JICHO LA MWALIMU : Ukimkosea mtoto umelikosea taifa zima

Joseph Chikaka

Muktasari:

  • Ukweli ni kwamba watoto wengi wamekuwa wakikosewa na watu wazima kwa makusudi ama kwa kutofahamu.

Watu wazima wengi hufikiri kuwa wao ndiyo hukosewa na watoto.

Ukweli ni kwamba watoto wengi wamekuwa wakikosewa na watu wazima kwa makusudi ama kwa kutofahamu.

Mara nyingi tumesikia na kushuhudia watu wengi wakiwalaumu vijana kuwa hawajitumi, hawana maadili mema, hawapendi kazi, hawataki kuchangamkia fursa na wala hawana ndoto za maisha yao.

Kati ya wanaolalamika, hawajawahi kujiuliza kwamba, “hivi, hao vijana na wahitimu, wameshushwa tu kutoka mbinguni ama hutokana na jamii yao inavyoishi?”

Kama vijana hutokana na jamii yao, kwa nini watu wamejikita katika kutazama majani ya mti ambayo ni matokeo; na kusahau kuwa ili mti ustawi vema ni vizuri ukahudumiwa kwa kutunzwa vizuri tangu ukiwa mdogo.

Kama mti hautotunzwa vizuri, watu wasitegemee kupata matunda bora.

Vivyo hivyo, kwa vijana wote hutokea utotoni. Kama jamii inahitaji kumpata kijana mwenye sifa zinazohitajika na taifa, jamii haina budi kuwekeza katika malezi na makuzi ya utotoni.

Katika mchakato huo, wajibu wa makundi haya yafuatayo hayakosekani; wazazi, walezi, watoto wenyewe, walimu, jamii, mazingira na mifumo inayomzunguka mtoto, ikiwamo sera na sheria, mila na desturi zinazomlinda ama kumkandamiza

Nafasi ya mwalimu katika kumfinyanga mtoto

Mwalimu ni kiungo muhimu katika kumwongoza mwanafunzi kufanya uchaguzi sahihi na anaoupenda.

Licha ya kufundisha, mwalimu huwajibika kama mlezi, mzazi, hakimu (mwamuzi), mratibu na msimamizi. Pia, hufanya kazi ya mtafiti, mhamasishaji na mchokonozi wa mabadiliko.

Mwalimu bora ni mtu muhimu katika ustawi wa mtoto na taifa kwa jumla. Kosa lolote la mwalimu kwa mtoto huwa halirekebishiki milele.

Mwalimu anapomkosea mtoto mdogo anakuwa ametengeneza mnyororo wa matatizo kwa mtoto na vizazi vyake vyote.

Kosa lolote au ukatili wa namna yoyote ambao mwalimu ataufanya darasani ama shuleni, utamgharimu mtoto katika maisha yake.

Utatengeneza mnyororo wa matatizo ambao utakuwa gharama kuukata.

Watoto huwaamini walimu kuliko wazazi wao. Mwalimu akimkosea mtoto na mtoto akalifyonza lile kosa katika ubongo wake, mwalimu hatapata tena uwezo wa kulirekebisha kwa maisha yote.

Hivyo, shule na walimu ambao hufundisha watoto wadogo katika elimu ya awali na makuzi, wanapaswa kuwa mahiri na wenye weledi mkubwa.

Hii ni kwa sababu, hatua hizi za awali ndio watu hutengenezwa haiba. Katika kipindi hiki, mabadiliko ya ukuaji wa mtoto kimwili na kiakili (ubongo) ni mkubwa. Kosa lolote la mwalimu hufyonza moja kwa moja ubongoni na kunasa.

Vipo visa vingi vya vijana ambao hushindwa kutimiza ndoto zao kwa sababu tu ya kutendewa vibaya katika hatua za utotoni.

Fikiri, ni madaktari, wauguzi, walimu na wataalamu wangapi jamii imewapoteza tangu wakiwa katika umri wa watoto wadogo? Ni watoto wangapi wameumizwa kwa kupewa mzigo wa chuki moyoni katika maisha yao?

Ni wazazi wangapi ambao leo hii kutokana na athari za utotoni, nao wamewatendea wale walio chini yao ukatili, kutokana tu na kosa la mwalimu mmoja aliyemtenda wakati mzazi huyo alipokuwa elimu ya awali, msingi au ngazi yoyote ile ya elimu?

Mwalimu bora huwatambua wanafunzi wake

Kunapokuwapo uhusiano mzuri kati ya mwalimu, mwanafunzi na mzazi, kunakuwa na nafasi kubwa ya kuhakikisha mtoto anafanya vizuri.

Mwalimu bora huwafahamu vizuri wanafunzi wake, mahali wanapotoka, familia zao na mazingira. Pia, hutambua kuwa wanafunzi wake hutoka katika aina mbalimbali ya familia.

Kwa muktadha wa makala haya, kuna aina tano za familia za wanafunzi ambazo mwalimu anaweza kuwa nazo darasani. Familia ya kwanza ni yenye wazazi wote yaani baba, mama na watoto; ya pili ni familia yenye mzazi mmoja yaani labda baba na watoto au mama na watoto.

Familia ya tatu ni familia yenye wazazi, watoto na ndugu; ya nne ni familia yenye mzazi wa kambo na ya tano ni familia ya yatima (isiyokuwa na wazazi) yaani ina watoto na ndugu

Ufahamu wa makundi hayo ya familia za wanafunzi humpatia mwalimu urahisi anapofundisha na kuwahudumua kwa kadri ya mahitaji ya elimu jumuishi.

Pia, humfanya awe mwangalifu kwa mifano na lugha ili asimuumize mtu. Kwa mfano, huweza kuwajengea kujiamini hasa pale anapotaka kila mwanafunzi ataje mambo mawili mazuri ambayo huyaona kwa mwenzake.

Ili tuweze kufanikiwa katika kupata vijana na taifa bora, ni vema jamii kwa kushirikina na Serikali kuwapa fursa watoto na vijana kustawi kimalezi na kimakuzi. Kwa sababu, mtu anapomkosesha mtoto, amemkosesha kijana na amelikosesha taifa kwa jumla.

Mwandishi wa safu hii ni mwalimu, mnasihi, mwandishi wa kitabu cha Watoto na ndoto za maisha. www.josephchikaka.com