Itapendeza Azory Gwanda akirejeshwa hai, salama

Muktasari:

  • Azory Gwanda ni mwandishi wa habari, tasnia nyeti na muhimu kwa maendeleo ya nchi. Unyeti na umuhimu wa kazi hii umejadiliwa sana na wasomi mbalimbali duniani katika machapisho na makongamano.

Nisijifanye kumjua sana Azory Gwanda. Kwa kweli hatufahamiani na naamini hatujawahi kuonana popote. Lakini jambo moja ni hakika. Kupotea kwake katika mazingira ya kutatanisha kuna athari kubwa kuliko madhara tunayoyahofu kutokea kwake yeye binafsi.

Azory Gwanda ni mwandishi wa habari, tasnia nyeti na muhimu kwa maendeleo ya nchi. Unyeti na umuhimu wa kazi hii umejadiliwa sana na wasomi mbalimbali duniani katika machapisho na makongamano.

Vyombo vya habari vimebatizwa kuwa ni mhimili wa nne wa dola katika mazingira ya utawala wa nchi za kidemokrasia, ukiungana na mihimili mingine mitatu kutekeleza udhibiti wa tawi moja dhidi ya jingine: Matawi hayo ni Serikali inayotekeleza sera kutokana ilani ya chama tawala, Bunge linalotunga sheria na Mahakama inayogawa haki.

Kwa upande wake, vyombo vya habari ni mhimili muhimu ambao unapasha habari wananchi, unaelimisha na kuburudisha. Si hivyo tu, vyombo vya habari vina jukumu muhimu sana la kukosoa na kuibua uozo serikalini na kwingineko, na ndio maana vikaitwa ‘watchdog’ yaani mlinzi.

Vyombo vya habari vinalinda tunu, masilahi na maadili ya nchi, na vinapaza sauti pale ambapo mambo hayaendi sawa. Vyombo vya habari ni jukwaa la mijadala. Na kama si mijadala huru, ni nini basi demokrasia? Vyombo vya habari pia vinawasemea wanyonge. Kwa hiyo kwa viongozi wapenda kweli na watenda haki, vyombo vya habari ni rafiki mzuri.

Lakini, ili vifanye kazi sawasawa na kuleta matokeo chanya, yaani kuimarisha demokrasia, kusimamisha utawala bora, kuleta uwazi na kuchochea mijadala huru na hatimaye maendeleo, vyombo vya habari vinafaa kuwa huru na watendaji wake wanafaa kuachiwa kutumia akili zao wakiongozwa na weledi, sheria na maadili ya taaluma.

Ni kwa sababu hii ndiyo maana vyombo vya habari huru vimetajwa kuwa ni moja kati ya nguzo muhimu za demokrasia. Kwa maoni yangu hakuna namna unaweza kujenga demokrasia bila vyombo vya habari huru na vyenye malengo tofauti.

Tatizo ni kwamba, kunapotokea matukio mabaya, mfano wa hili la kutekwa mwandishi Azory, dhana ya kwanza inayokuja akilini mwetu, sisi waandishi ni kuwa amefanyiwa hivi kwa sababu ya kazi yake, kwa sababu kinyume na kazi nyingine, uandishi wa habari ni taaluma ambayo sisi tunaoifanyia kazi kiasili ni rahisi kutengeneza maadui kwa kuwa tunaandikia kuhusu watu.

Dhana na hisia hizi, kwamba kazi ndiyo iliyomponza Azory, zinatupelekea kuingiwa na woga. Tunahisi kuwa, kumbe tukifanya kazi yetu vile itakiwavyo, kuna watu hawapendi. Tena si tu wanachukia bali wanapanga kutudhuru.

Mara waandishi tunaanza kuchuja tunachoandika, tena mchujo usio wa kiweledi, mchujo ambao si wa kutumia sheria zinazoongoza tasnia yetu na wala si kwa sababu ya maadili yanayotuongoza, bali mchujo wa kujaribu kuwafurahisha tu wale tunaowahisi wanatufuatilia, yaani mchujo wa kulinda usalama wetu. Katika hali hii yale matokeo tarajiwa – ujenzi wa demokrasia, utawala bora na hatimaye maendeleo - hatuwezi kuyafikia.

Kupotea kwa Azory kunaweza kukawa na maelezo mengi tofauti, lakini madhali yeye alikuwa mwandishi, dhana hiyo niliyoitaja hapo juu – kwamba kupotea kwake kunahusiana na kazi yake - haiwezi kufutika vichwani mwa waandishi mpaka ikithibitika vinginevyo. Na isipothibitika vinginevyo, wasiwasi hautatuisha.

