KILIMO BIASHARA: Tajirika na kilimo cha papai

Muktasari:

ZINGATIA

Uzoefu wangu unaonyesha kama unataka kutajirika na kilimo, wekeza ipasavyo kwenye mazao ya mbogamboga, matunda na viungo.
Sisemi kama mazao mengine kama nafaka hayana soko, lakini mazao niliyotaja hapo juu, kwa kawaida huchukua muda mfupi kuvuna, hivyo kumwezesha mkulima kuona faida kwa haraka. Nitoe wito kwa Watanzania wenzangu kuhusu kilimo hiki, kwani kwa hakika kinalipa kama utadhamiria, kuwa na nidhamu na kuheshimu kilimo kama sehemu ya maisha yako.

Karibu katika safu mpya ijulikanayo kwa jina la ‘Kilimo biashara’.

Hii itakuwa safu maalumu kwa ajili ya kuonyesha namna mkulima anavyoweza kulima kwa mtazamo wa kibishara badala ya kilimo cha mazoea au cha kuhemea tumbo.

Pamoja na mambo mengine ya kuhusu kilimo, safu hii itakuwa ikitoa undani wa mazao kwa maana namna ya kulima zao husika, menejimenti ya zao hilo, masoko na pia mahesabu kuhusu faida unazoweza kupata kwa zao husika hasa ikiwa utafuata kanuni za kilimo ambacho wengi hawajui kuwa kuna sayansi ndani yake.

Kwa utangulizi wa safu hii, leo tutaangazia kilimo cha papai, kwa kuwa ni miongoni mwa mazao yenye fursa kubwa ya kifedha kwa mtu atakayeamua kulima kitaalamu na kwa kufuata ushauri wa wataalamu.

Kwa kukosa elimu kuhusu umuhimu wa papai kwa afya zetu na maendeleo ya uchumi wa mtu mmojammoja na hata Taifa, zao hilo halipewi uzito kama ilivyo matunda mengine yanayokimbiliwa na wakulima wengi kama maembe, machungwa, matikiti na mengineyo.

Kimsingi, zao la papai lina uwezo mkubwa wa kubadili maisha ya Mtanzania wa chini kabisa na kufikia hatua ya  milionea.

Papai ni tunda la kitropiki, hivyo maeneo mengi ya Tanzania hili zao linastawi na kufanya vizuri hasa ukilima kitaalamu, ikiwa ni pamoja na kufuata hatua muhimu kama vile kupima udongo kabla ya kupanda.

Nitoe wito kwa Watanzania wenzangu kuhusu kilimo hiki, kwani kwa hakika kinalipa kama utadhamiria, kuwa na nidhamu na kuheshimu kilimo kama sehemu ya maisha yako.

Kupitia papai, nakuthibitishia kuwa hutokuwa na haja ya kuendelea kutetemekea ajira au kulalamika kuwa hakuna ajira.

Nataka kuanzia sasa ufikirie namna unavyoweza kupata kipande cha ardhi na kukitumia kwa ajili ya kilimo.

Makundi ya papai

Mapapai yamegawanyika katika makundi mawili; mapapai ya kienyeji na yale ya kisasa.

Nashauri  watu kujikita zaidi kuzalisha mapapai ya kisasa, kwani yana soko, yana uzalishaji mkubwa na mbegu zake zinavumilia magonjwa

Nimekutana na maswali mengi kuhusu mbegu za kisasa kuwa zina matatizo kiafya, Niwatoe hofu  Watanzania

Kitaalamu mbegu za kisasa hazina madhara yoyote kiafya, ila udhaifu wake ni pale mtu anapoamua kupanda mbegu za papai ambalo amelivuna mara ya kwanza kutoka kwenye mbegu za kisasa.

Hii hairuhusiwi na ni makossa, pia ukilazimisha hautopata matunda kama ya awamu ya kwanza. Kitu chenye matatizo ni mbegu zinazotengenezwa kwa kutumia teknolojia ya uhandisi jeni (GMO).

Mbegu za GMO  zinatengenezwa huku ndani yake kukipandikizwa viumbe kama bakteria kwa lengo la  kupata mmea ambao unakuwa na kinga dhidi ya wadudu waharibifu wa mazao.

Mdudu akiushambulia huo mmea lazima afe na hata mifugo ikila majani au mbegu ya aina ya hiyo mimea lazima ife. Athari hii pia inaendelea hadi kwa binadamu.

Nini cha kuzingatia?

Kuna fedha nyingi kwenye zao la papai kama utazingatia upimaji wa  udongo, kuwa na chanzo cha kuaminika cha maji, mbegu bora na imara, utaalamu wa kilimo na uhakika wa soko.

Kwa kawaida, katika eka moja ya shamba miche 1,000 hadi  1,225 inaweza kupandikizwa.

Kwa makadirio ya chini, mche mmoja kwa mwaka unaweza kukutolea  matunda 100.

Kwa maana hiyo kama una miche yako 1,000 una uwezo wa kupata matunda 100,000. Sasa ukiamua uuze papai lako kwa bei ya hasara ya Sh 500, hesabu hiyo itakupa jibu la Sh 50,000,000. Unataka nini Mtanzania mwenzangu?

Kwa nini sasa tusiamue kulima papai kama ilivyo kwa matikiti na maembe ili ifike hatua sasa kila genge, soko ukienda uyakute mapapai kama tunavyoona matunda mengine?

Kumbuka bei ya hasara nimesema ni sh 500,  lakini kwa maeneo ya mjini, zao hili hufika Sh 4,000.

Papai la kisasa linaanza kuzaa kuanzia mwezi wa nne na mti hudumu kwa miaka mitatu hadi mitano.

Kaa chini fikiria namna ya kujikwamua na umaskini kwa kulima papai. Kwa nini uendelee kulaumu kuwa ajira hakuna au mshahara unaolipwa ni kiduchu?

Jackson Bwire ni mtaalamu wa kilimo cha mazao ya mbogamboga na matunda. 0715500136/0768279408