Je watoto wote wanapata fursa sawa?

Muktasari:

Mjadala mkubwa umekuwa ukijikita katika namna ya kumsaidia mtoto wa kike kuendelea na elimu baada ya kujifungua pale apatapo ujauzito akiwa shuleni. Ingawa kumekuwa na pingamizi juu ya hili kutoka kwa watunga hata kwa baadhi ya wabunge wetu na kusababisha sintofahamu kwa watoto, wazazi, wadau wa haki za binadamu na maendeleo ya jamii. Hili halielezeki.

Ikiwa ni siku mbili tangu tuadhimishe siku ya mtoto wa Afrika, mzazi umejipangaje kuhakikisha unatekeleza dhamira ya watoto wako ya kuwapatia elimu bila ubaguzi? Makala yetu ya leo yatajikita katika kuangalia ni namna gani tunaenzi na kutekeleza lengo la watoto wa Afrika walioandamana kudai haki sawa katika utoaji wa elimu huko Soweto nchini Afrika kusini mnamo mwaka 1976 ambapo watoto takriban elfu 10,000 waliandamana kudai haki sawa katika elimu na kuitaka serikali kutoa elimu hiyo kwa lugha yao mama, katika maandamano haya watoto zaidi ya 100 walipoteza maisha kwa kupigwa risasi na polisi. Kutokana na tukio hili, mnamo mwaka 1991 nchi za umoja wa Afrika zilikubaliana siku ya tarehe 16 Juni kila mwaka iwe ni siku ya kuadhimisha siku ya mtoto wa Afrika.

Tukiangazia madai haya ya watoto, tujiulize. Je, tunawaenzi vipi kwa kuhakikisha tunawapatia elimu watoto wetu bila kujali changamoto wanazokumbana nazo. Changamoto tunazokumbana nazo kama mzazi, mwana jamii, wadau wa maendeleo, serikali na changamoto za kisera kwa ujumla. Kutokana na utafiti wa kitaifa juu ya vichocheo na madhara ya ndoa na mimba za utotoni uliofanywa na taasisi ya Utafiti wa Kidemografia na Afya Tanzania ya mwaka 2015-16, unaonyesha Utoaji wa elimu sawa kwa watoto umekuwa ukikumbwa na vikwazo vingi. Mojawapo ya vikwazo vikubwa hasa vilivyotajwa ni pamoja na mimba na ndoa za utotoni, umasikini pamoja na ubaguzi wa kijinsia. Utafiti huu unaonyesha kuwepo kwa ongezeko la mimba za utotoni katika maeneo mengi nchini hususani vijijini, na kwamba zaidi ya asilimia 27 ya wasichana wenye umri kati ya miaka 15-19 wamepata ujauzito. Kiwango hiki ni kikubwa ukilinganisha na ripoti ya mwaka 2010 ambapo iliripotiwa kuwepo asilimia 23.

Tafiti zingine zimeonesha kuwa asilimia 32 ya wasichana waliopo vijijini wameathirika na mimba za utotoni wakati waliopo mijini ni asilimia 19. Tafiti zimeutaja Mkoa wa Katavi kuongoza kwa mimba za utotoni kwa asilimia 45, Tabora asilimia 43, Dodoma na Morogoro asilimia 39, Mara asilimia 37 na Mbeya asilimia 32. Bado ile dhana ya kuwa mtoto wa kike hana haja ya kupata elimu bali kuolewa na kuwa msaidizi wa kazi za nyumbani bado ati ina mashiko! Kutokana na changamoto hizi kumeibua mijadala mikali baina ya watunga sera, jamii na wadau wa maendeleo juu ya nini kifanyike ili kuhakikisha watoto wanaipata elimu kwa usawa huku baadhi wakijaribu kutoa ufumbuzi wa namna gani watoto hawa wapate fursa ya elimu bila kujali changamoto wakati wengine wakipingana na mawazo hayo.

Mjadala mkubwa umekuwa ukijikita katika namna ya kumsaidia mtoto wa kike kuendelea na elimu baada ya kujifungua pale apatapo ujauzito akiwa shuleni. Ingawa kumekuwa na pingamizi juu ya hili kutoka kwa watunga hata kwa baadhi ya wabunge wetu na kusababisha sintofahamu kwa watoto, wazazi, wadau wa haki za binadamu na maendeleo ya jamii. Hili halielezeki.

Kutokana na changamoto zote hizi, tungependa kutoa wito hasa kwa wazazi wasikubali changamoto hizi zimkwamishe mwanao kupata elimu, weka mipango na malengo madhubuti juu ya ustawi wa mtoto wako, wahenga husema kuteleza si kuangua. Upo ushahidi wa kutosha wa wanawake na wasichana waliofanikiwa kielimu na kimaisha walipoamua kurudi shule baada ya kupata ujauzito. Wengine wapo vyuo vikuu wanaendelea na masomo hawakukata tamaa. Hivyo mzazi usiangalie mwanao alipoanguka bali alipojikwaa na ondoa kihunzi mtoto aendelee na shule kwa mustakabali wa maisha yake ya baadaye.

Tunapokuwa na taifa lenye wanawake wengi wasio na elimu tunatumbukia katika shimo la umaskini na itakuwa vigumu kufikia Tanzania yenye uchumi wa kati. Yaani wanawake wasio na uelewa ndio wanaoenda kulea familia zetu,