KONA YA KILIMO : Mafuta ya nje yanaathiri soko la alizeti nchini

Muktasari:

  • Zao hili lilipuuzwa  kwa kipindi kirefu kilichopita; licha ya ukweli kuwa  mahitaji ya mafuta ya kupikia au kukaangiza (edible vegetable cooking oil) yalikuwa yakiongezeka kwa kasi kila mwaka kutokana na kuboreka kwa kipato na maisha ya Watanzania,.
  • Ni kwa sababu hii, wafanyabiashara na wasindikaji wa mafuta ya kuupikia wakapata mwanya wa kuagiza mafuta ghafi ya mawese  kwa kiasi kikubwa kutoka nchi za nje hasa  Indonesia na Malaysia ili kuziba pengo la mahitaji.

Ukitaka kujua umuhimu na thamani halisi ya zao la alizeti, pitia mizania yetu ya biashara ya nje na ya kimataifa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita. Lipo utakalojifunza.
Zao hili lilipuuzwa  kwa kipindi kirefu kilichopita; licha ya ukweli kuwa  mahitaji ya mafuta ya kupikia au kukaangiza (edible vegetable cooking oil) yalikuwa yakiongezeka kwa kasi kila mwaka kutokana na kuboreka kwa kipato na maisha ya Watanzania,.
Ni kwa sababu hii, wafanyabiashara na wasindikaji wa mafuta ya kuupikia wakapata mwanya wa kuagiza mafuta ghafi ya mawese  kwa kiasi kikubwa kutoka nchi za nje hasa  Indonesia na Malaysia ili kuziba pengo la mahitaji.
Mahitaji ya mafuta ya kupikia au kukaangiza hapa nchini kwa makadirio ya watu milioni 55  na kipimo cha matumizi ya kilo 11 za mafuta kwa mtu kwa mwaka, yanaweza kufikia tani 605,000 za mafuta ya kupikia kwa mwaka.
Matumizi hayo ni wastani wa vijiko viwili vya chai vya mafuta ya kupikia kwa mtu mmoja kwa siku. Wengi tunajua matumizi yao ni makubwa zaidi ya kiwango hiki kilichowekwa na wataalamu wa masuala ya lishe.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Chakula Duniani (FAO), uzalishaji wa mbegu za alizeti ulikadiriwa kufikia tani milioni moja  mwaka 2013, ingawa takwimu za kilimo zilionyesha kiwango kikubwa zaidi.
Kwa ukamuaji wa mafuta wa kiwango cha lita 30 hadi 38 za mafuta kwa kila kilo 100 za mbegu za alizeti, uzalishaji wa mbegu kwa mwaka 2013 uliweza kutoa tani 380,000 za mafuta ya alizeti.
Ukweli ni kwamba, bado kuna kiasi kikubwa cha mbegu ghafi za alizeti zilizouzwa nchi za nje, hususan katika soko la India. Kwa hiyo, uzalishaji halisi wa mafuta ya alizeti ulikuwa chini ya makadirio hayo.
Kiasi cha mafuta ya alizeti kilichozalishwa hapa nchini kiliweza kutosheleza asilimia 40 tu ya mahitaji ya nchi. Asilimia 60 ya mahitaji ya mafuta nchini ilibidi yaagizwe kutoka nchi za nje ili kufidia pengo.
Utafiti mmoja wa FAO uliofanyika mwaka 2010 kwa awamu awamu mbili tofauti, ulibainisha kwamba iwapo fursa zote zilizopo nchini zitatumika kikamilifu na kwa tija ya hali ya juu, Tanzania ina uwezo wa kuzalisha tani milioni 100 za mbegu za alizeti kwa mwaka.
 Kiasi hicho cha uzalishaji kingeifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza duniani kwa uzalishaji wa mbegu za alizeti.
Tukirudi kwenye mizania yetu ya biashara ya nje katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, inabainisha kwamba bidhaa ya mafuta ghafi ya mawese ilikuwa katika kundi la bidhaa 10 za juu katika orodha ya bidhaa zilizoagizwa kutoka nje  kwa thamani.
Katika mwaka 2011 kwa mfano, bidhaa ya mafuta ghafi ya mawese ilishika nafasi ya 3 katika orodha ya bidhaa zilizo agizwa kutoka nje, na iligharimu Dola za Marekani milioni 274.6 baada ya mafuta ya petrol yaliyoshika mafasi ya kwanza, yakifuatiwa na ngano.
Mwaka 2012, bidhaa ya mafuta ghafi ya mawese ilishika nafasi ya nne  katika orodha ya bidhaa zilizoagizwa kutoka nje na iligharimu Dola za Marekani milioni 247.7 baada ya bidhaa za mafuta ya petroli na magari mchanganyiko.
Unaweza kuendelea na orodha hiyo, lakini ukweli utabakia kwamba mafuta ghafi ya mawese kutoka nje, yamekuwa yakiligharimu Taifa fedha nyingi za kigeni kwa kipindi kirefu.
Tukiangalia upande mwingine,  uzalishaji wa mafuta ya alizeti nchini ni wa kiwango cha chini na umekuwa ukisuasua kutokana na changamoto mbalimbali.
Wadau katika sekta ya alizeti wamekuwa wakilalamika kwamba, kuondolewa kabisa kwa ushuru wa forodha katika bidhaa ya mafuta ghafi ya mawese kutoka nje, na bidhaa hiyo ikiwa imeshapata ruzuku huko ilikozalishwa, kumeifanya shughuli nzima ya uzalishaji wa mafuta ya alizeti nchini kutolipa.