KILIMO BIASHARA: Umefikiria kulima papai?

Muktasari:

Mapapai yapo aina tatu, jinsia ya kiume, kike na jinsia zote (Hermaphrodite papaya).

Kilimo  kimeendelea kuwa na tija na kuleta sura ya kijasiriamali. Vijana wengi sasa wamejikita katika kilimo cha kisasa.

Si ajabu tena vijana kutumia muda mwingi kuzungumzia namna ya kulima zao lenye kipato cha haraka, siku hizi ofisini, sehemu za starehe na vijiweni au makundi ya Whattsap na mitandao mingine ya kijamii.

 Nimevutiwa na mada ya zao la mpapai, nimeona kilimo hiki kinafanyika kimazoea ingawa mahitaji ni makubwa, naomba nililete hapa hili somo ili tunafaike sote.

Mapapai yapo aina tatu, jinsia ya kiume, kike na jinsia zote (Hermaphrodite papaya).

Hata hivyo, aina zote tatu zinategemeana katika uzalishaji.

 Mpapai wenye maua ya kiume uhitajika katika urutubishaji wa mpapai wenye maua ya kike ili kupata matunda, ingawa wenye maua ya jinsia zote hujirutubisha wenyewe.

Zipo za aina mbili za mbegu: mbegu za kawaida ambazo huweza kupatikana popote kwenye papai lililoliwa. Changamoto iliyopo ni ugumu wa kubaini mbegu zipi ni za aina gani ya mpapai.

Aina ya pili ya mbegu ni chotara , mbegu zote huwa ni ya mipapai nyenye maua ya kike na ya kiume pamoja. Hii  hukua haraka na kutengeneza miti mifupi yenye uzao mkubwa ukilinganisha na ile ya kienyeji.

Upandaji

Panda mbegu moja tu kwa kila kiriba chenye udongo uliochanganywa vizuri na kujazwa robo tatu. Kisha viweke chini ya kivuli umwagilie maji.

Mbegu huchukua siku nane hadi 15 kuchomoza, hivyo hakikisha unamwagilia maji kila siku ila yasiwe maji mengi. Hamisha mche toka kwenye kitalu baada ya wiki ya sita hadi nane.

Hakikisha kazi ya uhamishaji mimea inafanyika wakati wa asubuhi sana, jioni ama kukiwa na mawingu ili kuzuia madhara ya jua kwa mimea.

Wakati wa kuhamishi miche shambani, hakikisha nafasi kati ya mmea na mmea ni mita 2 hadi 2.5 na kati ya mstari na mstari ni mita 2.5 hadi mita 3.

Andaa mashimo yenye upana na urefu wa sentimita 60, tenga udongo wa chini na wa juu kisha changanya udongo wa juu na mbolea ya samadi.

Unaporudisha udongo kwenye shimo tanguliza udongo uliochanganywa na mbolea ya samadi na juu malizia udongo ulioutoa chini wakati wa kuchimba shimo.

Kwa wale wenye mashamba makubwa, mipapai huingia kati ya miche 1000 hadi 2000 kwa hekari moja. Pia,  400 hadi 800 kwa ekari moja.

Mmea ukishahamia shambani bado kutahitajika matumizi ya mbolea, wiki moja baada ya kuhamishia shambani weka mbolea gramu 28 kila mmche lakini usitumie mbolea yenye Chlorine bali tumia yenye Phosphate, mfano; - 12:24:12. (NPK).

Baada ya hapo kila baada ya wiki mbili weka mbolea yenye Nitroni kwa kiasi kikubwa kiasi cha gramu 56 kwa mmea. Mfano, 20:10:10 (NPK).

Kisha tumia mbolea yenye Potassium kiasi cha gramu 114, baada ya maua na matunda kutokeza. Kisha fanya hivyo kila baada ya mwezi. Mfano wa mbolea hii ni 12:12:17 +2 (NPK).

Weka mbolea ya majani yenye virutubisho vidogo vidogo ikiwemo boron kila mwezi. Boron ni mbolea ya muhimu katika kupata matunda mazuri. Ukifuata utaratibu huu baada ya wiki 37 tangu kupanda mbegu utaanza kufaidi matunda hadi mpapai utakapochoka kuzaa.

Kwa mpapai uliotunzwa vizuri kwa msimu huweza kutoa matunda 80 hadi 120. Ikiwa umepanda mipapai 1000 kwa ekari maana yake utakua na mapapai 96,000 hadi 120,000.

0713593894