Kama Waziri Nape anakosa uvumilivu kiasi hiki, hiyo Sheria ya Habari itakuwaje?

Muktasari:

“Uzoefu unaonyesha kuwapo kwa tofauti kati ya vyeti na utendaji wa kazi. Wapo baadhi ya waajiri wameshindwa kuwaajiri wahitimu wa vyuo vikuu wenye shahada za uandishi wa habari kwa sababu hawana ujuzi badala yake wameajiri wenye elimu ndogo au shahada za fani nyingine wenye utendaji mzuri.”

Hivi karibuni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amewasilisha Muswada wa Huduma za Habari Bungeni ukiwa ni mchakato wa uundwaji wa Sheria mpya ya huduma za habari.

Hatua hizo zinawataka pia wadau na wananchi kwa jumla kutoa maoni yao ili kuuboresha kabla sheria haijatungwa rasmi bungeni.

Muswada huo unaanzia kwenye Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii na kujadiliwa na wajumbe wa kamati hiyo na wadau kutoa maoni yao.

Wakati wabunge na wadau wakianza kutoa maoni yao, tayari kuna walakini kwa upande wa Serikali katika upokeaji wa maoni.

Walakini huo umeonyeshwa na Waziri Nape alipomuibukia Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo), Zitto Kabwe baada ya kutoa maoni yake mitandaoni.

Zitto katika maoni yake ameukosoa muswada huyo akisema ni hatari kwa tasnia ya habari na uhuru wa maoni kwa wananchi. Amechambua vifungu kadha wa kadha huku akikosoa ushirikishwaji wa wadau kama utaratibu wa kuwasilishwa kwa miswada.

Andiko la Zitto lilisambaa mitandaoni na kusomwa na watu wengi mwishoni mwa wiki iliyopita. Ghafla Nape naye akamrushia kombora akimuita mnafiki.

Kwa ujumla majibu ya Nape yamejaa kejeli na dhihaka kwa mbunge mwenzake aliyekuwa akitoa maoni yake.

Inawezekana Nape ameunganisha matukio na kuamua kutumia nafasi hiyo kumnanga Zitto.

Itakumbukwa katika Bunge la Bajeti wakati Nape akiwasilisha bajeti ya wizara yake, miongoni mwa wabunge waliochangia kwa hisia kali ni Zitto.

Zitto alimkosoa vikali Nape katika hotuba yake hiyo akisema kwa mfano hotuba nzima haijataja hata timu ya Taifa. Pia, alikosoa suala la kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya televisheni kwa vipindi vya Bunge.

Japo Nape hakumjibu Zitto moja kwa moja, lakini alionekana kukasirika. Sasa inawezekana anaunganisha na ukosoaji huru tena kwenye muswada.

Vyovyote itakavyokuwa, Nape amekosea katika hili. Kwanza kabisa huu ni wakati wa wadau kutoa maoni yao kwa muswada, Zitto kama mdau katoa yake, tatizo liko wapi? Au kosa la Zitto ni kukosoa muswada? Au ndiyo kusema Nape anataka maoni ya kuusifu muswada tu?

Tuseme Nape atawajibu wadau wote kama alivyofanya kwa Zitto au ana ugomvi naye binafsi?

Jambo la pili, Nape anajua kwamba Zitto ni mbunge wa upinzani? Alitarajia nini kutoka kwake?

Tatu, majibu ya Nape kwa Zitto mitandaoni yanatoa picha gani kwa watoa maoni wengine? Kwamba ukikosoa muswada waziri anakuibukia na kukunanga?

Kama mbunge anaweza kujibiwa kwa dhihaka hivi, wachangiaji wengine itakuwaje?  Nadhani kwa kuwa huu ni wakati wa wadau kutoa maoni yao, Nape alipaswa kuwa mvumilivu kuwasikiliza hata kama maoni yao ni machungu kiasi gani.

Kama vitisho vinaanza kwa watoa maoni, hiyo sheria itakuwaje? Kwa nini sheria isukumwe kwa vitisho?

Kabla hata ya kuingia kwenye maudhui ya muswada wenyewe, wadau wa habari tunaanza kutilia shaka mikakati ya Serikali kutunga sheria hiyo.

Siyo kwamba wote ni mbaya, kuna mambo ya msingi na yenye manufaa kwa waandishi na vyombo vya habari. Kwa mfano, suala la masilahi limejadiliwa na pengine likawa suluhisho kwa waandishi wengi ambao hawana uhakika wa ajira zao.

Utata uliopo

Utata unaanzia kwenye tafsiri ya mwandishi wa habari hasa katika elimu. Je, ni lazima mwandishi asomee uandishi wa habari ndipo atambulike?

