JICHO LA MWALIMU : Kiasili mwalimu ni kiongozi

Muktasari:

Kundi la pili, ni lile la watu ambao hawana karama ya ualimu; lakini walipata fursa ya kusomea taaluma hiyo na kubadilishwa kifikra na kuuvaa uhalisia wa ualimu kivitendo na kimaadili.

Yapo makundi matatu ya walimu; kundi la kwanza ni lile la watu ambao walizaliwa wakiwa na kipaji cha ualimu na kisha wakapata fursa ya kusomea taaluma hiyo.

Kundi la pili, ni lile la watu ambao hawana karama ya ualimu; lakini walipata fursa ya kusomea taaluma hiyo na kubadilishwa kifikra na kuuvaa uhalisia wa ualimu kivitendo na kimaadili.

Kundi la tatu, ni la watu ambao hawana karama ya ualimu lakini walipata fursa ya kuisomea kama taaluma; bahati mbaya hawakubadilishwa kifikra ili kuuvaa uhalisia wa taaluma hiyo.

Katika muktadha huo, jamii itegemee kuona tofauti kubwa ya walimu hao wanapokuwa wakitenda kazi zao kila siku. Mwalimu ambaye hupatikana katika kundi la kwanza na la pili, huweza kuwa mwalimu bora kuliko anayetokana na kundi la tatu.

Mwalimu bora kwa asili huweza kuwa kiongozi bora. Makala haya yanamwangazia mwalimu mwalimu bora kama kiongozi bora.

Akizungumzia falsafa ya ualimu na uongozi, Katibu Msaidizi wa Tume ya Utumishi wa Walimu Manispaa ya Dodoma (TSC),anasema kifalsafa, uongozi ni kukubali, kuelewa hali, kuondoa upendeleo, kuondoa, kunena thabiti, kugawa madaraka, kuonyesha kwa mfano, kuzuia migongano na kuinua kiwango cha utendaji.

Falsafa ya mwalimu bora kama kiongozi bora; hubebwa na herufi zinazounda neno K-I-O-N-G-O-Z-I. Kama ambavyo uchambuzi wake unafanyika hapa chini.

Herufi ‘K’ hutafsiriwa kama kukubali ushauri au kushauriwa. Mwalimu bora na kiongozi mzuri hupima ushauri na kuukubali au kuukataa kwa nguvu ya hoja na siyo hoja ya nguvu.

Ushauri huo huenda ukatolewa na wanafunzi wake, wazazi, walezi au wadau mbalimbali wa elimu.

Mwalimu huyu huweza kuiambukiza tabia hiyo kwa wanafunzi wake na kuwa na uwezo huo. Kukubali ushauri na kushauriwa jambo jema ni uungwana.

Herufi ‘I’ husimama kama ‘ielewe’ hali ya maisha ya mahali ulipo na unaowaongoza. Mwalimu bora hawezi kushindwa kuishi na jamii yoyote atakayopaswa kuitumikia. Mwalimu huyo huwa na uwezo mkubwa wa kuchagiza mabadiliko na maendeleo katika jamii husika.

Katika hili, jamii na mamlaka husika zinapaswa kuwekeza katika mafunzo ya vitendo kwa walimu kwa kuongeza muda wake.

Herufi ‘O’ husimama kama ‘ondoa’. Herufi hii humlazimisha mwalimu bora kama kiongozi kuondoa upendeleo, uonevu na ubaguzi kwa anaowaongoza. Mwalimu bora hategemewi kuonyesha ubaguzi wowote kwa baadhi ya wanafunzi wake, kwani wote huwa sawa mbele yake bila kujali hali zao.

Herufi ‘N’ humaanisha ‘nena’. Herufi hii humlazimisha mwalimu bora au kiongozi kunena kauli thabiti daima. Mwalimu bora siyo mtu wa kuukwepa ukweli na kuufundisha.

