KUZA FURSA : Zingatia nguzo muhimu ukuze biashara yako

Muktasari:

  • Kwa waliopo na wanaotarajia kuanzisha biashara ni muhimu kuzingatia nguzo zilizopo ili kufanikisha miradi yao na kukuza kipato kama walivyokusudia. Kila mfanyabiashara na mjasiriamali anapaswa kuzifahamu nguzo hizi.

Sekta ya biashara inaajiri Watanzania wengi nchini huku serikali ikiendelea kuhimiza ujenzi wa viwanda ili kuikuza zaidi.

Kwa waliopo na wanaotarajia kuanzisha biashara ni muhimu kuzingatia nguzo zilizopo ili kufanikisha miradi yao na kukuza kipato kama walivyokusudia. Kila mfanyabiashara na mjasiriamali anapaswa kuzifahamu nguzo hizi.

Biashara mpya nyingi huanzishwa kila mwaka wakati nyingi nyingine zikifungwa kutokana na sababu mbalimbali. Lililowazi kwa wafanyabiashara wanaoshindwa kuziendesha biashara zao ni kutokuwa makini kwenye baadhi ya mambo muhimu kwa ustawi wa biashara.

Hivi sasa serikali inasisitiza urasmishaji wa biashara hata kuandaa utaratibu wa kuwatambua wafanyabiashara na wachimbaji wadogo wa madini nchini. Vilevile, inahakiki taasisi zisizo za kiserikali (NGO). Kwa mabadiliko haya, kila mfanyabiashara anahitaji mikakati makini.

Kwa ufupi, hebu tuangalie misingi muhimu katika kuimarisha biashara yako uliyotumia muda mrefu kuijenga baada ya kukabiliana na changamoto zilizojitokeza mara kadhaa.

Unahitaji huduma za mwanasheria kufanikisha mambo yako mengi has amikataba ya kibiashara. Inategemea uwezo na ukubwa wa biashara ila unalazimika kuwa na mwanasheria ambaye atakuwa anakusaidia kuandika barua na mikataba ya kibiashara ili kuepuka mgogoro hapo baadaye hata kushinda kesi endapo zitakuwepo.

Mshauri wa biashara ni muhimu hasa unapokuwa na shida mbalimbali. Shida hizo ni kama vile upungufu wa wateja, kupata hasara, mafunzo ya wafanyakazi, kuandaa mipango ya biashara na kutathmini mwenendo wa biashara na namna ya kukabiliana na ushindani sokoni.

Hata kama biashara yako ni ndeogo, unahitaji mhasibu au huduma zake. Hii ni fani kamili kwa ajili ya kuandaa mambo mengi yakiwamo makadirio ya kodi utakayowasilisha Mamlaka ya Mapato au benki ili upate mkopo. Wataalamu hawa unaweza kuwakodi kwa muda ikibidi wakusaidie namna nzuri ya kuweka kumbukumbu za fedha za biashara.

Akaunti ya benki. Fedha zako zihifadhi benki kwa usalama zaidi. Chagua benki yenye faida, iliyo karibu na isiyo na usumbufu. Zipo benki nyingi kila kona zinazokuwezesha kuhifadhi fedha kwa urahisi.

Bima ni muhimu katika kupunguza uwezekano wa kukabiliana hasara inayoweza kujitokeza. Kuna kampuni tofauti za huduma za bima ambazo unaweza kuchagua uipendayo. Unahitaji utulivu na umakini ili kuepuka usumbufu mbele ya safari utakapohitaji kufidiwa. Bima husaidia kukabiliana na hasara katika biashara.

Kadi ya mmawasiliano ya biashara au business card ni muhimu katika kufahamika na kungeza wateja. Inashauriwa kutengeneza kadi nyingi kadri iwezekanavyo ambazo zinaeleza kwa ufupi shughuli, jina na anuani ya biashara yako. Unapokuwa nazo, ni vyema kuhakikisha mawasiliano unayoyaweka yanafanyiwa kazi muda wote.

Leseni na vibali vyote vinavyohitajika huthibitisha biashara yako imefuata taratibu na sheria za nchi. Lipia leseni ya biashara na vibali mbalimbali kwa mujibu sekta uliyomo kwani kupuuzia hili kutakuletea usumbufu ikiwamo uwezekano wa kufungiwa biashara yako na kuchukuliwa hatua za kisheria. Tumia wanasheria na wataalamu wa biashara kukufanyia kazi hizi ili kuepuka usumbufu.

Kujisajili Mamlaka ya Mapato. Kumbuka, biashara yeyote inatakiwa kusajiriwa na mammlaka hii ili kulipa kodi kwa mujibu wa sheria za nchi. Kuepuka usumbufu na hasara ni vyema ukaisajiri biashara yako mapema.

Ukiwa mjasiriamali na mfanyabiashara usijitenge na umoja au mashirikisho ya wafanyabiashara. Kujiunga huko kuna faida nyingi ikiwamo kujuana na watu wenye malengo kama yako, kujua fursa za uwekezaji, kupata mafunzo na misaada ama maelekezo ya kisheria na fedha.

Ni muhimu kuhudhuria maonyesho ya biashara kila unapokuwa na uwezo wa kufanya hivyo ili kuzitangaza bidhaa au huduma zako. Kuhudhuria maonyesho kunahitaji maandalizi ya kutosha ili kupata faida na kuepuka hasara.

Mitandao ya jamii ni nguzo muhimu ya kutangaza biashara siku hizi. Kwa mjasiriamali mwenye bidhaa mbalimbali unazotengeneza ni vyema ukajiunga katika mitandao ya kijamii ili kutangaza bidhaa zako kama njia ya kutafuta wateja wapya na kufahamika zaidi.