JICHO LA MWALIMU : Hofu humkosesha mwanafunzi kujiamini

Tuesday March 13 2018



Joseph Chikaka

Joseph Chikaka 

By Joseph Chikaka

Hakuna jambo baya na linaloweza kumtesa binadamu kama kukubali kutawaliwa na hofu.

Hofu ni kitu kibaya na inaweza kuua haraka na kwa wingi kuliko silaha yoyote ile.

Wapo watu wenye hofu na kila kitu wanachokifanya. Kwa mfano, utakuta watu hao wakiwa na hofu na vyakula wanavyokula, wakiwa na hofu na vinywaji wanavyotumia, wakiwa na hofu na mazingira wanayoishi.

Pia, wana hofu na vyombo vya usafiri na vyombo vya kupikia wanavyotumia. Wana hofu hata na nyumba za ibada wanazohudhuria na wakati mwingine wakiwa na hofu hata na watu walio karibu nao.

Wanafunzi nao wakiwa shuleni hugubikwa na hofu kama hizo ambazo kama walimu, walezi na wazazi hawatakuwa na macho ya kuzibaini, zinaweza kusababisha kutofikiwa kwa matokeo chanya yaliyotarajiwa.

Mathalani, wanafunzi wengi wamekuwa na hofu zifuatazo hasa kipindi kinachoelekea mitihani yao;

Hofu ya aina ya maswali watakayoulizwa, hofu ya siku yenyewe ya mtihani, hofu ya kukosa maswali anayoyajua na asiyoyajua kana kwamba kukosea katika kujifunza ni dhambi.

Pia, hofu ya kuonekana hawafahamu, hofu ya akiwa katika siku zake pengine na mazingira yasiyokuwa rafiki kwa wasichana; hofu ya fimbo kutoka kwa walimu au wazazi, hofu ya kuogopa kuchekwa na wenzake au walimu na zaidi hofu ya kulaumiwa.

Wanafunzi hawa waliojawa hofu hushindwa kuwa na utulivu wakati wa kujisomea na wakati mwingine kushindwa kufuatilia masomo kwa usahihi, hivyo kufanya mambo wasiyopenda kuyafanya.

Kwa mfano, Jajuja ni mwanafunzi ambaye alikuwa na hofu kubwa kila alipoingia mwalimu wa somo fulani. Hii ni kwa sababu mwalimu huyo hakuwa na kawaida ya kusema lini atatoa jaribio ambalo atarekodi alama zake.

Aliweza kufundisha na zikasalia dakika 10 anatoa jaribio la haraka haraka katika vitu alivyofundisha ama ambavyo hata bado hajafundisha. Bahati mbaya kila akitoa jaribio fupi la papo kwa papo, Jajuja huwa hayuko vizuri.

Hujawa hofu mpaka kijasho chembamba kinamtoka. Ilifika kipindi Jajuja alifurahi akisikia siku hiyo mwalimu hatoweza kufika darasani. Hii yote ilisababishwa na hofu.

Hofu kwa wanafunzi haichagui darasa; inaweza kuanzia shule ya awali, msingi, sekondari mpaka chuo. Katika elimu ya juu wakati mwingine hofu hukua zaidi na kuwa hatari, kwani wengine huhofia kufanya mtihani wa kurudia tena kozi aliyoishindwa. Wengine huhofia watakaposhindwa kufaulu tena kwa mara nyingine, watapaswa kulibeba tena somo hilo katika mwaka mwingine unaofuata.

Hofu hizi zote za mchakamchaka wa ratiba, uhusiano na nyingine, huwapa wanafunzi wakati mgumu wakiwa shuleni.

Hofu hiyohiyo ikizoeleka na kujijenga, huharibu mitazamo ya mwanafunzi kiasi cha kumwandama kijana huyo hata katika shughuli zake za kijamii, kiuhusiano na kiimani.

Hivyo, jamii haina budi kuona inajenga matumaini na kujiamini kwa wanafunzi kwa kuwapa nafasi ya kuwasikiliza na kuondoa mazingira ya changamoto zinazo onekana.

Baadhi ya mambo yanayoweza kumsaidia mwanafunzi kuondokana na hisia za hofu darasani na shuleni ni kama haya:

Moja, kuwa na ratiba binafsi ya kujifunza. Ratiba hii isiishie tu kuwapo bali iheshimiwe kwa kufuatwa na kutekelezwa.

Mbili, kupata muda wa kupumzika. Mchakamchaka wa masomo na vipindi darasani na kazi za nyumbani husababisha mwanafunzi kukosa raha ya mazingira ya shule. Ni wajibu kwa mwanafunzi kupumzika kabla hajaendelea na ratiba nyingine.

Tatu, kuzungumza changamoto zinazomkabili. Kama kuna somo mwanafunzi hajalielewa ni vema akauliza kwa wenzake na pia kwa mwalimu husika ili aweze kuona namna anavyoweza kumsaidia.

Nne, kupanga vema malengo yake. Malengo ya kimasomo ya siku, wiki, mwezi na muhula ni vema yakapangwa na kutekelezwa vema na wakati mwingine kuyapunguza na kuanza kutekeleza yale yanayohitaji muda mfupi kabla ya yale ya muda mrefu na ya kudumu.

Tano, kuchukua hatua kwa ngazi kwa ngazi kwa mfuatano maalumu wakati wa kukabiliana na changamoto za masomo na maisha.

Sita, kuwa na mazoea ya kufanya mazoezi ya viungo. Mwili wenye mazoezi huwa uko tayari kupambana na kuketi katika dawati kwa hadi saa nne. Hivyo mazoezi yanahitajika ili kufanya mifumo na viungo mbalimbali vya mwili kufanya kazi yake vema na ipasavyo.

Saba, kuwa na mtazamo chanya juu ya masomo na changamoto zinazojitokeza kuwa zitaweza kupatiwa ufumbuzi. Kipindi cha majaribio ya mitihani ni vema mwanafunzi akajifunza kukuza staha au kujiamini kwake kuliko kuwa na mawazo hasi yanayoshusha morali na kujiamini.

Nane, kuepuka matumizi ya vilevi kama pombe, madawa ya kulevya na uvutaji wa sigara ama bangi. Vitu hivi hutengeneza utegemezi na kushusha kiwango chao cha kutafakari na kuona mambo.

Jamii ina nafasi kubwa pia ya kuweza kuwasaidia wanafunzi dhidi ya maisha ya hisia za hofu, kwa kuwaamini kuwa wanaweza na kuwasaidia kutatua matatizo yanayoweza kuwasababishia wasijifunze vema.

Jamii itambue vipawa vyao na kuviendeleza. Kwa sababu wanafunzi hutofautiana katika uwezo wa kujifunza, kukumbuka na kuchanganua masuala mbalimbali wanayojifunza.

Wengine huchukua muda mfupi kuelewa mambo na wengine hupaswa kurudiarudia yale wanayojifunza ili waweze kupata mantiki yake. Hivyo, walimu na wazazi watambue hilo na kuwasaidia wanafunzi kulingana na uwezo wao na vipaji vyao.

Wapo walimu ambao wao binafsi wana uwezo mkubwa wa kuchanganua mambo, hivyo wasipore nafasi ya mwanafunzi kukosea na kuona ni dhambi, bali waichukulie kuwa ni sehemu ya kujifunza.


Advertisement