MAONI YA MHARIRI: Jaji Mutungi simamia pia kanuni za haki, wajibu wa vyama

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi

Muktasari:

Mikakati hiyo ya Chadema, licha ya kuwaibua CCM ambao ni mahasimu wao wa kisiasa, pia imemuibua Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi aliyejitoa taarifa akisema tamko la Chadema limejaa lugha za uchochezi, kashfa na kuhamasisha uvunjifu wa amani.

Kumeibuka sintofahamu ya kisiasa baada ya chama cha Chadema kutangaza mikakati mitatu ya kupinga suala inaloliona kuwa ni ukandamizaji wa haki na demokrasia, ikiwa ndani ya operesheni iliyopewa jina la Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta) na kufanya maandamano na mikutano nchi nzima kuanzia Septemba Mosi.

Mikakati hiyo ya Chadema, licha ya kuwaibua CCM ambao ni mahasimu wao wa kisiasa, pia imemuibua Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi aliyejitoa taarifa akisema tamko la Chadema limejaa lugha za uchochezi, kashfa na kuhamasisha uvunjifu wa amani.

Jaji Mutungi alinukuu vipengele kadhaa vya Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 kwenye kanuni na maadili ya vyama vya siasa za mwaka 2007.

Ni jambo jema kwamba Jaji Mutungi amefanya jitihada za kuvikumbusha vyama vya siasa umuhimu wa kufuata sheria na kanuni.

Tunakubaliana naye kwa kuwa alirejea Sehemu ya Tatu ya sheria hiyo inayozungumzia wajibu wa chama cha siasa wa kutunza maadili kwa kunukuu kanuni ya 5 (1) (d) inayovikataza vyama kutoa maneno ya uongo au maandishi ya uongo kuhusu mtu yeyote au chama chochote cha siasa.

Tunaamini kuwa kwa dhamira hiyohiyo Jaji Mutungi ataendelea kufanya hivyo kwa kugisa maeneo mengine mengi ya sheria hiyo. Mfano kanuni ya “c” inazuia matumizi ya vyombo vya dola kukandamiza na kutoa vitisho kwa chama chochote cha siasa.

Pia, kanuni “e” inaruhusu kufanya mkutano wa kisiasa na maandamano bila kufanya vurugu kwa mujibu wa sheria za nchi. Pia kifungu “f” kinavitaka vyama vya siasa kulaani na kupinga vitendo vyenye kuashiria ukandamizaji, matumizi ya lugha ya matusi, vitendo vya kibabe na vurugu, matumizi ya nguvu ili kujipatia umaarufu wa chama au sababu yoyote ile.

Pia kifungu “i” kinavitaka vyama vya siasa kuepuka kutumia mamlaka, rasilimali za Serikali, vyombo vya dola au wadhifa wa kiserikali, kisiasa au ufadhili wa nje ama wa ndani kwa namna yoyote ile ili kukandamiza chama kingine.

Tunatumaini kuwa weledi aliouonyesha Jaji Mutungi, ambaye pia ni katibu wa Baraza la Vyama vya Siasa, atauendeleza katika kusimamia haki za vyama vya siasa kama ilivyoelezwa Sehemu ya Pili ya kanuni ya 4(1) (b) kwamba chama kina haki ya kutoa maoni ya kisiasa kadri kitakavyoona inafaa ili kutekeleza sera zake kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya Zanzibar.

Hatuna shaka kwamba Jaji Mutungi atasimamia kanuni “c” ya haki ya chama ili vipate fursa ya kujadili na kushindanisha sera zake na zile za chama kingine cha siasa kwa lengo la kutaka kukubalika kwa wananchi.

Kwa weledi ule ule tunaamini atahakikisha kanuni ya “d” ya haki ya chama inatoa fursa kama ilivyotamkwa kwamba viwe na uhuru wa kutafuta wanachama na kama ni wakati wa kampeni, basi kuwe na uhuru wa kutafuta kuungwa mkono na wapiga kura. Pia, tuna hakika atasimamia kanuni “e” inayotoa fursa kwa kila chama cha siasa kuwa na haki ya kufanya mikutano ya kisiasa na maandamano kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa.

Ni vizuri Jaji Mutungi akasimamia sheria hiyo ya vyama vya siasa inayovipa haki za kufanya mikutano ya hadhara, kuandamana, kutafuta wanachama na kukemea jambo vinaloona ni la ukandamizaji ili kuondoa matatizo yanayoonekana kunyatia amani yetu.