Wasiwasi wa waandishi utawafanya waogope kuandika kila aina ya habari inayosema watu vibaya maana hatujui nani aliyehusika katika kumpoteza Azory. Anaweza kuwa yoyote aliyewahi kuandikwa au kutajwa vibaya. Katika mazingira hayo, namna gani bora ya kujihami zaidi ya kuzikwepa habari za kuudhi watu?

Utakapokwepa habari za kuudhi watu na kuandika za kuwajenga na kuwapamba waonekane wazuri, hapo tunaingia katika fani nyingine inayoitwa Uhusiano wa Umma (Public Relations). Unakuwa huandiki tena habari bali unatoa matangazo.

Kuna mtaalamu mmoja aliwahi kusema, habari ni ile ambayo kuna watu fulani hawataki itolewe, mengine yaliyobaki ni matangazo, na ndiyo maana si bahati mbaya ilipotokea kwamba mamlaka zilichukia hadi wakamkamata kijana mmoja kwa kusambaza habari za kuwapo nyufa katika hosteli mpya za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Nimetaja kuwa kuna habari halisi, habari za wananchi zinazoibua mijadala na kusababisha wenye mamlaka kuwekwa kiti moto kujieleza na hata kuwajibika, kama ilivyokuwa kwenye habari ya nyufa za hosteli. Kinyume chake, kuna habari kutoka kwa wenye mamlaka kwenda kwa wananchi, habari ambazo wanaozitoa wamezitengeneza vizuri ili kujijengea taswira waitakayo katika jamii, wakiremba na kutaja mazuri tu ya taasisi zao au wao wenyewe.

Je, Serikali itaridhika na kupendezewa kama waandishi wajikite kwenye kuandika habari kutoka vyanzo vya mamlaka tu, au kukwepa kuandika habari za uovu na waovu badala ya kutoa habari za wananchi zenye athari na ambazo zinaenda kuleta mabadiliko katika jamii?

Kama Serikali haitaki haya yatokee, kama inathamini mchango wa vyombo vya habari, kama inaviona vyombo vya habari kama washirika, basi ni vema Serikali iongeze nguvu na kutoa kipaumbele katika kuhakikisha inampata Azory na anarejea akiwa mzima na salama na pia iwahakikishie waandishi usalama wao siku za usoni kwa kuwalinda kwa namna yoyote.

Ni kwa masilahi ya Serikali kuongeza nguvu katika kumtafuta Azory kwa sababu mara nyingi matukio kama haya ya kupotea waandishi yanaharibu taswira ya nchi duniani kwa sababu waandishi wa habari wana mtandao mpana wa kupeana taarifa kama hizi. Mbaya zaidi vyombo vya habari vya nje vinaweza kuipaka Serikali matope kwa kuituhumu kuhusika.

Tasnia ya uandishi wa habari ina matatizo tayari ya kutosha, kabla hata ya kuongeza hili la mwandishi kupotea. Weledi uko chini, vipato vya waandishi ni duni kiasi cha kuwafanya waombeombe na kujihusisha na rushwa, elimu na ufahamu wa baadhi yao ni mdogo, kibano kutoka serikalini nk. Kama changamoto hizi zilifanya tasnia ichechemee, bila shaka hili la mwandishi kupotea – kama hamna ufumbuzi - litadumaza kabisa tasnia.

Nikiangalia mustakabali wa fani hii ya uandishi wa habari, kama Azory hatapatikana, naona uwezekano wa ongezeko la kasi ya waandishi makini kutafuta kazi za uofisa habari kwenye makampuni na serikalini na vilevile kuongezeka kwa umaarufu wa mitandao ya kijamii na matumizi ya majina ya uongo mitandaoni.

Ushauri kwa waandishi katika tasnia nzima. Tusimame kukemea jambo hili. Tusiwe kama yule jamaa aliyeona wenzake wanafuatwa kuuliwa akawabagua, kwa kuwaita ‘ahh hao ni wajamaa ndiyo wameuawa, mara ahh hao Wayahudi ndiyo maana, kisha wakauawa wote. Ilipofika zamu yake kuuawa, hakukuwa na wa kumtetea.

Mliomshikilia Azory Gwanda, hakika itapendeza mkimuachia akiwa hai na salama na salama ya nchi.