KUTOKA LONDON : Bangi, kuku, mafuta muflisi na wasichana wetu

Muktasari:

  • Stephen Glover (Daily Mail) alidai George Michael, David Bowie na mshairi Leonard Cohen walikiri walivuta sana bangi na kunusa unga wa Cocaine, ujanani. Mpiga gitaa mkali Rick Parfitt (bendi maarufu, Status Quo) aliyefariki usiku wa kuamkia Krismasi aliwahi kuungama akiwa kijana alitumia paundi milioni 1.7 (zaidi ya dola milioni 2) kwa dawa za kulevya na sigara 30 kwa siku. Wote walifariki kwa mstuko wa moyo. Mwimbaji machachari Prince aliyefariki katika lifti alikuwa na miaka 57 tu. George Michael miaka 53. Kwanini wafe mapema vile?

Baada ya vifo vya wanamuziki maarufu wengi mwaka 2016 mwanasafu wa Kiingereza kauliza: “Vifo vyao ni janga ndiyo. Lakini kwanini hakuna mtu anayesema George Michael na wengine walikufa mapema baada ya kutumia dawa za kulevya miaka mingi?”

Stephen Glover (Daily Mail) alidai George Michael, David Bowie na mshairi Leonard Cohen walikiri walivuta sana bangi na kunusa unga wa Cocaine, ujanani. Mpiga gitaa mkali Rick Parfitt (bendi maarufu, Status Quo) aliyefariki usiku wa kuamkia Krismasi aliwahi kuungama akiwa kijana alitumia paundi milioni 1.7 (zaidi ya dola milioni 2) kwa dawa za kulevya na sigara 30 kwa siku. Wote walifariki kwa mstuko wa moyo. Mwimbaji machachari Prince aliyefariki katika lifti alikuwa na miaka 57 tu. George Michael miaka 53. Kwanini wafe mapema vile?

Funzo kwa vijana na Watanzania mnaohusudu dawa za kulevya, bangi na sigara, ni moja. Havina faida. Ikiwa vinaua matajiri, je sisi maskini?

Habari nyingine ni utupwaji wa vyakula vichafu au dawa Afrika. Kwa kuwa Waafrika hatuangalii sana tunachokula, kwa kuendekeza bei, ladha na urahisi, tumegeuzwa jalala la taka zisizotakiwa nchi zilizoendelea.

Nadhani mmesikia kuhusu mchele wa plastiki kutoka China.

Waafrika tunahusudu sana nyama.

“Ukitaka Mwafrika akufanyie lolote”, aliandika mwana riwaya, Wilbur Smith, (A Time To Die, 1989), “Mpe nyama.”

Mapenzi ya kuku wa kienyeji yamekwisha. Kuku wa taa wanapigiwa madebe. Mayai yanayotagwa kutokana na kuku waliofugwa haraka haraka katika hali mbaya yanazagaa Tanzania.

Kipya kinyemi

Mwaka 2014, ujumbe maalumu wa Serikali ya Marekani uliwasili kufanya kampeni ya Watanzania kununua kuku wa Brazil na Marekani. Habari zilizochapwa Citizen zilidai kuku hao wa kigeni hawakuelezwa wamekaa muda gani au kufugwa namna gani. Ili mradi wanatoka ng’ambo.

Huku Uzunguni vuguvugu dhidi ya kuku wanaofugwa haraka haraka katika mazingira mabaya ya kuteseka linazidi kukua. Wananchi wengi hawataki kula nyama. Nyama zinazofugwa hivi husababisha maradhi kama utasa, watoto kuzaliwa na magonjwa yasiyotibika, nk.

Jingine ni matumizi ya mafuta

Waafrika tunapenda sana vyakula vya mafuta, chumvi na sukari nyingi. Mfano mkuu ni wimbi la ulaji wa viazi vya kukaanga, yaani chips. Chakula hiki kilichovumbuliwa na Waingereza karne ya 19 kimetuchota kabisa Watanzania. Siku hizi hatupiki tena vyakula asilia. Mafuta yanatumika na kurudiwa rudiwa. Matokeo ni maradhi kama lehemu (cholestrol) na shinikizo la damu. Maradhi ya wazee yanawapata vijana : ukosefu wa nguvu za kiume, kisukari, mshtuko wa moyo, figo na utasa.

La mwisho ni tamko la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, la wasichana wetu kupewa nafasi ya kusoma hadi kidato cha sita. Sera hii ni nzuri shauri mfanyakazi mkuu katika jamii ya Kiafrika ni mwanamke. Mbali na kuzaa, mwanamke ndiye mfugaji, mlimaji na mlezi wa watoto. Kuna picha mtandaoni inawaonyesha wanawake kijijini Afrika wamebeba malundo ya kuni kichwani. George Monbiot anakejeli : “Ingekuwa utajiri ni matokeo ya bidii na kazi kila mwanamke Afrika angekuwa milionea.”

Lakini sivyo

Waziri Mkuu ameonya kifungo cha miaka 30 jela kwa mwanaume atakayesababisha msichana kuacha shule shauri ya mimba. Wanawake wetu wanategemea wanaume kifedha, kulalamika hawana ajira au kugeuka malaya. Tukiwasomesha wanawake, hatutaachana tu na tabia ya kuomba omba; pia tutajenga wataalamu watakaohakikisha ujinga unaondelea wa kula vibaya, kuweka sana chumvi katika vyakula au kutojua mambo kunapungua. Kumsomesha mwanamke ni kuendeleza taifa zima.