Jifunze jinsi ya kuepuka madhara ya kuahirisha kutekeleza mambo yako

Muktasari:

Aliendelea kusema “Zamani nilikuwa naogopa sana kufanya uamuzi na mara nyingi nilikwepa kufanya shughuli zangu hasa zile zisizovutia na nilizoziona ni ngumu. Hususan, nilikuwa naahirisha yale mambo niliyoyafikiria sio ya haraka na wala hayaniwajibishi. Lakini kuna rafiki yangu mmoja aliyenitahadharisha kuhusu madhara ya tabia hiyo na kunihimiza kutekeleza kila jambo linalonikabili bila kupoteza wakati.

Siku moja niliona katika ofisi ya mfanyabiashara maarufu ameweka maneno yanayosema “Usingojee kesho kwani huwa haifiki” Nilipomuuliza sababu ya kuweka maneno hayo akasema yanamtahadharisha asiwe na tabia ya kuahirisha kutekeleza mambo kwa kusema atafanya kesho. Alisisitiza kuwa tabia hiyo ilimchelewesha sana kupata maendeleo.

Aliendelea kusema “Zamani nilikuwa naogopa sana kufanya uamuzi na mara nyingi nilikwepa kufanya shughuli zangu hasa zile zisizovutia na nilizoziona ni ngumu. Hususan, nilikuwa naahirisha yale mambo niliyoyafikiria sio ya haraka na wala hayaniwajibishi. Lakini kuna rafiki yangu mmoja aliyenitahadharisha kuhusu madhara ya tabia hiyo na kunihimiza kutekeleza kila jambo linalonikabili bila kupoteza wakati.

Je wewe ni mmoja kati ya watu wenye tabia kama hii? Je umewahi kujuta kuwa kuna baadhi ya mambo ulichelewa kuyatekeleza yakakuletea shida katika maisha yako? Tabia hii huambatana na uvivu. Je kama una tatizo hili umewahi kufikiria jinsi unavyoweza kuachana na tabia hii au umeichukulia kama ni kitu ambacho huwezi kuachana nacho. Tabia hii sio kilema wala ugonjwa usioweza kutibika. Ni hulka ambayo kila mtu hana budi kuikomesha ili isiathiri maisha yake. Kwa hakika watu wenye maendeleo katika maisha ni wale ambao hawana tabia ya kuahirisha utekelezaji wa mambo yanayowabidi kuyatekeleza.

Kwa kuwa tabia hii ni adui wa maisha soma mbinu zifuatazo zinazoweza kukusaidia kuiepuka.

•Epuka kufikiria kuwa tabia ya kuahirisha haina madhara

Wafanyabiashara wengi hukwama kwa huahirisha kufanya maamuzi muhimu. Baadhi ya ndoa huathirika kutokana na tabia ya mume au mke kuahirisha utekelezaji wa mambo muhimu kwa maisha yao. Kuna watu ambao hata huweza kupoteza maisha kwa kufanya ajizi na kuahirisha kila mara kwenda kumuona daktari. Kuahirisha sio tu ni tabia mbaya bali ni adui anayeweza kuathiri shauku na ndoto zako za maisha na hata kukufanya ukakosa mwelekeo katika maisha yako.

•Tambua aina ya mambo ambayo umezoea kuyaahirisha zaidi

Kuna rafiki yangu meneja ambaye anaogopa sana vikao vya wafanyakazi wote, hivyo huwa anaviahirisha kila inapotokea haja ya kuvifanya. Matokeo yake yakawa mabaya sana hadi ikafikia hatua ya wafanyakazi kumfungia mlango wa ofisi yake asiingie kazini.

Hili ndilo lililokuwa eneo lake sugu zaidi kwa tabia yake ya kuahirisha. Kama wewe utatambua eneo ambalo umezoea sana kuahirisha utekelezaji na ukaweza kuishinda tabia hiyo katika eneo hilo, utaweza taratibu kuvuka katika maeneo mengine hadi ukahakikisha umeachana kabisa na tabia hiyo.

•Weka kipaumbele kwa kila jambo na wakati na muda wa utekelezaji wake

Mtu ambaye anajikuta amerundika mambo mengi ambayo hayajayatekeleza hulazimika kupoteza wakati mwingi kwa kujiuliza aanze kushughulikia mambo yapi katika rundo la mambo yanayomlazimu kuyashughulikia. Kama ilivyo kwa mwanafunzi ambaye amejilimbikizia mazoezi mengi yakufanya anaweza kugundua amechanganyikiwa. Wala asijue la kufanya mwisho huamua kutazama televisheni au kutoka nje akacheza michezo anayopenda badala ya kushughulikia zoezi moja baada ya jingine.

