Hoja ya Bashe kuhusu ‘wasiojulikana’, demokrasia iungwe mkono, iboreshwe

Muktasari:

  • Nilichambua zaidi jinsi Bunge la Marekani mwaka 1974, lilipomlazimisha Rais wa 37 wa nchi hiyo, Richard Nixon kujiuzulu, baada ya kufanya uchunguzi na kumbaini kuwa alitumia njia batili kushinda uchaguzi wa Rais uliofanyika Novemba 7, 1972 ambao alishinda na kuwa Rais wa Marekani kwa muhula wa pili.

Oktoba mwaka jana niliandika makala yenye kichwa “Bunge linaweza kumaliza utata wa wasiojulikana”. Nilijenga hoja kuhusu nafasi ya Bunge kikatiba, mamlaka yake na kuchukua mifano ya mabunge mengine duniani, nini hufanya yanapoibuka mazingira yenye kukosa majibu yaliyonyooka kutoka kwa Serikali.

Nilichambua zaidi jinsi Bunge la Marekani mwaka 1974, lilipomlazimisha Rais wa 37 wa nchi hiyo, Richard Nixon kujiuzulu, baada ya kufanya uchunguzi na kumbaini kuwa alitumia njia batili kushinda uchaguzi wa Rais uliofanyika Novemba 7, 1972 ambao alishinda na kuwa Rais wa Marekani kwa muhula wa pili.

Timu ya kampeni ya Nixon (chama cha Republican), ilivamia ofisi za kampeni za Democratic, zilizokuwepo kwenye jengo la Watergate, Washington DC, wakatega vifaa vya kunasa mazungumzo, vilevile waliiba nyaraka ambazo ziliwezesha Republican kujua mbinu zote za mgombea wa Democratic, George McGovern.

Watu waliokamatwa wakiingia ofisi za Democratic walibainika ni makomandoo wa Cuba waliokuwepo Marekani wakipikwa na kuwekwa tayari kwa ajili ya kumpindua aliyekuwa Rais wa Cuba, Fidel Castro. Baada ya idara ya upelelezi ya FBI kuwakamata makomandoo hao, mchezo uligeuzwa.

Makomandoo wa Cuba walisema walivamia ofisi za Democratic baada ya kupata taarifa kuwa McGovern alikuwa na mawasiliano ya ukaribu na Castro. Awali ikaonekana kweli Democratic walitenda jambo haramu kwa kuruhusu Castro kuingilia uchaguzi wa Marekani.

Hata hivyo, uchunguzi wa kibunge uliwezesha kubaini umafia wote ambao ulitekelezwa na Nixon, zikiwemo nyaraka za Democratic zilizoibwa, kukutwa Ikulu. Ikabidi Congress waanze mchakato wa kumpigia Nixon kura ya kutokuwa na imani naye, ndipo Nixon akajiuzulu.

Tafsiri ya mfano

Mfano huo wa namna ambavyo kashfa ya Watergate ilivyoshughulikiwa ni jawabu kwambe Bunge linapoamua kusimamia misingi huwezesha majibu magumu kupatikana. Kulikuwa na hila nyingi zilizofanywa ili kumlinda Nixon, zilizozuia vyombo vya kiuchunguzi kutimiza wajibu wake. Kwa Congress haikuwa rahisi kuizuia.

Mafanikio ya uchunguzi wa Bunge huambatana na nchi kuwa na wabunge wanaotambua hadhi ya mhimili wenyewe. Wabunge wenye kuelewa na kuheshimu kuwa Bunge ndicho chombo kinachoweza kuiweka nchi sawa, pale Serikali inapovurunda au kunapokuwa na matukio yenye kuwaweka watu roho juu.

Ukumbi wa Bunge kwa lugha nyingine huitwa August House (Nyumba Tukufu). Kwa maana ndilo jengo lenye kubeba hisia za wananchi kwa nchi yao, maana wabunge ni wawakilishi wa watu. Wabunge hutakiwa kuutendea haki uwepo wao bungeni kwa kuweka mbele maslahi na hisia za wapigakura wao.

Nyakati ambazo watu wanapotea na haijulikani wanapelekwa wapi. Wananchi wanakuwa na maswali mengi ambayo vyombo vya usalama nchini haviyajibu. Ni hapo sasa Bunge hutakiwa kuthibitisha utukufu wake kwa kuonyesha umahiri wa kuchimba jambo husika na kukata mzizi wa fitina.

Bunge kukaa kimya kipindi ambacho nchi inakuwa kwenye hali ya wasiwasi, watu wanakutwa wamekufa kwenye fukwe za Bahari ya Hindi na Mto Ruvu, tena haliwi tukio la mara moja bali matukio yanafuatana. Wakati huohuo vyombo rasmi havitoi majawabu yenye kunyooka kuhusu hali hiyo. Hiyo ni aibu kubwa kwa Bunge.

Kwa bahati mbaya Bunge la 11 la Tanzania, limekuwa likivumilia sana aibu hiyo ya kukaa kimya kwenye nyakati ambazo nchi inakuwa imezingirwa na viulizo vingi kuhusu usalama wao. Lilikaa kimya hata wakati wa mfululizo wa mauaji Kibiti. Mpaka sasa Watanzania hawajui nini kilitokea na nini kinaendelea. Je, yale mambo yamekwisha au yamepoa kwa muda?

