Hizi zilipigwa ndani-nje na Mnyama

Muktasari:

  • Ruvu Shooting ndiyo timu iliyochezea kipigo cha maana kutoka kwa Simba msimu huu. Itakumbukwa mzunguko wa kwanza ilifungwa 7-0 kabla ya kupigwa 3-0 marudiano.

ZIPO timu zilizoonja joto ya jiwe kutoka kwa Simba ilipokuwa inasaka heshima ya kutwaa ubingwa kwa msimu wa 2017/18, zilifungwa ndani na nje kwa maana ya mechi za nyumbani na ugenini.

RUVU Shooting -mabao 10

Ruvu Shooting ndiyo timu iliyochezea kipigo cha maana kutoka kwa Simba msimu huu. Itakumbukwa mzunguko wa kwanza ilifungwa 7-0 kabla ya kupigwa 3-0 marudiano.

Simba ilipata mabao yake yakifungwa na Emmanuel Okwi na John Bocco.

NJOMBE MJI-mabao 6

Njombe ilianza kucheza ugenini dhidi ya Simba, ikiwa ndio msimu wake wa kwanza ikajikuta ikiambulia kipigo cha mabao 4-0 Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Kwa mechi ya mzunguko wa pili ilipunguza idadi ya mabao ya kufungwa badala ya manne, ikafungwa 2-0 na kujikuta imegawa pointi sita na jumla ya mabao sita.

PRISONS-mabao 3

Prisons ilianza kupata kipigo kwenye Uwanja wa Sokoine na Simba iliibuka na ushindi wa 1-0.

Mechi yao ya mzunguko wa pili, haikufurukuta baada ya kufungwa tena dimba la Taifa jijini Dar es Salaam mabao 2-0 na kujikuta ikigawa pointi sita.

MBEYA CITY- mabao 4

Katika mzunguko wa kwanza Simba, ilikuwa mgeni wa Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine ambako waliibuka na ushindi wa bao 1-0 na baadaye kurudiana Taifa na kushinda kwa mara nyingine mabao 3-1 na kujikuta ikiachia pointi sita Msimbazi.

NDANDA FC -mabao 3

Katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, John Bocco aliwalazama mapema wenyeji wao kwa kuwafunga mabao 2-0 wakati katika mechi ya marudiano Dimba la Taifa jijini Dar es Salaam bado Simba ilimaliza dakika 90 kibabe kwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

SINGIDA UNITED-mabao 5

Kilichowakuta Singida United, ilipokuwa imecheza na Simba Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kiliwaacha mdomo wazi baada ya kupata kipigo cha mabao 4-0, tofauti na walivyokuwa wamefikiri kabla ya mchezo.

Badaye Simba waliifuata Singida United na kuwafunga katika Uwanja wao wa Namfua bao 1-0.

MWADUI FC Mabao 5

Mwadui ilifungwa mabao 3-2 mchezo wa kwanza kwenye Uwanja wa Taifa, lakini kwenye Uwanja wa Kambarage wakapigwa kiulaini kabisa mabao 2-0. Mchezo wa mwisho ni Simba na Majimaji mjini Songea na Simba ilishinda 4-0 Dar.