Kumbuka hakuna shughuli mbili tofauti ambazo zinazofanana kwa umuhimu wake. Mambo ambayo mtu ameyalimbikiza kutokana na tabia ya kuahirisha anaweza kujikuta pengine anaanza kushughulikia yale yasiyo na umuhimu zaidi na kuacha yale yaliyo muhimu zaidi. Jambo baya zaidi anaweza kusahau mengine muhimu mpaka siku yatakapozua changamoto kubwa. Hapa kuna njia unayoweza kutumia ili kuweka vipaumbele.

Tunza kujitabu cha shujara ya kila siku ambacho pia huitwa ‘diary’ Kila siku jioni andika orodha ya mambo unayopanga kufanya siku inayofuata. Yapange kufuatana na vipaumbele vyake, ukianzia na lile lililo muhimu sana hadi lile ambalo umuhimu wake ni nafuu kidogo. Siku inapoanza uanze kutekeleza mambo uliyopanga. Jioni tazama orodha yako na anza kuandaa ukurasa wa siku inayofuata. Kwanza andika yale ambayo hukufanikiwa kuyatekeleza. Kisha ongezea yale mapya unayokusudia kuyatekeleza siku inayofuta. Endelea kufanya hivyo siku hadi siku. Jambo linalohamishwa siku siku tatu mfululizo, anza kuliandika kwa wino mwekundu kama ishara kuwa limechelewa kutekelezwa.

Unapoiongoza akili yako kufuatilia utaratibu huu kwa umakini na nidhamu ya kutosha utagundua kuwa ni mchakato utakaokusukuma usifanye tabia ya kuahirisha mambo.

•Jiwekee wewe mwenyewe muda wa mwisho wa kukamilisha kila jambo

Kujiwekea muda wa kukamilisha utekeleza wa kila jambo unalolikusudia kulifanya ni wa kitaalamu na kutumiwa na watu wote walio makini katika maisha yao. Pamoja na kuyaorodhesha mambo unayokusudia kuyatekeleza pia kumbuka kukadiria na kujiwekea muda utakaotumia kwa kufanya na kukamilisha kila jambo.

Kila unapojiwekea muda wa kukamilisha kila jambo jitahidi kwa namna moja au nyingine uweke mashahidi watakaotambua muda uliojipangia. Kwa mfano kama ni shughuli ambayo mara unapoimaliza unatakiwa uiwasilishe kwa mtu fulani, basi mfanye awe shahidi kwa kumtangazia siku utakapoiwasilisha kwake. Kwa kuweka mashahidi hautaweza kuahirisha jambo ulilopanga kulitekeleza na wala hutachelewa kulikamilisha katika wakati uliojipangia.

• Usikwepe shughuli zilizo ngumu

Kuahirisha jambo fulani kwa kuwa utekeleza wake ni mgumu hakutakusaidia bali hatimaye huenda hutakusababishia tatizo kubwa.

Nakumbuka nilipokuwa nikifanyakazi katika ofisi kubwa kila nilipogundua kuwa kuna lundo kubwa la barua ambazo nilikuwa nalazimika kuzishughulikia nilikuwa naziweka kando. Siku moja mtaalam wa saikolojia alinionya nisifanye hivyo huku akiniasa kuwa ni vyema nikabiliane na ugumu wa suala hilo. Alinifahamisha kuwa juhudi ninazozitumia katika masuala mepesi daima inanipatia lifti ya kukabiliana na mambo yasiyo mepesi.

• Epuka kuacha kutekeleza kwa hofu kuwa hataweza kufanya vizuri.

Watu wengi huwa wanaahirisha kufanya jambo fulani kwa hofu kuwa hawataweza kulifanya vizuri. Hii isiwe sababu tekeleza jambo hata kama sio vizuri zaidi mradi tu usiliahirishe likabaki halijatekelezwa.

Kwa hakika kadri tutakavyomudu kuepuka tabia ya kuhairisha kutekeleza mambo katika maisha yetu ndivyo kadri tutakavyofanikiwa kuwa na maendeleo makubwa.