KUTOKA LONDON : Eti ,kwani ajabu watanzania hatukuambulia chochote Olimpiki 2016?

Muktasari:

Kuna utani uliosambazwa mtandaoni juma hili baada ya mashindano ya Brazil. Unaorodhesha nchi kadhaa za Afrika zilizopata medali.

Hebu tuweke Tanzania kando kidogo.

Tuzungumzie Afrika, Olimpiki ya Rio.

Kuna utani uliosambazwa mtandaoni juma hili baada ya mashindano ya Brazil. Unaorodhesha nchi kadhaa za Afrika zilizopata medali.

Afrika Kusini: Dhahabu 3. Fedha 2 na Shaba 1.

Ethiopia : Dhababu 2, Fedha 1.

Kenya: Dhahabu 1, Shaba 1.

Misri : Shaba moja. Tunisia: pia, Fedha moja.

Utani ukaongeza pilipili kwa kudai eti Nigeria : Shaba Nyekundu moja, Mbao 2, Mipira 3.

Tanzania: Alumini 4, Zinki 2, Magnezium 3, Asbesto 23 na Mawe manne.

Utani umekusudia Watanzania.

Je, ajabu Watanzania kutoambulia medali? Na je bara letu?

Kitakwimu, Olimpiki ya Rio, ilikuwa ya mafanikio zaidi kwa Waafrika kuliko awali. Medali zilizokusanywa Beijing mwaka 2008 zilikuwa 40. Olimpiki ya London 2012, bara Afrika lilipata medali 34.

Rio 2016 idadi imefikia 45. Medali tano zaidi ya Beijing; na 11 kuliko London.

BBC imesifu Waafrika kwa kusema Olimpiki ya Brazil ni ya mafanikio makubwa sana.

Kati ya vilele vya mafanikio haya ni ushindi wa medali ya dhahabu aliyoinyakua mkimbiaji wa mita 400- Wayde Van Niekerk, toka Afrika Kusini.

Mwanariadha Van Niekerk alipiku muda uliofikiwa mwaka 1999 na Michael Johnson kwa sekunde 43.03.

Hapajawahi kutokea Mwafrika kushinda dhahabu katika mbio fupi za haraka (“sprint”). Mbio hizi hutawaliwa na weusi wa visiwa vya Karibian, Marekani na Ulaya. Naye Almaz Ayana wa Ethiopia alivunja rekodi ya mbio 10,000 kwa sekundi 14 pungufu ya iliyowekwa na Mchina Wang Junxia, 1993. Ilidaiwa Junxia alitumia dawa za kuongeza nguvu (“doping”) jambo linalochunguzwa sasa hivi na Shirikisho la Riadha Duniani- IAAF.

Tatu, kwa mara ya kwanza Ivory Coast ilishinda dhahabu mchezo wa mapigano ya Tae Kwando . Cheick Sallah Cisse alimpiga mwenzie teke lililompa taji hiyo. Ivory Coast iko nafasi ya nne katika orodha ya washindi viongozi wa medali barani. Kenya (13), Afrika Kusini (10), Ethiopia (8), Ivory Coast (2) , Algeria (2), Niger (1), Misri naTunisia (3).

Afrika Kusini ni nchi pekee Afrika iliyopata ushindi michezo mbalimbali ikiwemo kutupa mkuki, kuruka, kuogelea , Rugby na riadha.

Orodha hii inathibitisha Afrika haikuzorota.

Ukichunguza utaona Kenya na Afrika Kusini ziliyapita mataifa matajiri kama New Zealand, Denmark, Canada hata Jamaica- yenye mkimbiaji mashuhuri, Usain Bolt. Majirani zetu walirudi na medali 13 ilhali Wajamaika 11. Kati ya hizo dhahabu za Kenya zilikuwa sita, Jamaica sita vile vile. Ila Kenya walipata medali za fedha sita huku Jamaica wakiambulia nusu yake.

Afrika Juu!

Sasa iweje utani na bezo zimesambazwa mitandaoni kuhusu Afrika? Kwamba Nigeria walishinda medali zilizotengenezwa kwa mipira (du!) na eti Tanzania wakarudi Dar Es Salaam na mawe (kashfa!) manne.

Kawaida watunzi wa matani ya aina hii mitandaoni huficha majina yao. Tungependa kujua nini hasa maudhui ya misuto kama hii. Iweje nchi zote zilizotajwa zilishinda medali za kweli, na Tanzania haimo kabisa orodhani? Iweje Nigeria iliyopata medali mbili, mojawapo shaba katika soka isutwe kwamba imeamulia medali za kutengenezea malapa (mpira)? Ikumbukwe mwaka 1996 -Nigeria ilishinda medali ya dhahabu, Olimpiki Atlanta, Marekani.

