KSC yaongeza uzalishaji wa sukari 2016

Muktasari:

  • Kwa 2016/17, kampuni hiyo imezalisha tani 132,100 kutoka 121,702 za msimu uliotangulia. Kiasi kilichozalishwa kwa msimu huu ni kikubwa kwa miaka 10 iliyopita. Sukari nyingi zaidi iliyowahi kuzalishwa na kiwanda hicho ni ile ya msimu wa mwaka 2005/2006 ambao ulikuwa na tani 136,941.

Dar es Salaam. Mwaka mmoja baada ya Serikali kupiga marufuku uagizaji wa sukari kutoka nje, Kampuni ya Sukari Kilombero (KSC) imevunja rekodi yake ya miaka 10 iliyopita kwa kuongeza uzalishaji kwa msimu huu wa mwaka 2016/17.

Kwa 2016/17, kampuni hiyo imezalisha tani 132,100 kutoka 121,702 za msimu uliotangulia. Kiasi kilichozalishwa kwa msimu huu ni kikubwa kwa miaka 10 iliyopita. Sukari nyingi zaidi iliyowahi kuzalishwa na kiwanda hicho ni ile ya msimu wa mwaka 2005/2006 ambao ulikuwa na tani 136,941.

Mkurugenzi wa Uhusiano wa KSC, Joseph Rugaimukamu alisema juhudi za ufanisi huo zilianza Juni mwaka jana kwa kushirikiana na wakulima zaidi ya 8,000 ambao walipata tani 1.165 milioni zilizotumika kuzalisha sukari hiyo.

“Hii ni dalili njema ya kujitegemea katika mahitaji ya sukari nchini. Hali ikiendelea kuwa hivi itavutia uwekezaji zaidi na kwa ushirikiano uliopo baina yetu na wakulima ni jambo jingine muhimu,” alisema Rugaimukamu.

Taarifa za kampuni hiyo kubwa zaidi katika sekta ya sukari nchini inasema kwa miezi 18 iliyopita, bei ya miwa imeongezeka kutokana na juhudi za Serikali kuzuia uingizaji holela ambao umetoa soko la uhakika nchini. Inabainisha kwamba, tani moja ya miwa ambayo ilikuwa inanunuliwa kwa Sh59,000 msimu wa 2014/15 iliuzwa kwa Sh90,000 mwaka jana.

Februari mwaka jana, Rais John Magufuli alipiga marufuku uagizaji wa sukari kutoka nje ya nchi na kutaka mfumo ubadilishwe ili iwe inaagizwa kwa pamoja ili kulinda viwanda vya ndani na kukabiliana na magendo.

Vilevile, alieleza licha ya viwanda vya ndani kuzalisha sukari, hununua miwa kutoka kwa wakulima wadogo, kutoa ajira na kuchangia mapato ya Serikali bali kuna watu serikalini wanavikandamiza hivyo hakuna vibali vitakavyotolewa isipokuwa kwa mahitaji maalumu.

Mahitaji ya sukari nchini ni tani 420,000 kwa nyumbani na 170,000 kwa viwanda kwa mwaka, lakini uwezo wa uzalishaji kutoka viwanda vilivyopo ni tani 300,000 hivyo kuwa na upungufu wa tani 290,000 kila mwaka.

“Mafanikio yetu yamechangiwa na juhudi za Serikali. Soko limetulia kwa sasa hali inayovutia kuongeza uwekezaji,” alisema Rugaimukamu.

KSC kilichobinafsishwa mwaka 1998 kinalima zaidi ya hekta 10,000 za miwa kila mwaka huku kikiwekeza zaidi ya Sh240 bilioni na kuimarisha uzalishaji wa sukari kutoka wastani wa tani 30,000 miaka hiyo.

Mchango wa wakulima umeongezeka kutoka wastani wa tani 140,000 kabla ya ubinafsishaji mpaka zaidi ya tani 500,000 huku eneo lao likiongezeka kutoka hekta 3,500 mpaka 16,000 za miwa.

Mpaka Desemba, mwaka jana, kampuni hiyo ambayo inaongoza kwa kulipa kodi kubwa nchini, ikilipa zaidi ya Sh26 bilioni ilikuwa na wafanyakazi 3,700 huku wananchi wengine zaidi ya 100,000 wakiwa wananufaika kwa ajira zisizo za moja kwa moja.