Hoja za Zitto nzito hadi Katiba mpya

Muktasari:

  • Kwa utaratibu huu uliowekwa na Katiba, wananchi wakapewa mamlaka ya kuchagua wabunge katika kila jimbo, na wabunge wengine wanaopatikana kwa utaratibu mwingine, ili waweze kuchukua maoni yao, kero zao na kuziwakilisha bungeni.

Kwa lugha ya kawaida, Watanzania wote milioni 50 wangetakiwa kushiriki katika mikutano ya Bunge kutunga sheria, kupitisha bajeti na kuisimamia Serikali lakini kutokana na ugumu wa jambo hilo, ukawekwa utaratibu wa uwakilishi unaotumika sasa.

Kwa utaratibu huu uliowekwa na Katiba, wananchi wakapewa mamlaka ya kuchagua wabunge katika kila jimbo, na wabunge wengine wanaopatikana kwa utaratibu mwingine, ili waweze kuchukua maoni yao, kero zao na kuziwakilisha bungeni.

Uhuru wa wananchi kuchagua wawakilishi hao kupitia vyama tofauti vya siasa ulianza katika uchaguzi wa mwaka 1995. Kabla ya hapo wabunge hao walitokana na chama kimoja kilichokuwapo – Chama cha Mapinduzi (CCM).

Hata hivyo, licha ya wawakilishi hao kuchaguliwa chini ya mfumo unaotambulika kikatiba, katika siku za karibuni malalamiko ya upinzani kukandamizwa ndani ya chombo, na washindani wao kupendelewa yaliyokuwapo muda mrefu yamezidi kukomaa.

Wakati hali ikiwa hivyo, pia yameibuka madai ambayo pia yanazidi kukita mizizi kuwa Bunge hilo limekosa meno ya kuisimamia Serikali kwa niaba ya wananchi.

Ingawa mara kadhaa uongozi wa Bunge umekanusha madai hayo na kutunisha misuli kuulinda muhimili huo, madai hayo yamezidi kuongezeka.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe ameibua hoja 10 anazodai zinaonyesha udhaifu wa chombo hicho huku akisema hali hiyo haijawahi kutokea katika historia ya Tanzania.

Wiki iliyopita, Zitto alitoa hoja hizo mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge akisisitiza kuwa Bunge hilo limeingiliwa na mhimili wa Serikali, linapangiwa cha kufanya na namna ya kuisimamia Serikali.

Mengi aliyoyaeleza Zitto si mapya, yamekuwapo ya wabunge wamekuwa wakiyasema, lakini alichofanya ni kuyakusanya kujenga uzito wa hoja yake kuwa chombo hicho kimejisalimisha kwa Serikali kinyume na inavyotakiwa kuwa.

Kabla ya tukio hilo, Mbunge huyo alikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) akitokea Kigoma baada ya kuitwa na Kamati hiyo kwa agizo la Spika wa Bunge, Job Ndugai kutokana na maoni yake kwenye mitandao ya kijamii akimkosoa kiongozi huyo.

Hii si mara ya kwanza tangu kuanza kwa Bunge la 11 kwa wabunge wa upinzani kuibua tuhuma kama hizo huku wakijenga hoja zinazoakisi udhaifu wa Bunge hilo. Vilevile, hata jicho la watu walio nje ya Bunge wanaeleza hisia zao zinazoonyesha hali hilo.

Aliyekuwa Katibu mkuu wa NCCR-Mageuzi, Samwel Ruhuza anasema si wapinzani tu, hata mwanaCCM wanaona na kutambua udhaifu huo lakini wamekuwa waoga wa kukiri mbele ya wananchi.

Ruhuza anasema sababu ya kutokiri udhaifu inachagizwa na woga wa wabunge wengi wa chama hicho.

“Kinachosikitisha zaidi, baadhi ya wanaCCM wanaopinga udhaifu wa Serikali au Bunge wanatengwa, si wenzao. Mfano, Nape Nnauye aliponzwa na msimamo wake wa kukosoa udhaifu wa Serikali, wabunge wengine wameamua kuangalia masilahi yao tu na huo ndiyo usaliti kwa Watanzania waliowatuma bungeni,” anasema Ruhuza.

