Ijue ‘dawa’ sahihi ya kutokomeza uvivu sugu kazini

Muktasari:

  • Siyo kwamba wanaofanikiwa wanafanya kazi dunia nyingine la hasha. Sehemu kubwa ya wanaofanikiwa wanajituma zaidi kikazi kwa kuziishi ndoto zao huku wakitafuta suluhu mbadala kila wanapokumbana na vikwazo.

Nuzulack Dausen, Mwananchi [email protected]

Kila siku tunaamka asubuhi kwa ajili ya kuanza pilikapilika za kupambana na hali zetu za maisha. Katika mihangaiko hiyo ya kila siku, baadhi yetu wanafanikiwa kutimiza malengo yao na wengine hawafanikiwi.

Siyo kwamba wanaofanikiwa wanafanya kazi dunia nyingine la hasha. Sehemu kubwa ya wanaofanikiwa wanajituma zaidi kikazi kwa kuziishi ndoto zao huku wakitafuta suluhu mbadala kila wanapokumbana na vikwazo.

Upande wa pili wa wale wanaofeli kila mara kuna vitu wanavifanya kinyume na wanaofanikiwa.

Hata hivyo, miongoni mwa sababu kubwa zinazofanya watu wengi wasifanikiwe ni uvivu. Uvivu una hatua za ukuaji. Kuna uvivu unaochipukia, uvivu ‘kijana’ na uvivu sugu.

Kama ilivyo kwa tabia nyingine za binadamu, uvivu unajengwa na mtu husika kutoka ule unaochipukia hadi sugu.

Baadhi ya watu vivu sugu huanza tangu wakiwa watoto wadogo kutokana na malezi hafifu ya wazazi au walezi wao.

Madhara ya uvivu ni makubwa kwa maisha ya mwanadamu kiafya, kijamii na kiuchumi.

Mvivu yeyote anapata shida kuanzia kwenye kuutunza mwili wake hadi kazini kwake. Hakuna jambo litakalokuwa rahisi kwake.

Hata hivyo, uvivu unaweza kutokomezwa na kumrudisha mtu husika katika ari ya uchapakazi na kuchochea mafanikio yake. Miongoni mwa tabia zinazoweza kuutokomeza uvivu sugu ni kuwa na malengo.

Utaratibu wa kupanga malengo unasaidia kupata dira kwa kila myu akifanyacho. Panga malengo katika nyanja zote za maisha kuanzia mipango ya afya, kijamii na kiuchumi.

Weka muda pendekezwa utakaokuwa na ukomo wa kufikia malengo husika. Mfano, kama ni mfanyakazi ainisha malengo binafsi unayotaka kufikia kazini na maisha binafsi.

Kwa malengo ya kazini ambayo mara nyingi huwa na muda maalumu wa kuyafikia, yabainishe wazi na ikiwezekana punguza muda wa kuyafikia.

Fanya hivyo pia kwa malengo binafsi kama ni kuanzisha biashara ndani ya kipindi cha miezi mitatu, ufanye hivyo huku ukitekeleza mikakati ya kulifikia lengo hilo ikiwamo kutafuta mtaji na wateja. Malengo yenye ukomo wa muda wa kuyafikia yanaleta hamasa ya kujituma wakati wote na yanapunguza tabia ya ubongo kujisemea “aaah nitayafikia tu muda bado”.Hamasa hiyo inakufanya muda wote utafute mbadala kwa kila kitu kinachokukwamisha ili mradi ufikie malengo yako.

Tabia hii inaondoa moja kwa moja uvivu sugu unaochelewesha mafanikio kutokana na mawazo ya kuwa siku zote muda upo.

Amka mapema kila siku

Tabia ya kuchelewa kuamka ni moja ya kiashiria kikubwa cha uvivu sugu.

Huanza taratibu na mwisho huwa tabia inayomfanya mtu akose fursa lukuki katika maisha.

Uvivu wa kuchelewa kuamka huwafanya watu kuchelewa kazini na kwenye mikutano. Unafanya watu wafanye vitu kwa haraka bila umakini kwa kuwa wana muda mfupi wa kujiandaa na kutekeleza kazi zao.

Ili niwahi kazini na kupata muda wa kufanya mazoezi asubuhi, mapema mwaka huu nilipanga kuamka Saa 11 alfajiri.

Niliseti simu yangu iniamshe muda huo. Uamuzi huu ulikuja baada ya kujikuta nalala hadi Saa 12.30 asubuhi kiasi cha kunifanya nichelewe kazini siku kukiwa na foleni kubwa.

Nilibaini siku nikichelewa kuamka kiwango cha utendaji kazi pia kinashuka tofauti na siku ninazowahi kufika ofisini.

Japo inakuwa ngumu kwa siku za mwanzo, lakini ukizoea inakuwa sehemu ya maisha yako na unapata muda mwingi wa kufanya kazi.

Mtaalamu wa Baiolojia wa Chuo Kikuu cha Havard nchini Marekani, Christoph Randler 2008 alibaini katika utafiti wake, watu wanaoamka mapema huwa makini zaidi na wanatumia muda mwingi kutekeleza malengo yao kuliko wale wanaochelewa kuamka.

