Juma Mpongo;Alisugua benchi Yanga,sasa tegemeo la KCB FC

Muktasari:

  • Mafanikio yanayo tafutwa ni kucheza ligi kubwa kwenye nchi mbalimbali zilizoendelea, kwenye harakati za utafutaji wa mafanikio hayo wapo ambao tayari wamefika mbali kama Mbwana Samatta ukilinganisha na wanao mfuata nyuma.

 Inawezekana kwa siku za usoni kikosi cha Taifa Stars kikaundwa na wachezaji wengi kutoka nje,maana kadri siku zinavyosogea kumekuwa na wimbi kubwa la wachezaji wa Kitanzania ambao wanasaka mafanikio ya soka nje ya nchi.

Mafanikio yanayo tafutwa ni kucheza ligi kubwa kwenye nchi mbalimbali zilizoendelea, kwenye harakati za utafutaji wa mafanikio hayo wapo ambao tayari wamefika mbali kama Mbwana Samatta ukilinganisha na wanao mfuata nyuma.

Kazi ya Spoti Mikiki ni kuwaibua nyota wa Kitanzania ambao wapo nje ya nchi kwenye utafutaji wa mafanikio ya soka, nyota hao wapo ambao shauku yao ni siku moja kuja kulitumikia Taifa lao kupitia vipaji ambavyo Mungu amewapa.

Katika mfululizo wa Makala zetu za wachezaji hao, tuliona wiki iliyopita namna ambavyo safari ya winga wa Kitanzania, Hamad Mbumba wa Stima FC alivyopigania nafasi ya kucheza Ligi Kuu Kenya. Stima iko Daraja la Kwanza.

Leo tunaye kipa wa KCB FC, Juma Mpongo (31) ambaye naye anacheza Ligi Daraja la Kwanza Kenya, kipa huyo mzoefu amewataka wachezaji wenzake kuitumia vizuri nafasi ya kuichezea timu ya Taifa.

“Sio kila mchezaji anaweza kucheza timu ya Taifa na hakuna asiyependa kucheza timu ya Taifa lake labla awe na mambo yake mengine, inatakiwa kwa kila anayebahatika kupata hiyo nafasi kuonyesha kweli na sio kuvimbia hiyo nafasi.

“Bado nina uwezo wa kucheza timu ya Taifa, inawezekana kwa sababu msimu ujao tunaweza kuanza kucheza Ligi Kuu, tupo nafasi ya tatu na upishano wetu wa alama ni mdogo na ambao wametutangulia mbele.

“Michezo imebaki mitatu na mfumo wetu wa timu zitakazofuzu huwa ni mbili moja kwa moja alafu itakayoshika nafasi ya tatu itacheza mchujo na ile ambayo iliteleza kwa bahati mbaya kuwa kwenye hatari ya kushuka, mshindi wa hapo hupanda,” anasema.

Mpongo amewahi kuichezea Yanga na timu nyingine kibao za hapa Tanzania kabla ya kwenda kucheza kwenye ligi za mataifa mengine jirani kama vile DR Congo na Rwanda.

“Timu yangu ya kwanza kuicheza Ligi Kuu Tamzania Bara ilikwa Tanzania Prisons mwaka 2002, nikicheza hapo kwa msimu mmoja na kujiunga na Twiga Sports ya Kinondoni ambayo ilikuwa kama daraja kwangu la kujiunga na Yanga, 2004.

“Yanga sikukaa sana, niliondoka baada ya msimu mmoja kuisha na kwenda DR Congo kujiunga na DC Virunga ambayo ilikuwa ligi kuu, kuna mambo hayakuwa sawa Congo hivyo 2009, nilirejea Bongo na kujiunga na Moro United.

“2010 nilipata ofa ya kujiunga na S.C. Kiyovu Sports ya Rwanda, niliichangamkia ofa hiyo na kuona huo ni mwendelezo wa kuendelea kucheza soka la Kimataifa,” anasema kipa huyo.

Msimu uliofuata wa 2011/2012 mpongo amesema kutoka na uwezo aliouonyesha kwenye ligi alizivutia timu kadhaa na hatimaye akasajiliwa na Rayon Sports F.C.

“Mkataba wangu ulivyomalizika nikarudi Tanzania kuzichezea Coastal Union ya Tanga na Ashanti United ya Dar es Salaam kisha nikatimkia zangu Uarabuni ambapo na kwenyewe nilicheza kwa msimu mmoja na nikasajiliwa na hii timu ambayo naichezea mpaka sasa Kenya, “ anasema.

Akizungumzia ugumu wa ligi ambazo amezichezea, Mpongo amesema ni mdogo ila ligi ya Congo itabaki kuwa ligi yake bora kutokana na ushindani uliopo kwenye ligi hiyo.

“Mmmh!! Wakongo wametuacha mbali, ligi yao ni bora zaidi ndiyo maana hata kwenye mashindano ya Kimataifa yani klabu bingwa na shirikisho wamekuwa wakitoa timu nyingi kushiriki.

“Ukiondoa hiyo ligi naona Kenya, Rwanda na Tanzania zina viwango ambavyo havipishani sana, kuanzia uwezo wa wachezaji binafsi na hata namna ambvyo timu zinavyocheza.

“Kwa upande wa hamasa nje ya uwanja, Tanzania ni namba moja kwa ligi za Afrika Mashariki,ila kiuwezo wa ushindani inaweza kuwa ya pili mbele ya Kenya kisha Rwanda naweza kuiweka nyuma yetu ,” amesema

Mpongo alimalizia kwa kuwataka wachezaji wa Kitanzania kutokuwa na uoga wa kwenda kufanya majaribio nje ya nchi kwa sababu mpira unaochezwa ni ule ule kinachobadilika huwa ni falsafa za uchezaji kwa nchi husika.

“Kuna Mataifa yana utamaduni wa kupenda kucheza soka la kasi, hivyo kama mchezaji unatakiwa kujua mapema na kujiandaa na soka lao, utakapoenda kufanya majaribio usishindwe,” anasema.