Ifahamu hedhi ya kawaida kwa wanawake wengi

Muktasari:

Makala hizo zimegusa wanawake na kuzua maswali mbalimbali niliyoulizwa kwa ujumbe mfupi wa maneno, hivyo nimeona leo niwape dondoo muhimu juu ya mzunguko wa kawaida wa hedhi.

Kwenye makala zilizopita tuliona mambo yanayochangia uwezekano wa nafasi ya kupata mtoto wa kiume na kufunga mfululizo wake kuhusu mada hiyo.

Makala hizo zimegusa wanawake na kuzua maswali mbalimbali niliyoulizwa kwa ujumbe mfupi wa maneno, hivyo nimeona leo niwape dondoo muhimu juu ya mzunguko wa kawaida wa hedhi.

Kupata ufahamu wa jambo hili angalau kutasaidia kubaini mambo yanapokwenda mrama katika mzunguko wa kila mwezi kwa wanawake wengi.

Mzunguko wa hedhi unahusisha matukio mbalimbali yanayoleta mabadiliko mbalimbali mwilini mwa mwanamke, lengo likiwa kuiandaa nyumba ya uzazi kutoa hifadhi iwapo mimba itatungwa.

Hedhi hutokea baada ya mimba kutotungwa hivyo utando mwororo maalumu ulio tayari kutoa mazingira ya kujipachika kwa yai lililotungishwa kupiga hatua za ukuaji, hujinyofoa na kutolewa nje ya nyumba ya uzazi na yai ambalo halikukutana na mbegu ya kiume.

Mzunguko wa hedhi huhesabiwa siku ya kwanza damu inapoanza kutoka na kwa mwezi huo mpaka mwezi mwingine, itakapojirudia tena.

Damu na taka nyingine hutoka kupitia uwazi mdogo wa mlango wa nyumba ya uzazi, hutolewa nje kupitia mfereji wa uke.

Mzunguko huu huwa na hatua kuu tatu yaani ya kuvuja kwa damu (menstruation), urutubishwaji wa yai na utolewaji wa yai lililokomaa na kipindi cha maandalizi ya mzunguko mpya wa hedhi.

Mzunguko huu unahusisha mfululizo wa matukio ya mabadiliko katika mwili wa mwanamke. Vichochezi ndiyo vinavyodhibiti mzunguko huu, wakati wa mzunguko tezi mbili za kichwani zinazopeleka na kurudisha mrejesho katika via vya uzazi (ovary).

Taarifa hizo ni kuziweka tayari kokwa za uzazi na mji wa mimba kupokea mimba itakayotungwa. Homoni inayoitwa estrogen na progestrone ndiyo hufanya kazi ya mabadiliko mbalimbali katika mji wa mimba.

Ni wanawake waliovunja ungo pekee ndiyo wanaopata mzunguko wa hedhi. Kwa kawaida wanawake wengi hufanya hivyo kuanzia umri wa miaka 11 mpaka 15.

Kwa kawaida wanawake wengi duniani mizunguko yao ya hedhi huwa iko tofauti, ingawa wote hupata hedhi yao kati ya siku 21 mpaka 35, wastani ukiwa ni siku 28.

Kwa maneno mengine naweza kusema, hedhi hutokea mara moja kwa mwezi. Kwa kawaida damu inayokadiriwa kiasi cha sentimita za ujazo 100 hadi 150 hutoka kwa siku tatu mpaka tano mfululizo.

Kwa kawaida mwanamke hutakiwa kubadili pedi au taulo za kike mara mbili mpaka tatu kwa siku, huku ikiwa imenyonya damu yote kabla haijalowa chapachapa. Rangi ya damu inayotoka inatakiwa kuwa nyeusi au nyekundu iliyo na giza.

Damu hiyo haitakiwi kuwa na harufu kali ya kukera wala haitakiwi kuwa imeganda na kukakamaa. Maumivu ya chini ya tumbo yanatakiwa kuwa ya kawaida, yawe ya kuvumilika na yaishe hedhi inapokoma kumwagika hasa siku ya kwanza ilipoanza.

Hii ndiyo hedhi ya kawaida, iwapo kutakuwa na mabadaliko nje ya haya niliyoeleza tunakutana na mzunguko wa hedhi usiyo wa kawaida, yaani wenye hitilafu ambayo huenda ni tatizo la afya linalohitaji ushauri na matibabu.

Wiki ijayo tutaona mambo mbalimbali yanayosababisha kubadilika kwa mzunguko wa hedhi.