Jihadhari na vikao vinavyopoteza muda

Unaweza kuwahi kuamka ukiwa na malengo madhubuti katika kazi na maisha yako, lakini kwa bahati mbaya mfumo wake wa kushiriki vikao vya kikazi au vya kijamii ukakufanya ushindwe kufikia mipango yako. Tabia ya kuendekeza vikao virefu visivyo na ulazima, hugeuka kuwa uvivu sugu.

Jaribu kufikiri, upo kazini umetingwa na majukumu na ghafla anakuja mtu aliyemaliza kazi zake anaanzisha mazungumzo yasiyo ya kikazi unayojikuta yanaenda zaidi ya nusu saa. Muda huo ambao umeupoteza hauwezi kurudi na haukuwa kwenye mipango yako.

Pia, kuna baadhi ya vikao ofisini huwa virefu bila ya ulazima. Jaribu kushauri wenzio kufupisha ili mpate muda wa kuyatekeleza mnayoyajadili. Jiwekeeni utaratibu wa kuwa na mtunza muda anayekumbusha kila wakati.

Kama wewe ni mwenyekiti wa kikao, hakikisha hamtoki nje ya mada ili kulinda muda. Wajumbe pia mnatakiwa kumkumbusha mwenyekiti juu ya jambo hilo. Ukikaa kimya, wewe ndiye utakayeathirika na upotevu huo wa muda ambao baadaye wakati wa tathmini ya kazi utahesabika kuwa ni sehemu ya uvivu sugu.

Ili kufanikiwa hili, ni vema ukapanga ratiba ya kazi zako na masuala ya kijamii.

Hakikisha kila kikao kipo kwenye ratiba isipokuwa vile vya dharura ambavyo kwa namna nyingine huwezi kuvikwepa.

Kwa vikao vinavyohusu watu wawili na vinahitaji kutoka nje ya ofisi, jaribu kuvifanya kwa kutumia teknolojia ya video kama Google Hangouts, Skype au Whatsapp.

Teknolojia kwa sasa inaokoa muda na fedha na inakufanya ufanye kazi nyingi na vikao vingi ndani ya muda mfupi.

Usipuuze vitu vidogo vidogo

Uvivu huanza na kupuuza vitu vidogo vidogo katika maisha na baadaye hugeuka kuwa tabia sugu inayopuuza mambo makubwa.

Mfano, ni rahisi mtu kuamka na kutotandika kitanda. Tabia hii inakua hadi kwenye maeneo mengine ya maisha. Anakunywa chai na kuacha kikombe juu meza nyumbani. Baadaye tabia ya kuacha vikombe bila kuosha inahamia ofisini. Anaweza kuacha vifaa vya kazi vimezagaa kwa sababu tu “kuviweka vizuri kutampotezea muda”.

Ufanyaji wa mambo unayodhani ni madogo unakufanya uwe mwajibikaji kila wakati.

Mtu anayepuuza vitu anavyodhani ni vidogo siku moja vitamgharimu kupata vikubwa. Uzembe huo ni matokeo ya uvivu.

Hivyo, ukitaka uondokane na uvivu sugu anza kufanya vitu unavyohisi ni vidogo. Amka asubuhi na utandike kitanda vema. Weka kila kitu mahali pake chumbani kwako.

Kwa wale waliooa au kuolewa hawana budi kusaidiana katika kujenga tabia hii ya uwajibikaji.

Baada ya muda mfupi uvivu utatoweka maeneo yote na utakuwa mtu mwenye kiwango kikubwa cha uzalishaji.

Hii inasaidia hata kwa viongozi ofisini kubaini tabia za kizembe na kama zitaachwa, huigharimu kampuni kiutendaji au wakati mwingine huleta hasara kubwa ya fedha.

Kwa kuwa sehemu kubwa tunafanya kazi ama za kujiajiri au kuajiriwa ili kujiingizia vipato ni vema tukautokomeza uvivu.

Ukiukabili ni rahisi kufanya vema kwenye kila nyanja ya maisha.

Uvivu unatufanya tuziweke rehani afya zetu kwa kushindwa kufanya mazoezi kila wakati.

Unatufanya tukose fursa muhimu za maisha kwa kuchelewa kufika kwenye mikutano ama kazini.

Unafanya tuchelewe kutimiza ndoto zetu kwa dhana tu muda upo na kubwa kuliko yote unatufanya tuwe walalamikaji wakubwa na kujiaminisha kuwa hatukubarikiwa kuwa na maendeleo.Wachapakazi wanafanikiwa kwa sababu wana malengo, hawapotezi muda, wanajali kila kitu vikiwamo vile unavyoona ni vidogo na huamka mapema kwa kuwa kulala sana kwao ni kutafuta umaskini.

Nuzulack Dausen ni Mwandishi mwandamizi wa biashara na teknolojia wa Mwananchi Communications Ltd (MCL) +255714382434/ 0764176793