Jacob: Ninacheza soka Kenya lakini sitaki kudumu hapa

Muktasari:

  • Tanzania ni miongoni mwa mataifa ambayo watu wake kwanza wana kiu ya mafanikio, pia wachezaji wake wamekuwa na kiu ya kutaka mafanikio zaidi kwa kucheza soka la kimataifa, Wiki iliyopita tuliona vile ambavyo Daud Aboud na Adolf Bitegeko walivyoipa ubingwa, LCC Men’s Soccer ya Marekani.

Kiu ya kuhitaji mafanikio kwenye soka la kimataifa ni moja ya sababu ambayo inaweza kutajwa na wachezaji wengi ambao wamekuwa wakitoka kwenye mataifa yao na kwenda kwingine kucheza soka.

Tanzania ni miongoni mwa mataifa ambayo watu wake kwanza wana kiu ya mafanikio, pia wachezaji wake wamekuwa na kiu ya kutaka mafanikio zaidi kwa kucheza soka la kimataifa, Wiki iliyopita tuliona vile ambavyo Daud Aboud na Adolf Bitegeko walivyoipa ubingwa, LCC Men’s Soccer ya Marekani.

Kwenda kwao huko ni juhudi za kutaka mafanikio,Leo tunaye Benedictor Jacob ambaye anaichezea Palos FC ya Ligi Daraja la Kwanza nchini Kenya, Palos ipo kwenye mazingira mazuri ya kupanda Ligi Kuu msimu ujao.

Watanzania wengine ambao wanacheza Kenya ni Abdul Hilal wa Tusker, Abdallah Hamis (Sony Sugar), Aman Kyata (Chemelil Sugar) za Ligi Kuu, Hamad Mbumba wa Stima FC ambayo imeshuka daraja msimu huu na Juma Mpondo wa KCB FC nayo ya Daraja la Kwanza.

Bene amezungumza na Spoti Mikiki na kusema safari yake ya soka ilivyoanza hapa nchini mpaka kufika Kenya ambapo na kwenyewe amepanga kuendelea kupatumia kama njia ili aweze kupiga hatua zaidi.

“Tupo nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi, tunahitaji kushinda mchezo wetu wa mwisho kisha walio juu yetu wapoteze ili tumalize kwenye nafasi ya tatu, kama ikiwa hivyo inamaana tutakuwa na nafasi ya kucheza mchujo.

“Mchezaji wa daraja la kwanza moja kwa moja mpaka timu ya Taifa ni jambo gumu kidogo, labla kama ningekuwa nacheza Ulaya kwa sababu ngazi ya ligi za chini Ulaya ni kubwa mno ukilinganisha na hizi za Ligi Kuu hasa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

“Kama nitafanikiwa kuipandisha timu daraja, ninajua nami nitakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuichezea Taifa Stars, inawezekana na kikubwa ni kuendelea kuwa na uvumilivu mpaka mwisho, mbona Hilal na Hamis wameitwa,” anasema Bene.

Hata hivyo Bene mwenye miaka 21 ambaye ana uwezo wa kucheza mshambuliaji wa mwisho ‘9’ au winga wa kulia ama kushoto, amesema kupata nafasi kwa Hilal na Hamis kwenye timu ya Taifa kumewafanya kuamini kuwa inawezekana.

”Mwanzo kulikuwa na ugumu wa kuita mchezaji ambaye anatoka kwenye ligi za maeneo ya karibu na Tanzania, siwezi kusema kuwa kocha alikuwa akiita timu kwa mazoea ila naona kama mlango wa fursa, umefunguliwa,” anasema mchezaji huyo.

African Lyon inaonekana ni kama kiwanda cha kutoa wachezaji wengi ambao wamekuwa na bahati ya kupata nafasi ya kucheza nje, hata Mbwana Samatta alipitia hapo kabla ya kujiunga na Simba kisha TP Mazembe.

“Mwanzo wangu kabisa ulikuwa DYOC, halafu ndiyo nikajiunga na African Lyon ambayo ilinifanya kupata nafasi ya kwenda nje kwa mara ya kwanza kwenye maisha yangu ya soka na kujiunga na AFC Lupopo ya Congo.

“Msimu wa 2014-2015 nilipata majeraha ya goti kwa hiyo ilinibidi kukaa nje mwaka mzima,nilivyopona majeraha yule mwalimu wangu wa Kituo cha DYOC, Aluko aliniambia kuna nafasi Kenya ya kujiunga na Palos.

“2016 nilijiunga nao na hadi leo bado nipo timu hiyo ya daraja la kwanza, mchezaji ni sawa na mkulima, siku zote mkulima mzuri hatakiwi kuchagua jembe, sikuona haja na mimi ya kuchagua timu,” anasema Bene.

Hata hivyo, Bene ameuzungumzia msimu huu ambao unaelekea ukingoni kwa madaraja ya chini na kudai itakuwa vyema kama watafanikiwa kuipandisha daraja timu hiyo.

“Binafsi nimeifungia timu mabao matano na kutengeneza matatu, ligi ilikuwa ngumu na nimekuwa nikicheza kwenye nafasi tofauti, kuna muda kocha anaweza kunitumia kwenye maeneo ya ulinzi, endapo labla mchezaji muhimu wa eneo hilo amekosekana.

“Wastani wa mabao niliofunga sio mkubwa ila nitauchukulia kama changamoto ya kunifanya kuongeza makali kwenye ufungaji na utengenezaji wa nafasi zaidi,” anasema Bene.

Ni ngumu kujua timu gani itapanda daraja, amesema Bene kutokana na ushindani ulivyo kwenye ligi hiyo, hakusita kusema unaweza kuipa sana nafasi timu fulani lakini mwisho wa msimu inaweza kukosa hata kwenye nafaso 10 za juu kwenye msimamo.

Bene alimalizia kwa kusema amejiwekea malengo ya kwenda kufanya majaribio miezi kadhaa ijayo ili kuona kama anaweza pia kuanza kukumbana na changamoto mpya za soka.

“Siwezi kukaa kwenye hii timu kipindi chote cha maisha yangu,hapana. Napenda sana kupiga hatua hivyo itanibidi kwa siku za hivi karibuni kwenda kufanya majaribio sehemu nyingine, nitalenga nchi za Afrika Magharibi,” anasema mchezaji huyo.