawake vijana wa Marekani mambo mazuri kwa vile mmoja wao, yeye, sasa anaweza kuwa rais.

Haikataliki kwamba kuteuliwa kwa Hillary Clinton kutawapa moyo wanawake wa Marekani na wa dunia, kwa jumla. Wengi wao, pamoja na watoto wao wa kiume, hivi sasa wanatokwa na machozi ya furaha.

Wanajihisi vizuri. Wanaume pia, ambao ni watoto wa kina mama, wanatokwa na machozi ya furaha kwa tukio hili la kihistoria.

Nakumbuka karibu miaka minane iliopita pale Barack Obama alipoteuliwa na chama chake cha Democratic agombee urais wa Marekani, nilikuwa naangalia runinga ya Marekani. Nilimuona mtoto mdogo wa Kimarekani mwenye asili ya Kiafrika akimkimbilia mama yake pale alipomuona baba yake akilia na kutokwa na machozi akiwa ameketi katika sofa anaangalia runinga.

Mtoto huyo alimuuliza mama yake:” Mama! mbona baba analia, na nini maana ya historia?”

Baba huyo alilia kwa sababu mtu mweusi kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yake ya Marekani atakuwa rais wa Marekani kabla ya hata mwanamke mweupe kuteuliwa na chama kikubwa kuwania nafasi hiyo.

Mwafrika yeyote lazima alitokwa na machozi ya furaha wakati huo, si tu wale wenye asili ya Kiafrika huko Marekani.

Na pale Novemba 8 Hillary Clinton atakapochaguliwa kuwa rais wa dola kubwa, yenye nguvu kabisa duniani, sote sisi binadamu tuna kila sababu ya kutokwa na machozi ya furaha.

Mwanadamu angalau anapiga hatua, licha ya matatizo yote makubwa yanayomzunguka, kuelekea kwenye dunia iliyo huru kutokana na ubaguzi wa rangi na wa jinsia uliotamalaki duniani.