Jinsi ya kufanya ili mtoto apende chakula

Muktasari:

  • Shosho anashauri kwamba wakati wa kumlisha mtoto ni vyema mzazi au mlezi utumie lugha ya upole na upendo ili kumuhamasisha mtoto kula. Lugha za matusi, vitisho na ukali humfanya mtoto achukie na akatae kula chakula.

Wazazi wengi hasa waishio mijini wanakumbana na changamoto ya watoto wao kutopenda kula ama kwa kukosa hamu na hata vinginevyo. Tumepata wasaa wa kuzungumza na mtaalamu wa lishe kutoka Shirika la Chakula Dunia (WFP), Neema Shosho na hapa tutakupa machache juu ya nini ufanye mwanao apende kula.

Shosho anashauri kwamba wakati wa kumlisha mtoto ni vyema mzazi au mlezi utumie lugha ya upole na upendo ili kumuhamasisha mtoto kula. Lugha za matusi, vitisho na ukali humfanya mtoto achukie na akatae kula chakula.

Kwamba ili mtoto apende kula, pendelea kumpa chakula chake kipindi ambacho familia pia inakula. Hii itamuhamasisha kula zaidi. Asile peke yake mara zote. Hata hivyo kumlisha mtoto kunahitaji uvumilivu. Tenga muda wa kutosha wa kumlisha mtoto wako. Ongea nae, zunguka nae na cheza nae huku ukimbembeleza kula kwa upole na upendo

Kamwe usijaribu kumkaba mtoto ili ale chakula. Hii inaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo chakula kupita njia ya hewa jambo linaloweza kugharimu uhai wake. Vilevile kumkaba koo kunaleta madhara ya kisaikolojia wakati mtoto ataona kula ni adhabu na kuchukia chakula.

Jaribu kumpa mtoto vyakula vya aina mbalimbali ili ujue anapenda vyakula gani. Kwa watoto wakubwa kidogo mfano miaka mitatu na kuendelea ni muhimu kumshirikisha mtoto katika uandaaji wa chakula. Muulize angependa kula nini? Zungumza naye kama inawezekana kuandaa anachotaka mwambie na kama haiwezekani ajue kwa nini. Usimkaripie. Unampotezea uwezo wa kujiamini na ujenzi wa hoja. Nenda na watoto wako eneo unalonunulia chakula (gengeni, sokoni, supermarket, dukani, gulioni) na uwasikilize nini wanapendelea kula. Kumbuka mnaweza kufanya machaguo sahihi ya vyakula kwa bei nafuu kabisa.

Wewe mzazi au mlezi uwe kioo kwa mtoto wako kwa kula mlo kamili na wa bora. Mzazi ukila mlo kamili na wa bora ni rahisi mtoto kuiga na kupenda mlo wake. Vilevile jitahidi vyombo unavyotumia kumlishia mtoto viwe vinavutia. Usiweke chakula kwenye bakuli lililoharibika mfano lililoungua, lenye ufa, lililopondeka na kadhalika. Nunua vyombo vya watoto vizuri, vyenye kuvutia na vya bei nafuu kabisa ili kumuhamasisha mtoto kula.

Watoto wakubwa waruhusiwe kuingia jikoni chini ya uangalizi wa mzazi au mlezi. Waonyeshe unavyoandaa chakula na washirikishe msaidiane kuandaa mlo kamili na ulio bora. Kumbuka kula mlo bora na kamili sio lazima uwe na pesa nyingi. Pangilia pesa uliyonayo na hakikisha unanunua vyakula bora, kamili na asili vinayopatikana kwenye eneo lako unaloishi