Tafakari.

Ikiwa chini ya kocha Samson Siasia na nahodha John Mikel Obi,Nieria ilipata shida sana kabla ya michuano. Ndege yao ilikwamishwa uwanja wa ndege wa Atlanta, Marekani ikielekea Brazil, kwa kusokena malipo ya safari. Wachezaji waligoma kwenda uwanjani kufanya mazoezi, sababu ya kutolipwa fedha za posho. Hata hivyo wanasoka hawa walipiga moyo konde, wakajitahidi kufikia nusu fainali. Wakawachapa Honduras 3-0.

Juhudi za Nigeria zilimgusa tajiri wa Kijapani, Katsuya Takasu, mganga wa upasuaji akasafiri hadi Rio De Janeiro kuwazawadia timu nzima ya Nigeria, Dola 390,000. Bw. Takasu alisema timu hii imeonesha ari ya mafanikio. “Ingekuwa wengine wangekata tamaa.”

Hapo sasa tujiulize vipi bezo limeilenga Nigeria?

Yumkini, utani uliilenga Tanzania.

Kama kawaida yetu hatukuambulia kitu.

Imekuwa desturi kurudi nyumbani mikono mitupu.

Wapenzi wa michezo na wazalendo tulifarijika tuliomwona mkimbiaji wa mbio ndefu za Marathon, Alphonce Simbu, akichukua nafasi ya tano. Tulifarijika tulipokuwa tukitazama wanaume wakikimbia katika mvua ya manyunyu mitaa ya Rio, Simbu akiwa mbele na kikosi kilichoongoza mbio hizo toka mwanzo hadi mwisho. Hatujawahi umwona Mtanzania akivalishwa medali huku “Mungu Ibariki Tanzania” ikiimbwa. Toka enzi za Juma Ikangaa, Sulemani Nyambui na Filbert Bayi.

Mwaka 2012 hapa London niliwahoji wachezaji na makocha wetu. Wote walilalamika namna vyombo vyetu vya habari vinavyowaponda kuwa hawafanyi vizuri. Ukweli wananchi tunatazamia wachezaji wetu kushinda medali. Kwani tuna tofauti gani na waEthiopia na Wakenya. Sote tuna mazingira yanayofanana fanana.

Ila siri na suluhisho siyo hilo peke yake. Wachezaji wana mioyo, vipaji na ari ya kushinda. Kinachokosekana ni msukumo wa juu. Nimeliona hili kwa hawa Waingereza nnaoishi nao.

Miaka 20 iliyopita Waingereza walifanya vibaya katika Olimpiki na riadha. Ndiyo walipata medali. Lakini hawakufikia kiwango mataifa ya wenzao matajiri. Wakatathmini udhaifu. Serikali na vyombo mbalimbali vya michezo vikaamua fedha ziwekezwe katika mafunzo, vifaa na taaluma.

Shirikisho la michezo, UK Sport lilipitisha paundi milioni 350 kusaidia wanamichezo kati ya 2013 hadi 2017. Matokeo mwaka huu Uingereza imeshika nafasi ya pili kwa kupata medali 67. Linganisha hizo na 15 za Wakenya au sifuri za Tanzania. Kati medali 67, dhahabu ni 27. Waingereza wamefanya vizuri katiak michezo mseto : mbio za farasi (mzee wa miaka 58 alipata dhahabu), kuogelea, ngumi, riadha (Mo Farah), ngalawa, sarakasi, nk.

Hapa inaridhihisha fika kuwa ushindi wa Olimpiki hutegemea wachezaji wanavyosaidiwa. Matayarisho Uingereza huanzia shule za msingi na kila taasisi husika vijijini na mijini. Hilo limezaa matokeo na mafanikio.

Waingereza sasa hivi wana hamasa na matumaini makubwa ya kuishi. Taifa hili lililoongoza ukoloni zamani ni la wabunifu sana. Wao ndiyo waliovumbua michezo mbalimbali mathalan mpira ya mikono, nyavu na miguu, (tunaoupenda), Kiingereza (tunachokizungumza), mabenki (tunayoyatumia) , hata mtandao au inteneti tunayoitumia (na kuienzi).

Ubunifu hufanikiwa pale wahusika wanapothaminiwa. Hilo ni funzo kwetu Tanzania. La sivyo tutabezana na kuchekana kisirisiri mitandaoni mithili ya wehu.

-Tovuti: www.freddymacha.com