Bunge lina mamlaka ya kikatiba ya kuisimamia Serikali. Usimamizi huo ni kwa njia ya kuisikiliza au kuihoji. Kwamba kama idara za Serikali hazioni kuwa zinawiwa kujitokeza zenyewe kwenye kamati za Bunge na kueleza kinagaubaga masuala ambayo wananchi wanataka majibu, basi Bunge halina budi kuihoji Serikali, ama kupitia kwa wakuu wa idara, mawaziri na hata Waziri Mkuu.

Zipo nyakati mambo yanaweza kuwa moto kwenye nchi. Serikali inaweza kuziba masikio au ikawa inapuuza joto husika kama vile halipo. Bunge kwa sababu lenyewe ndiyo linawakilisha sauti, matarajio na hisia za watu, hupaswa kuibana Serikali ili ama itoe majibu au ifanyie kazi suala husika. Ikibidi, Bunge linachunguza na kuiwajibisha Serikali pale inapostahili.

Bunge linaweza kuiwajibisha Serikali si kwa sababu ya kutenda au kuhusika na vitendo husika, bali linaweza kuchukua dhima hiyo hata pale ambapo Serikali haikuchukua hatua stahiki au ilichelewa kutimiza wajibu wake.

Na tafsiri ya Bunge kutoichukulia hatua Serikali au kutoibana kwa matukio yaliyo wazi kabisa, maana yake haliwajibiki ipasavyo. Linakuwa Bunge lisilo na meno.

Hoja ya Bashe

Mwanzoni mwa Februari mwaka huu, wakati mwandishi wa habari wa kujitegemea, aliyekuwa akiripoti gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda, alipokuwa na zaidi ya miezi miwili tangu alipotoweka, niliandika makala nikieleza aibu ya Bunge, kukutana na kuahirisha mkutano bila kupata fursa ya kujadili kupotea kwa Mtanzania huyo.

Nilisema kuwa aibu hiyo ya Bunge inamgusa moja kwa moja mbunge anayewakilisha jimbo la Azory, kwani vyombo vya habari vinaripoti, gazeti la Mwananchi lilikuwa linatoa kipaumbele kwa kukumbusha kila siku kuhusu idadi ya siku zinavyoongezeka tangu alipotoweka, lakini mbunge wa jimbo analotoka mwandishi huyo hajaguswa japo robo.

Kipindi ambacho Bunge linaonekana kubeba lawama kwa sababu ya wabunge kuonekana hawajali yanayoendelea au kutotimiza wajibu wao, ni hali ambayo inaweza kuwakatisha tamaa wananchi juu ya chombo chao cha uwakilishi. Wakati huo sasa anaibuka mbunge na kuweka kusudio la kuwasilisha hoja binafsi ili Bunge lijadili yote.

Mbunge huyo wa CCM anataka Bunge liunde Kamati Teule ya kuchunguza mwenendo wa matukio yote. Anataka uchunguzi huru wa kibunge juu ya tukio la kushambuliwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, Septemba 7, mwaka jana, vilevile kupotea kwa kada wa Chadema, Ben Saanane Novemba 2016.

Mbunge huyo, Hussein Bashe (Nzega Mjini), ambaye mwaka jana alipata kulia bungeni, akitoa ushuhuda kwamba naye aliwahi kutekwa. Anataka uchunguzi wa kibunge mpaka kuhusu tukio la kifo cha Katibu wa Chadema, Kata ya Hananasif, Kinondoni, Daniel John, aliyeuawa wakati wa mchakato wa uchaguzi mdogo jimbo la Kinondoni, Februari mwaka huu.

Hoja ya Bashe inahusu kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini, aliyepigwa risasi akiwa kwenye daladala, wakati polisi wakidhibiti maandamano ya Chadema.

Bashe anataka Bunge lichunguze kuhusu polisi kutumia risasi za moto katika tukio hilo. Kimsingi Bashe anataka uchunguzi dhidi ya matukio yote yenye kukiuka misingi ya haki za binadamu na kuminywa kwa demokrasia.

Hoja iboreshwe

Kuna la kujiuliza, je, Bashe anatania? Jawabu la swali hilo lipo Aprili mwaka jana. Bashe alisimama bungeni kuomba Bunge lijadili tukio la kutekwa kwa Saanane na mwanamuziki Ibrahim Mshana ‘Roma Mkatoliki’ na wenzake watatu ambao walikuwa wametekwa wakati huo kabla ya kuachiwa baada ya siku tatu.

Kulipokuwa na hali ya kupinga watu kujadili bungeni suala hilo la utekaji watu, Bashe alisema waliokuwa wakipinga ni kwa sababu hawajawahi kuonewa wala kunyanyaswa. Alijisema yeye kuwa amewahi kutekwa. Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alikataa mjadala huo.

Hivyo, hoja ya sasa ya Bashe unaweza kutafsiri kwamba ameamua kuirudisha bungeni kivingine. Kwa maana hiyo Bashe anastahili kuungwa mkono na kupongezwa kwa kuguswa na mwenendo mbaya wa matukio yenye kuvunja haki za binadamu na demokrasia. Muhimu aboreshe hoja yake kwa kuongeza ombi la Bunge kuchunguza matukio ya madiwani na wabunge kuhama vyama. Je, wanahama kwa utashi wao au kwa ushawishi wa fedha?