SIMULIZI ZA MUZIKI: Jimi Hendrix, Whitney, Chris Kelly ni kielelezo cha ubaya wa dawa za kulevya

Muktasari:

  • Janis Joplin alikuwa binti mdogo wa miaka 27 tu alipofariki.

Ukiangalia kwa juu juu kuna raha sana  kuwa mwanamuziki maarufu. Ni ndoto ya vijana wengi kwani huonekana ni kujiondoa katika maisha ya dhiki na kuanza kuishi  yaliyojaa furaha za kuwa na nyumba nzuri, magari ya kifahari na kusafiri nchi mbalimbali kwa ndege.

Hiyo ndio picha inayotengenezwa kuhusu wasanii maarufu, lakini nyuma ya hadithi hii kuna vijana kujikuta wameingia katika makucha ya matumizi ya dawa za kulevya.

Vijana hudanganywa kuwa dawa hizo zina uwezo wa kuongeza ubora wao katika usanii na kuongeza raha katika maisha yao.

Wengi huishia kuingia kwenye matumizi ya dawa za kulevya bila kutimiza hata asilimia moja ya ndoto zao na kuishia kuwa mzigo kwa familia na jamii inayowazunguka.

Historia inaonyesha mlolongo mrefu wa wasanii maarufu duniani ambao waliishia kupoteza maisha yao kutokana na matumizi ya dawa za kulevya.

Leo tuangalie baadhi ya wanamuziki maarufu duniani ambao walipoteza maisha yao kutokana na matumizi ya dawa za kulevya

Janis Joplin alikuwa binti mdogo wa miaka 27 tu alipofariki. Kifo chake katika umri huo kilimfanya kuingia katika kundi la wanamuziki maarufu waliofariki wakiwa na umri wa miaka 27.

Kundi hili lilikuwa na wanamuziki wengine kama Jimi Hendrix mpiga gitaa maarufu, Brian Jones mpiga drums na Amy Winehouse mwimbaji.

Jimi Hendrix aliyefariki Septemba 18, 1970, mpaka leo wapiga magitaa huendelea kumsifu. Alifia katika hoteli baada ya kuanza kutapika kutokana na dawa alizokunywa, ambazo alizishushia na mvinyo. Kwa kuwa alikuwa peke yake matapishi yake ndio yakamziba pumzi akapoteza maisha.

Chris Kelly aliyetamba na kundi la  Kris Kross ni mwathirika mwingine wa dawa za kulevya. Mama yake alieleza baadae kuwa usiku kabla hajalala mwanae alitumia dawa zakulevya mchanganyiko. Asubuhi ya Mei 1, 2013 alikutwa amekufa. Vipimo vilidhihirisha kuwa kifo chake kilitokana na dawa hizo.

Asubuhi ya  Februari 11, 2012 habari za kusikitisha za kifo cha Whitney Houston, mwanamke mwenye sura na sauti nzuri zilianza kuenea duniani.

Whitney alikutwa amezama kwenye maji ya kuoga bafuni kwake. Inaonekana alikuwa anaoga kujitayarisha kuhudhuria sherehe za tuzo za Grammy, kabla ya hapo  alitumia mchanganyiko wa dawa za kulevya akapitiwa na uzingizi akiwa ndani ya ‘bathtub’. Whitney alifariki akiwa na umri wa miaka 48.

Kifo cha  Michael Jackson  Juni 25, 2009 kiliuingiza ulimwengu mzima katika majonzi. Michael alipatwa na matatizo ya moyo kutokana na mchanganyiko wa madawa aliyokuwa akipewa ambayo yalikuwa yamemtawala kiasi cha kutoweza kupata usingizi kama asingetumia. Michael alifariki akiwa na miaka 50. 

Novemba 13 , 2004, siku mbili kabla ya kusherehekea mwaka wake wa 36 toka kuzaliwa, Russel Tyrone maarufu kwa jina la ODB na  mwanzilishi wa kundi la Rap la Wu Tang, akiwa anarekodi kazi yake alianza kulalamika kuwa ana maumivu makali kifuani baada muda mfupi akazimia na hatimae kufariki.

 Vipimo baadae vilionyesha kuwa alikuwa ametumia dawa za kulevya mchanganyiko.

Wapenzi wa muziki wa miaka ya 1970 na 1980 wanalikumbuka kundi lililotikisha dunia la Temptations ambalo Lionel Ritchie alitokea.

Katika kundi hili kulikuwa na muimbaji aliyeitwa David Ruffin. Sauti yake ilisikika katika nyimbo maarufu kama My Girl na Ain’t Too Proud to Beg.

Naye bahati mbaya ni mmoja ya wanamuziki waliopoteza maisha yao kutokana na dawa za kulevya. Alihangaika kujaribu kuachana na dawa hizo lakini hatimae tarehe  Juni 1, 1991 mauti yalimkuta na uchunguzi ulionyesha kuwa kifo chake kilikuwa matokeo ya dawa za kulevya.

Unaweza kutumia karatasi nyingi kuandika kuhusu madhara mbalimbali ambayo dawa za kulevya zimewaletea wasanii maarufu. Wengine wamefilisika, wameharibika akili, kujiua, lakini jambo moja tu lina ukweli kuwa dawa za kulevya hudanganya akili na kumuingiza mtu katika utumwa wa kuzitegemea na hivyo maisha kuanza kuendeshwa na dawa hizo.

Wasanii tujue wazi sanaa bila dawa za kulevya inawezekana