Herufi ‘G’ humaanisha ‘gawa’. Herufi hii humtaka mwalimu au kiongozi kugawa madaraka kwa anaowaongoza. Kwa mfano, walimu wamekuwa wakishirikisha madaraka kwa wanafunzi wao kupitia serikali za wanafunzi shuleni au vyuoni. Sehemu nyingine wapo watu ambao ni wakurugenzi na chini yao wapo meneja na wahasibu, lakini cha ajabu hutokuta majukumu ya meneja au mhasibu yanafanywa na mkurugenzi.

Ni vema kiongozi anayejiamini akawaamini na wenzake na kuwapa fursa ya kukua kiuongozi.

Herufi ‘O’ humaanisha ‘onyesha’. Herufi hii humtaka mwalimu bora au kiongozi kuonyesha mfano kwa vitendo. Walimu wengi bora hufanyika kuwa wa mfano katika shughuli mbalimbali za maisha za kila siku.

Walimu wengi bora wamekuwa wakitumia njia na mbinu shirikishi ili kuweza kuwajengea wanafunzi wao stadi muhimu katika mada husika.

Herufi ‘Z’ humaanisha ‘zuia’. Herufi hii humtaka mwalimu bora au kiongozi kuzuia migongano, chuki, fitina, majungu au umbea.

Tabia hizi zinapoendelezwa katika shule au sehemu za kazi, husababisha utendaji mbaya na kutengeneza makundi. Kukiwa na makundi kazini au shuleni, shughuli huwa haziendi ipasavyo.

Kwa mfano, walimu wanaweza kuchukua hatua za kuzuia tabia zisizofaa kwa wanafunzi kwa kufahamu hatua za mabadiliko yao katika makuzi na tabia, kwa kutoa ushauri na elimu ya mabadiliko ya mwili. Pia, kwa kuwa karibu na wanafunzi wao, wanaweza kuwafahamu vema na hata matatizo yao, hivyo kuwashauri ipasavyo

Herufi ‘I’ humaanisha ‘inua’. Herufi hii humtaka mwalimu bora au kiongozi kuinua kiwango cha utendaji kazi kwake na kwa anaowaongoza.

Mwalimu bora huwatia ari wanafunzi wake vivyo hivyo kwa kiongozi bora. Huwa na uwezo wa kutatua matatizo yanayowakabili wanafunzi wake na kutengeneza mazingira rafiki ya utendaji kazi.

Mwalimu bora ni mwanafunzi wa kudumu, daima hujifunza bila kukoma. Hutafuta maarifa kwa kusoma, kutafiti na kufanya majaribio kwa vitendo kwani hufahamu kuwa pasipo kufanya hivyo anaweza kupitwa na maarifa mapya. Kama mwalimu atafanya hivyo,ni dhahiri tabia hiyo ataiambukiza kwa wanafunzi wake bila ya kutumia nguvu.

Tafsiri hii ya falsafa ya uongozi na misingi ya kiutendaji inayoonyeshwa na walimu bora huweza kuonekana kuanzia kwa mtu binafsi mpaka ngazi ya kitaifa.

Ni wajibu wa walimu popote pale walipo kuchukua hatua za dhati za kuwafanya waendelee kuheshimika, kuthaminiwa, kuaminika, kuigwa na kuonya.

Kwa muktadha huo, ni vema mamlaka zinazosimamia mafunzo ya walimu kuhakikisha walimu wanapikwa na kuivishwa ipasavyo.

Aidha, wanapokuwa kazini, waendelee kupatiwa semina na mafunzo kazini ili viwe chachu ya kuwakumbusha na kukuza umahiri na uweledi. Hii itasababisha tupate taifa imara, taifa la viongozi bora watakaokuja kuliendeleza pale wengine walipoishia.

Jamii inapopata kiongozi ambaye hapendi kushauriwa, huwa ni matokeo tu ya jamii hiyo na namna inavyoendeleza mkufu wa matatizo kwa vizazi vijavyo.