Kampeni zinavyoamsha hamu ya mikutano ya siasa

Muktasari:

  • Uchaguzi huu wa madiwani, ni moja ya vipimo vya kujua uhai wa vyama vya siasa katika ngazi za chini.

Kampeni za uchaguzi wa mdogo madiwani katika Kata 43 unaotarajiwa kufanyika Jumapili, zinaendelea kwa kasi.

Uchaguzi huu wa madiwani, ni moja ya vipimo vya kujua uhai wa vyama vya siasa katika ngazi za chini.

Vyama vyote vikubwa vya siasa, CCM, Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi, ACT-Wazalendo na vingine zimesimamisha wagombea na vinaendelea kuwanadi kwa wananchi.

Tofauti na chaguzi ndogo zilizopita, hadi sasa hakuna mgombea yoyote wa udiwani ambaye amepitia bila kupingwa, japo jaribio la kuwaengua baadhi yao lilifanyika na kukataliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Hii ni ishara nzuri ya kukua kwa demokrasia nchini, ingawa kuna kata ambazo uchaguzi unafanyika kutokana na madiwani kujiuzulu kwa sababu mbalimbali yakiwamo madai ya kurubuniwa au kuhongwa.

Tofauti na chaguzi zilizopita za udiwani, hivi sasa tunashuhudia vyama vya siasa vikiwatumia viongozi wake wa kitaifa katika kampeni.

Vilevile tunashuhudia baadhi ya mawaziri, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wakipanda katika majukwaa ya kampeni kuwaombea kura wagombea wa vyama vyao.

Hatua hii inaonesha ni jinsi gani, uchaguzi huu ulivyopewa uzito na vyama vyote vya siasa.

Jambo zuri zaidi hadi sasa kampeni katika maeneo mengi ni shwari japo kuna maeneo ya kuanza kuumizana miongoni mwa wafuasi wa vyama, jambo ambalo halina tija kwa nchi wala vyama vyao.

Vilevile katika siku za karibuni, tumeanza kuona kukamata ya wanasiasa kutokana na kauli zao majukwaani au mizozo baada ya kampeni.

Ingawa sheria zinaruhusu kukamata watuhumiwa wanapovunja sheria wakati wowote, lakini naamini ni busara sasa vyama vya siasa vikaachwa kupambana vyenyewe kwa hoja.

Kamatakamata ikiendelea inaweza kuathiri uchaguzi huu mdogo jambo ambalo sio zuri katika kushamirisha demokrasia.

Naamini kutokana na kuzuiwa mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa, sasa wamepata fursa ya kuwasiliana na wananchi, hivyo wangeachwa kufanya kazi hiyo ambayo ni kwa mujibu wa Katiba kwa kuwa katika mazingira ya sasa, uvumilivu wa kisiasa ni jambo jema sana kwani taifa linapita katika kipindi kigumu ambacho wanasiasa wengi hawakukizoea.

Vyama vya siasa vilizoea mikutano na maandamano, kila kukicha lakini sasa utaratibu umewekwa kuzuia maandamano na mikutano isiyo na tija kwa Serikali.

Ingawa suala hili linakinzana na sheria ya vyama vya siasa, lakini limeanza kuzoeleka taratibu, hivyo uchaguzi mdogo wa madiwani umekuwa ni fursa kwa vyama vya siasa kurejesha siasa za majukwaani walau kwa mwezi mmoja.

Wanasiasa wakipata nafasi ya “kupumua” ni afya katika ujenzi wa demokrasia kuliko kukaa wakiwa wananung’unika na mwisho wanaweza kuibuka na mambo ambayo yanaweza kuyumbisha utulivu na amani.

Lakini ni vizuri vyombo vyetu vya dola sasa vikawavumilia wanasiasa wetu kidogo, kwa kuzingatia kuwa wamepata fursa kupumua yaliyo moyoni mwao, la sivyo vinaweza kuwa na utaratibu wa kuwaita viongozi wa kisiasa na kuwapa onyo na wakirudia makosa wawachukulie hatua.

Kufanya hivi wataacha uwanja ulio sawa wa kisiasa katika kampeni hizi za madiwani ambazo kimsingi hazina madhara makubwa.