Je, bado unapoteza muda wako kwa ‘Mr Wrong’?

Muktasari:

Unaweza pia kujiuliza inakuwaje wanawake wengi wazuri na walio makini hujikuta wakiangukia katika uhusiano usiowapa furaha na kinyume chake kujikuta wanaumia kila mara. Ni ukweli usiopingika kwamba kama umewekeza penzi, moyo na muda wako mwingi katika uhusiano mawazo ya kuachana na kuanza upya huwa yanatisha sana. Mtaalamu wa saikolojia za uhusiano Donna Dawson anasema wengi wetu wanajikuta wanaamua bora kukaa na shetani unayemjua kuliko yule usiye mjua, kwa hiyo wanaamua kuendelea kwa kuhofia wasije kuamua kuanza uhusiano mpya na kujikuta wameruka majivu na kukanyaga moto.

Inawezekana kabisa kujikuta ukiwa katika uhusiano usiokupa furaha lakini ni kwa jinsi gani unaweza kujizuia usikwame na kuzama katika mahusiano hayo na kukosa furaha katika maisha yako yote?

Unaweza pia kujiuliza inakuwaje wanawake wengi wazuri na walio makini hujikuta wakiangukia katika uhusiano usiowapa furaha na kinyume chake kujikuta wanaumia kila mara. Ni ukweli usiopingika kwamba kama umewekeza penzi, moyo na muda wako mwingi katika uhusiano mawazo ya kuachana na kuanza upya huwa yanatisha sana. Mtaalamu wa saikolojia za uhusiano Donna Dawson anasema wengi wetu wanajikuta wanaamua bora kukaa na shetani unayemjua kuliko yule usiye mjua, kwa hiyo wanaamua kuendelea kwa kuhofia wasije kuamua kuanza uhusiano mpya na kujikuta wameruka majivu na kukanyaga moto.

Sasa unajuaje kuwa uko katika kuzama kwa mpenzi asiyekufaa na unatakiwa kufanya nini ilikujisidia?

Acha sababu za visingizio

Kama mpenzi wako anafanya vitu vinavyokuumiza na kukusononesha na badala ya kuvielezea jinsi vilivyo wewe unapindisha ukweli na kujaribu kuvifunika kama vile anavyovifanya ni haki, nadhani inabidi ufike wakati ujitahidi kuwa mkweli, muwazi na halisi.

Kubali kabisa kuwa uhusiano wenu unayumba na unaonekana kutofanikiwa kabisa. Inawezekana kabisa na ni kitu cha kiasili kuangalia tu kila kilicho chema kutoka kwa mtu unayempenda lakini usiache hii ikupofushe kuuona ukweli uliodhahiri. Karibu kila uhusiano una nyakati za kupitia katika misukosuko ya aina fulani lakini kama unatumia muda wote katika kuchanganyikiwa na kuhofia nini mpenzi wako atakifanya, na kujaribu kumtetea tabia zake mnapokuwa na marafiki, ndugu au hata wewe mwenyewe unapojizuia kuuangalia ukweli wa maumivu na kujilazimisha kuona vile visivyo halisi, ili tu uendelee kumpenda. Hapa ni sawa sawa na kujizika kichwa chako mwenyewe katika mchanga.

Lazima uwe jasiri na kujiuliza je, mpenzi huyu anakupa furaha? Jaribu kuandika mazuri na mabaya yake yote kwenye karatasi ili uweze kupata picha nzuri ya nini utapoteza au nini utafaidika kwa kuondokana na uhusiano huo. Baada ya kupata hayo, kaa naye chini muongee ni kwa jinsi gani mnahitaji mabadiliko ili uhusiano wenu uweze kuwa na mustakabali mzuri. Kama yeye haoni tatizo kama ulionavyo wewe na labda hayuko tayari kufanya yale unayoona yataleta mabadiliko katika penzi lenu au yawezekana aliahidi kubadilika lakini haikuwa kama alivyo ahidi, huu unaweza kuwa wakati muafaka wa kuhitimisha mahusiano yenu.

Pigana na hofu zako

Kufahamu kuwa uko katika uhusiano mbovu na hatarishi ni kitu kimoja na jinsi ya kutoka ni kitu kingine. Lazima kwanza uhakikishe unakuwa halisi na pia lazima uwe jasiri kuwaambia wanaowazunguka kuwa uhusiano wenu umefikia mwisho.

Dawson anaongeza kwamba mara nyingine kuvunjika kwa uhusiano kwaweza kuwa kama tangazo kwa umma kuwa wewe ni kati ya wale wasioweza kukaa katika uhusiano, wala usihofie hili kwa sababu litakunyima ujasiri na kukufanya uzidi kupoteza muda kwa kuwa na uhusiano na mtu asiyeyafaa maisha yako.

Hakuna uhusiano ambao ni kamilifu lakini unahitaji mpenzi ambaye atayafaa maisha yako na anayekustahili kikweli. Jiulize, je mpenzi wako anakufanya ujihisi kuwa unahitajika, unasaidika, na unalindwa? Je, furaha bado ipo baina yenu? Mtaalam Dawson anasema kwamba siku zote inawezekana kumpata anayekufaa “lakini kwanza ni vyema kumjua asiyekufaa”.

Amini katika mazuri

Yawezekana uhusiano wako umefeli lakini kumbuka sio wewe uliye feli. Kubali kwamba waweza kuomboleza kwa ulichopoteza baada ya uhusiano wenu kuvunjika lakini pia fikiria yale mema uliyojitahidi kuyafanya ili muweze kuendelea na ikashindikana.

Kwa kukaa kwa muda mrefu katika uhusiano yasiyokupa furaha kunaweza kumong’onyoa ujasiri wote uliokuwanao katika kila eneo la maisha yako, fanya uamuzi mapema na ichukue hiyo kama nafasi ya kujifunza kuhusu wewe mwenyewe na pia kujifunza kutokana na makosa yako. Wakati utakapojifunza kuwa na furaha wewe binafsi utakuwa kama sumaku kuwavuta wengi kukupenda.

Mara nyingi kila mtu hujitahidi kuonyesha kila kilicho bora mwanzoni mwa uhusiano, kwahiyo wala huna haja ya kujilaumu kuwa kwa nini hukumjua vizuri tokea mwanzoni, badala yake amua kwamba kamwe hutozembea katika kuzitazama alama za maonyo tokea mapema. Jiulize ni aina gani ya uhusiano ulio nao, je, unatumia kila muda kutafuta kukubalika machoni kwa mpenzi wako mwenye kuhitaji mengi kutoka kwako? Au unavutiwa na maisha na roho ya huyo mpenzi wako wakati akisha kuumiza moyo hutoka na kwenda kuitafuta furaha sehemu nyingine?.

Wakati utakapogundua kile kilichokuumiza mwanzoni utajua ni nini unatakiwa kukiepuka na nini usijaribu kukifanya ili kuepusha shari baadae. Hii yote ni katika kuhakikisha unajipatia afya na heshima binafsi katika uwezo wako wa kufanya uamuzi. Mtaalam Dawson anadokeza kuwa ni lazima kufahamu kwanza kuwa unastahili kilicho chema kabla ya kuanza kukitafuta chema hicho.

Kama kuna kitu hakijakaa sawa katika uhusiano wako jitahidi sana kuwa muwazi, mkweli na halisia. Kumbuka kwamba kila dakika unayoipoteza na mpenzi asiyekufaa ni dakika ambayo ungeweza kuitumia ukiwa na mpenzi ambaye angeweza kukufanya mwenye furaha ya kweli.