Thursday, September 14, 2017

KUZA FURSA : Jipange kukuza biashara yako kwa wakati woteAlly  Mbuyu

Ally  Mbuyu 

By Ally Mbuyu

Muda wote biashara inatakiwa kukua kwa kutatua vikwazo vilivyopo na kuangalia fursa za ukuaji kwa siku zijazo.

Ili kuendelea kukua, mjasiriamali hutakiwa kutafakari mwenendo wa biashara uliopo na kuweka dira ya jinsi gani biashara yake itakua miaka kadhaa ijayo. Namna ya kutafakari ni kama vile unapokuwa juu ya ndege angani na ukaangalia chini, utaona ardhi na vingine jinsi vilivyokaa. Muonekano huo hutaweza kuuona ukiwa umesimama ardhini.

Hivyo dira na mipango itawekwa kwajinsi mjasiriamali anavyoiona biashara yake itakavyokuwa miaka labda mitano ijayo. Hivyo kuweka mikakati itakayowezesha kufikia malengo hayo inajumuisha kuwafunza wafanyakazi mbinu mpya za kuhudumia wateja, kufanya kazi kwa pamoja na kutatua matatizo yaliyopo kwa usahihi na umakini bila kuathiri biashara na wateja.

Dira na mikakati itasaidia pia kukabiliana na mabadiliko, kuwa imara katika kipindi cha mpito kufikia malengo na kufanyia kazi fursa mpya zinazojitokeza.

Katika kutafakari na kuandaa dira ya biashara, inashauriwa kuzingatia vitu kadhaa muhimu ili kuwa na uhakika wa kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Muundo wa kampuni ni miongoni mwa vitu hivyo. Mipango, dira na mikakati ya kukuza biashara lazima iangalie muundo wa biashara yako kwa maana kwamba kuna wafanyakazi wangapi kwa sasa na watahitajika wangapi ili kuongeza nguvu ya fikra na utaalamu, kuupanga upya muundo wa uongozi ambao utawezesha mafanikio yajayo, jinsi ya kuwaongoza wafanyakazi na vitendeakazi kufikia matokeo yatarajiwayo kwa muda mahsusi.

Kufikia malengo kunatakiwa kutengenezewa mazingira ya kila idara katika kampuni ama biashara ijitume kufanya kazi bila uzembe wala kutegea. Hii itasaidia matokeo yaliyokusudiwa kufikika kwa urahisi. Mazingira hayo ni kuzawadia wafanyakazi, kuweka malengo kwa kila idara na wafanyakazi, kupanga semina na mafunzo kukabili mabadiliko ya kampuni, biashara, masoko na utandawazi, kujituma na wafanyakazi kujua mwelekeo wa kampuni yao kikamilifu.

Matumizi ya teknolojia hayaepukiki. Mjasiriamali ni muhimu sana kujua matumizi mbalimbali ya teknolojia kwa kuongeza tija na kupanua uendeshaji. Teknolojia hizo ni pamoja na;

Program za mahesabu ambazo zinasaidia kuona faida na hasara muda mfupi na kurahisisha kuandaa bajeti na hivyo kumpunguzia kazi mhasibu na kumuwezesha kufanya kazi nyingi kwa muda mfupi na kwa uhakika.

Program za kisasa za kusimamia kalenda ya kazi ya kampuni na wafanyakazi. Pia husimamia siku za mikutano, maeneo ya mikutano, wahusika na kukumbusha siku moja kabla ya mikutano.

Program ya kupokea na kupangilia baruapepe za kampuni. Kwa wakati uliopo barua pepe ni nguzo ya mawasiliano kibiashara na kwa siku zinaingia barua pepe nyingi kwa mujibu wa ukubwa wa kampuni. Hivyo uwezo wa kujibu na kuzipanga kila siku inakuwa ni jambo gumu bila kuwa na visaidizi kama hivi vya barua pepe.

Ni muhimu kuangalia, kupanga na kuamua ni aina gani ya teknolojia inatakiwa katika biashara na utaalamu wa wafanyakazi ili kuleta ufanisi na kufikia malengo yaliyo kusudiwa.

Ikibidi fungua matawi. Kufungua matawi katika maeneo mengine kama vile wilaya, mikoa, kanda na nchi jirani kutegemea ukubwa na nguvu ya kampuni na biashara zake. Hii njia inatakiwa kuwa na uhakika wa soko kule ambako unatarajia kufungua matawi ili kuepuka hasara. Masoko yakiwa ya uhakika yatasaidia kampuni kukua kwa kuwa na soko pana na kuuza zaidi.

Usiogope kuchukua mkopo kutoka kwenye taasisi zinazoaminika. Wataalamu wa fedha wanahitajika kufanya upembuzi sahihi ili kuona uhitaji wa mkopo, uwezo wa kuusimamia, kiasi cha mkopo, uwezo wa kulipa na faida ya mkopo katika uzalishaji.

-->