Jinsi ya kumgundua mpenzi tapeli-2

Muktasari:

  • Leo hii ninaendelea kuelezea tabia nyingine kwamba mara nyingi hawajiachii sana kihisia na kuzama kimapenzi, lugha ya mtaani wanasema “hawataki kuonekana wako deep” kilakitu wanakifanya kirahisi tu, hakuna kumaanisha sana katika mambo yao.

Wiki iliyopita nilizungumzia tabia ya kwanza ya mwanamume msanii ambayo ni kutopenda kupokea zawadi au kujifanya hapendi kabisa mambo hayo.

Leo hii ninaendelea kuelezea tabia nyingine kwamba mara nyingi hawajiachii sana kihisia na kuzama kimapenzi, lugha ya mtaani wanasema “hawataki kuonekana wako deep” kilakitu wanakifanya kirahisi tu, hakuna kumaanisha sana katika mambo yao.

Kama bado hajaoa basi hata siku moja hutosikia akiongelea maisha yenu ya mbeleni kama vile mambo ya watoto na maendeleo mengine, yeye ni kula raha na wewe tu hakuna kingine.

Nimeletewa malalamiko tele kwamba mpenzi wa kiume kila siku anaahidi kumpeleka mpenzi wake kwa ndugu zake lakini hiyo siku haifiki, hata pale anapoambiwa basi haya twende ukawaone ndugu za mwanamke, yeye hujaribu kupoteza lengo, hapo ujue anaogopa kujizamisha katika maji asiyoweza kuyaogelea

Kama mpenzi uliye naye ni mwenye ndoa tayari basi fahamu na ikuingie akilini kuwa kamwe hatomuacha mke wake aliyenaye eti akuoe wewe hata kama amewahi kukuahidi hilo. Fahamu tu huyo ni msanii wa kawaida na anatafuta tu “good time” na wewe na wala siyo mapenzi.

Tabia ya tatu

Mara nyingi hatopenda mkutane sehemu zenye watu wengi. Wewe fikiria tu pale anapopapendekeza mkutane, utakuta ni hotelini tena siyo nje bali chumbani au eneo la kujifichaficha. Pamoja na kukuonyesha kuwa anakupenda kuliko yoyote aliyenae lakini hawezi kuruhusu watu wajue kuwa anakupenda.

Najua kisaikolojia wanawake hupenda mwanaume aonyeshe upendo wake mbele ya watu kwa mfano; kumbusu, kumshika mkono, kumkumbatia, kumfungulia mlango wa gari au kummiminia kinywaji katika glasi. Pole sana kwa maana kama una mpenzi wa tabia hii ya tatu basi hizi raha utazisikia tu kwa wenzako. Kamwe hutozipata kwa maana anaepusha sana mazingira ya jamii au marafiki zake kugundua uhusiano na kuogopa taarifa zaweza kumfikia mamsap wake aliye rasmi. Usivumilie tu hali hii unapoteza vingi, kumbuka mwenye macho haambiwi tazama.

Tabia ya nne

Ni wataalamu na watu wakujua kuzifuata kanuni za kuficha ukweli, watakupa mida maalumu ya kuwapigia simu, wakijitetea kuwa wana mikutano mida fulani au wengine wanakuwa wazi kukwambia usimpigie ikifika muda fulani maana atakuwa nyumbani maana mkewe anaweza kushituka na akalidhuru penzi la nje. Wengine ilikukata mizizi ya fitina kuna mida fulani hata uwatafute kwa tatizo gani kamwe hutompata hewani, simu zao zinazimwa hasa mida ya jioni au usiku wanapokuwa majumbani kwao.

Tahadhari, kama una mpenzi ambaye ana tabia ya kuzima simu mara kwa mara, au katika mida fulani, au kuiweka katika hali ya kuondoa sauti “silent mode” hiyo ni dalili au ishara ya taa nyekundu, unahitaji kufumbua macho zaidi.

Wapo wanawake ambao hawajawahi kusikia simu yoyote ikipigwa na mwanamke kwa waume zao wakiwa nyumbani, simu zote ni marafiki zake na wafanyakazi wenzake, usifurahie sana hali hiyo, yawezekana wako wengi wanaopiga simu hizo mida ya mchana na jioni wanaambiwa wasitishe mawasiliano.

Wengine hutoa taarifa ya kuingia kwenye mkutano au darasani ili usimtafute mida fulani lakini siyo wote ambao wanakuwa huko wanakodai au kufanya kile wanachosema.

Tabia ya tano

Tabia nyingine wanayoizingatia sana ni kwamba daima hujiepusha kuweka chochote katika maandishi, watasemama kila kitu kwa mdomo ana kwa ana au hata kwenye simu lakini siyo kutuma meseji au kuandika barua pepe au ya kawaida. Wako wakina dada ambao wanajisifia kuwa wapenzi wao wanawapigia tu simu hawajawahi kutuma meseji hata siku moja, usidhani ana hela sana? hapana! Anafuata kanuni inayosema “never put anything in writing”. We we ni shahidi wengi wamekamatwa na kugundulika kupitia ujumbe wa maandishi katika simu.

Simu zimekuwa tatizo kubwa katika uhusiano wa watu kwa sababu ya vinavyoandikwa ndani zaidi ya vile vinavyosemwa.

Ni hamu yangu kubwa kama mshauri kukusaidia wewe usiingie katika dimbwi la machozi na kujuta, na mwisho kuipoteza kabisa dira ya maisha yako. Leo yaweza kuwa ni siku ya kufanya uamuzi wa mabadiliko.