KUTOKA MEZA YA MHARIRI WA JAMII: Hivi ndivyo barua ya kuomba kazi inavyoandikwa

Muktasari:

Kwa mfano, mmoja ameandika, “bro, fanyafanya kibarua basi;” mwingine ameandika, “dingi huwezi kunipatia kazi huko;” na mwingine, “mimi mariamu.naishi korogwe.nimemaliza darasa la saba.nipe kazi yoyote.nina mtoto mmoja yusufu.”

Wiki tatu zilizopita nilieleza katika safu hii jinsi ninavyopokea maombi ya kazi, ama kwa njia ya mzaha au kwa jinsi waombaji wanavyoelewa.

Kwa mfano, mmoja ameandika, “bro, fanyafanya kibarua basi;” mwingine ameandika, “dingi huwezi kunipatia kazi huko;” na mwingine, “mimi mariamu.naishi korogwe.nimemaliza darasa la saba.nipe kazi yoyote.nina mtoto mmoja yusufu.”

Rafiki yangu anasema “huo ndio ulimwengu wao na hapo wameomba; tena kwa dhati.” Si rahisi kuamini hivyo.

Niliahidi kuweka hapa mifano ya barua za kuomba kazi na ufafanuzi juu ya njia mbalimbali za kuandika barua za aina hiyo. Hivi ndivyo nifanyavyo leo.

Mpaka sasa nina barua 12 za wasomaji ambazo wahusika wanasema waliombea kazi na kupata ajira. Sitachapisha zote; bali leo tusome ya mstaafu Alphonce Bagambi.

Amekataa kutaja jina la kampuni alikoajiriwa. Alimaliza Darasa la 12 (Form IV) mwaka 1964. Aliomba kazi kwa barua iliyoandikwa kwa mkono na katika lugha ya Kiingereza. Alipata ajira. Barua ilikuwa kama ifuatavyo (ametafsiri mwenyewe kwa Kiswahili):

Alphonce Kasisi Bagambi,

k.k. P. E. Kajumulo,

S.L.P. 198,

Bukoba.

21 Juni 1965.

Maneja Mkuu,

Kampuni ya …,

S.L.P. …,

Dar es Salaam.

Bw,

MAOMBI YA KAZI YA FUNDI MITAMBO

Ninayo heshima kuleta kwako, maombi yangu ya kuajiriwa kama fundi mitambo katika kampuni yako.

Mimi ni mwanaume; nimemaliza masomo ya Darasa la 12 mwaka jana (1964) katika Shule ya Sekondari Kahororo, Bukoba na kuhitimu kama ifuatavyo: Kiingereza 4, Hesabu 3, Fizikia 4, Kemia 3, Baolojia 4 na Jiografia 6.

Sijafanya kazi mahali popote lakini nina hamu ya kuwa fundi wa mitambo ya kutengeneza … Nina kipaji cha kushika haraka ninapoelekezwa na niko tayari kujifunza kadri ya mahitaji ya kampuni yako.

Ninawasilisha maombi yangu haya kwa matumaini kwamba yatafikiriwa vema; huku nikiahidi kuwa na bidii kazini na kuwa mwaminifu.

Ndimi mtiifu,

……………

(saini)

Alphonce K. Bagambi.”

• Kiambatisho: Nakala ya matokeo rasmi ya mtihani wa Darasa la 12.

Bagambi anasema wiki tatu baada ya kupeleka maombi yake, alipokea barua ikimwelekeza kwenda ofisi ya wakala wa kampuni alikoomba kazi, iliyokuwa mjini Bukoba, ili awezeshwe kusafiri kwenda Dar es Salaam kwa usaili. Alipenya na kuajiriwa.

Barua hii inaonyesha kuwa mwombaji alitupa tu ndoana ziwani. Akavua samaki aliyetaka. Nafasi ya kazi haikuwa imetangazwa. Angeweza kuvua chochote kile kilichomo majini; hata kutojibiwa au kuambiwa “hakuna kazi.”

Angalia mpangilio wa barua hii ambao hufundishwa kuanzia madarasa ya awali. Njoo kwenye maudhui muhimu ya barua na nyongeza zisizo za lazima lakini zinazosindikiza maombi.

Katika aya ya kwanza anasema kile anachotaka. Katika aya ya pili na tatu anajieleza – yeye ni nani; ana nini cha kushindanisha – uwezo uliothibitika darasani na hamu yake. Anatumia aya ya nne kuonyesha anavyojiamini: Kama si yeye, nani?

Ukiunganisha yote haya, na kama mwombaji hakuandikiwa, utagundua ung’avu wa mawazo, wepesi wa kuelewa; na uwezekano wa kufundishika haraka ambavyo huthibitishwa wakati wa usaili.

Wewe msomaji unasemaje? Wiki ijayo: Maelezo juu ya aina nyingine za kuandika barua za kuomba kazi.

Mwandishi ni Mhariri wa Jamii wa vyombo vya habari vya Mwananchi Communications Limited wachapishaji wa magazeti ya The Citizen, Mwanaspoti na hili. Kwa maswali na hoja j, wasiliana naye kwa: 0713614872 au 0763670229; e-mail: [email protected] au [email protected]