INAENDELEA UK 26

INATOKA UK 25

Ruhuza anasema wananchi wanatakiwa kutambua kuwa Bunge si chombo chao bali ni chombo kinachotumiwa na CCM na Serikali yake, na kutolea mfano wa muswada binafsi wa Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia wa kutaka kuongeza muda wa ukomo wa urais na ubunge hadi miaka saba.

Anasema hata mapendekezo yaliyokuwa kwenye rasimu ya Jaji Warioba, kuhusu wananchi kumwajibisha mbunge wao na vipengele vya maadili waliviondoa.

“Kwa hatua hiyo, Bunge ni la wananchi au la CCM?” anahoji.

Ruhuza anasema matokeo ya haki wananchi kukosa taarifa sahihi kuhusu mwenendo wa Serikali ili kuiwajibisha kupitia uchaguzi.

Mwenyekiti wa Baraza la Katiba Zanzibar, Profesa Abdul Sherrif anasema kwa mamlaka aliyopewa rais kikatiba ni hatari na vigumu kwa Bunge kuisimamia Serikali.

Profesa Sherrif anasema tatizo hilo lilibainika miaka mingi ndani ya Bunge hilo na ndiyo sababu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyokuwa chini ya Jaji Joseph Warioba ilikuwa imepunguza baadhi ya madaraka ya rais ili kuimarisha uhuru wa chombo hicho.

“Bunge linapokuwa katika hali hii ni vigumu kubadilika bila Katiba, na hali hii imekuwa ni tatizo la nchi nyingi Afrika,” anasema Profesa Sherrif.

Hata hivyo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbas anakanusha madai ya Serikali kuliingilia Bunge akimtaka Zitto kuchukua hatua kama sheria zimevunjwa.

“Serikali ina majukumu yake, inatoa bajeti kwa Bunge, huko ndiyo kuingilia Bunge? Bunge linatunga sheria ndiyo tuseme linaingilia mahakama? Mahakama inapotafsiri sheria inaingilia Bunge? Hii mihimili haiwezi kufanya kazi in isolation (kwa kutengana).

Kuhusu madai Serikali kuhusika na shambulio la Lissu (Tundu), Dk Abbas anamtaka Zitto kusubiri uchunguzi wa Serikali badala ya kujadili hisia.

Kilio cha wapinzani

Siku chache zilizopita, Spika Zitto kwamba, anao uwezo wa kumzuia asizungumze ndani ya vikao vyote vya Bunge hilo hadi muda wake kumalizika.

Mbali na hilo, tayari wabunge wawili, Halima Mdee na Ester Bulaya wanatumikia hukumu itakayoweka nje ya mikutano minne ya Bunge hilo la 11 kutokana na adhabu ya Spika Ndugai kwa madai ya kukosa nidhamu.

Wabunge wengine waliowahi kusimamishwa kwa vipindi tofauti ni Zitto, Godbless Lema (Arusha Majini), Tundu Lissu (Singida Mashariki), John Mnyika (Kibamba) na Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini).

Si hayo tu, Bunge la kumi na moja limeweka rekodi ya kushuhudia askari wa polisi wakiingia kuwaondoa kwa nguvu wabunge ama baada ya kutofautiana na hoja na Spika au kupinga mambo fulani ndani ya ukumbi huo.

Mei 30, mwaka jana wabunge saba wa upinzani walisimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa vipindi tofauti baada ya kupatikana na hatia ya kukiuka kanuni na kusababisha vurugu bungeni.

Chanzo chake

Wakati Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa George Shumbusho anasema hali hiyo inachagizwa na uvumilivu mdogo wa kisiasa, ujana na masilahi binafsi ya vyama, mwenzake wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda anasema huo ni mpasuko unaotokana na kukomaa kwa itikadi za uchama zaidi kuliko hoja zinazojadiliwa.

Mbunda anasema hali iliyofikia ni kiti kutumia mamlaka yake kuwakomoa wapinzani wanapojaribu kuibua hoja dhidi ya chama kilichopo madarakani.