Mwandishi bora ni yule aliye na stashahada au shahada ya uandishi wa habari na siyo fani nyingine? Uandishi wa habari ni vyeti au utendaji wa kazi? Ni waandishi wangapi wenye hizo shahada za uandishi?

Uzoefu unaonyesha kuwapo kwa tofauti kati ya vyeti na utendaji wa kazi. Wapo baadhi ya waajiri wameshindwa kuwaajiri wahitimu wa vyuo vikuu wenye shahada za uandishi wa habari kwa sababu hawana ujuzi, badala yake wameajiri wenye elimu ndogo au wenye shahada za fani nyingine wenye utendaji mzuri.

Hapa kuna utata mkubwa na usipoangaliwa, utaivuruga tasnia ya habari.

Jambo lingine katika muswada huo ni madaraka atakayokuwa nayo waziri wa habari. Tazama sehemu ya 7(1)(b)(iv) inatamka wazi kwamba waziri anaweza kuagiza chombo chochote cha habari cha binafsi kutangaza habari fulani au masuala fulani yenye umuhimu kwa taifa.

Kwamba waziri mwenye dhamana ataweka vigezo na masharti kwa uendeshaji wa vyombo vya habari, hapo kutakuwa tena na uhuru wa habari?

Maoni yangu hasa kwa waandishi wa habari wawe wa vyombo binafsi au vya Serikali, muswada huu siyo lelemama. Ni mapambano kwa sababu tutakaoathirika ni sisi.

Kwa mfano, ukiangalia baadhi ya adhabu zinazotajwa kwenye muswada huo ni ama miaka mitatu jela au faini ya kati ya Sh5 milioni na Sh10 milioni. Maisha haya ya uandishi unaipataje hela hiyo? Kazi yenyewe ina harakati nyingi, kupata habari ya kuuza gazeti siyo mchezo.

Halafu Nape anasema, huo ni muswada unaowajali waandishi. Hivi ukishamfunga mtu miaka mitatu kwa kosa ambalo labda angeomba radhi au hata kupatana na aliyemkosea, umemsaidiaje?

Sijui kama Nape amewahi kufanya kazi kwenye chombo cha habari akapata uzoefu walau wa miaka miwili au mitatu, ndipo aelewe ninachokieleza.

Sipingi njia za uwajibishaji, kama faini au vifungo, wala sisemi kwamba uandishi ni kazi holela, lakini muswada huu umepitiliza. Utaua kabisa uandishi wa habari na uhuru wa wananchi kutoa maoni ambayo ni haki ya kikatiba.

Yaani waandishi tutalazimika kuelekezwa cha kuandika. Hata haya maoni ninayoandika hapa itakuwa shida. Huwezi kuzungumzia uhuru wa maoni wakati waziri wa habari anapewa madaraka ya kuamua chombo cha habari kiandike nini.

Kubanwa vyombo vya habari

Kuna kila dalili kwamba Serikali haipendi kuhojiwa wala kukosolewa kwa kila inalofanya. Ndiyo maana walipoingia madarakani kwanza wamefuta vipindi vya Bunge vya moja kwa moja wakiacha kipindi cha maswali na majibu tu.

Awali Nape alisema ni kutokana na gharama kubwa inazoingia TBC, lakini walipotokea wafadhili akabadilika tena. Sasa hata kuripori Bunge inabidi wapigapicha wa televisheni wakaombe kwenye studio za Bunge.

Ni wakati huu tunaona utekelezaji wa sheria ngumu za Makosa ya Mitandao na Sheria ya Takwimu. Wengi wameshaonja machungu ya sheria hizi.

Kwa muda mrefu wanahabari tumekuwa tukilalamikia Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976, leo inaletwa sheria mbovu zaidi ya hiyo. Kama kweli Nape anataka kuisaidia tasnia ya habari nchini angepambana na sheria hizi na siyo kuziongeza.

Namaliza kwa kusema kuwa, muswada huu ni hatari kwa tasnia ya habari na uhuru wa maoni kwa wananchi wote. Ni hatari kwa utawala wa kidemokrasia tulionao. Wadau wa habari na wabunge tuukatae kwa masilahi ya Taifa letu.

Namshauri Waziri Nape awe mvumilivu wa kukosolewa na atoe muda wa kutosha kuujadili muswada huru ili tufukie mwafaka. Muda uliotolewa hautoshi, waandishi na wadau wapewe walau miezi mitatu tena ya kujadili bila kutishiwa, vinginevyo tutauziwa mbuzi kwenye gunia.

Elias Msuya ni mwandishi wa gazeti hili. [email protected] na 0754897287