“Maamuzi yanayotolewa na lugha chafu zinazotolewa zinatafsiri wazi hali ya kutokuheshimiana. Uchama umefikia hatua ya kuharibu ladha ya Bunge. Nilitegemea kuona busara zaidi ya kiti cha Spika, kinachoendelea na vita ya kukomoana,” anasema.

Pamoja na mazingira hayo, Mbunda anaunga mkono nadharia ya kuendelea kwa misuguano hiyo akisema ni njia ya kutafuta suluhu kwa miaka ijayo.

“Kuna nadharia ya Mao Zedong, ‘contradiction’ akimaanisha kwamba, migogoro siyo mibaya, ni lazima itokee ili kujifunza kwa hapo baadaye,” anasema.

Pia, tatizo hilo linaweza kutokana na mfumo wa Bunge lenyewe na uongozi wa Bunge kuwa sehemu ya uongozi wa chama kinachotawala.

Ibara ya 62 ya Katiba ya mwaka 1977 inaeleza kuwa Bunge ni chombo cha uwakilishi wa wananchi na Bunge hilo litakuwa na sehemu mbili, yaani Rais na wabunge.

Kwa mujibu wa ibara hiyo, Rais kama sehemu moja ya Bunge atatekeleza yote aliyokabidhiwa na Katiba huku sehemu ya pili ya Bunge ikiwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Katiba”

Pili, kwa mujibu wa Ibara ya 66 ya Katiba ya mwaka 1977 kama ilivyorekebishwa chini ya mabadiliko ya 5 na 14 kwamba, kuhusu aina sita za wabunge, kuna kundi la wabunge wasiozidi (10) wa kuteuliwa na Rais.

Aidha, kuna wabunge ambao ni mawaziri wanaoteuliwa na Rais, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye huingia bungeni kwa nafasi yake baada ya kuteuliwa a Rais.

Pia, katika Bunge la sasa Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alipata sifa ya kuchaguliwa kushika nafasi hiyo baada ya kuteuliwa na Rais John Magufuli kuwa mbunge.

Kwa upande mwingine, Spika wa Bunge anayetokana na CCM anakuwa mjumbe wa vikao vyote vya juu vya chama na anaingia kwenye kamati ya wabunge wa CCM.

Suluhisho pekee

Suluhisho la matatizo hayo ni upinzani kujijenga na kuongezeka kwenye chombo hicho ili kuweka uwiano ulio sawa na pengine kuwa na uwezekano wa kumwondoa spika kama anatenda kinyume na Katiba, jambo ambalo kwa sasa haliwezekani.

Kutokana na mazingira hayo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kufuatilia mwenendo wa Bunge, Albanie Marcosy, alikaririwa na gazeti hili hivi karibuni akisema kwa sasa hakuna uwezekano wa kumwondoa Spika au Bunge hilo kuongozwa na upinzani hadi pale Katiba mpya itakapopatikana au upinzani utakapokuwa na wabunge wengi.

Kwa mujibu wa Katiba, utaratibu wa kumwondoa Spika au Naibu Spika madarakani unatajwa katika Ibara ya 85(4) pamoja na Kanuni ya 138 (1) ya kanuni za kudumu za Bunge.

Hata hivyo, kanuni ya 138 (3), inamtaka Spika kukalia kiti wakati wa mjadala wa hoja ya kumwondoa madarakani Naibu Spika.

Katika Bunge la Kumi, wabunge wa upinzani akiwamo Tundu Lissu waliwasilisha hoja tisa za kumwondoa madarakani Job Ndugai (wakati huo akiwa naibu spika), lakini hadi Bunge hilo linavunjwa hakuna hata hoja moja iliyojadiliwa.

Juni mwaka jana, Spika Ndugai aliwasilisha kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, ombi la Ukawa la kumng’oa naibu wake Dk Tulia baada ya wapinzani hao kuainisha hoja sita za kumng’oa madarakani kutokana na kuvunja kanuni za Bunge hilo, kuonyesha upendeleo, kutumia lugha za maudhi na kuonyesha upendeleo kwa wabunge wa CCM, ambayo hata hivyo haikuzaa matunda.