Karibu TTCL Kindamba, tutakupima kwa namba

Waziri Kindamba, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Simu (TTCL)

Muktasari:

Hata hivyo, sikutaka kumpongeza Kindamba mapema kiasi hicho kabla sijaona namba za kiutendaji zinazohusiana na TTCL ambazo zinaweza kusaidia kupima anapoanzia.

Baada ya Rais John Magufuli kumteua Waziri Kindamba kuwa Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Simu (TTCL), nilitamani kutoa pongezi za uteuzi huo.

Hata hivyo, sikutaka kumpongeza Kindamba mapema kiasi hicho kabla sijaona namba za kiutendaji zinazohusiana na TTCL ambazo zinaweza kusaidia kupima anapoanzia.

Jambo la haraka nililoweza kufanya ni kumtakia kila la kheri Dk Kamugisha Kazaura, ofisa mtendaji mkuu wa zamani kwa kupambana na kuifikisha TTCL ilipo.

Lakini baada ya Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kutoa takwimu za sekta ya mawasiliano za robo ya pili ya mwaka huu wiki iliyopita, naweza nikampongeza Kindamba kwa kuteuliwa kwake na kumtakia heri katika nafasi hiyo mpya.

Kindamba anaingia TTCL ikiwa imedumaa. Ina asilimia moja tu ya watumiaji wote wa simu za mkononi nchini licha ya ukongwe wa miaka 22 sokoni.

Takwimu za robo mwaka ya kati ya Aprili na Juni mwaka huu zinaonyesha, TTCL ilikuwa na wateja 304,058 kiwango ambacho ni chini ya kile kilichorekodiwa Oktoba, 2014 wakati ikiwa na watumiaji 324,470. Wateja wanapungua.

Kwa miaka yote hiyo TTCL imekuwa na mipango mikakati lukuki kama kampuni yoyote ya simu ikiwemo kuvutia wananchi kutumia huduma za simu za mkononi. Takwimu za TCRA zikitumika kama nguzo ya kupima utendaji wa kampuni, mikakati hiyo haijazaa matunda iwapo.

Kwa mfano, Oktoba 2015 TTCL ilikuwa na wateja wa huduma za simu 304,214 idadi ambayo haikukua wala kupungua hadi mwishoni mwa mwaka jana.

Wakati Halotel iliyoanza biashara zake rasmi mwaka jana, Oktoba ilikuwa na wateja 433,295 kiwango ambacho ni juu ya kile cha TTCL kwa watumiaji zaidi ya 130,000.

Ndani ya muda mfupi Halotel ilipiga hatua ndani ya miezi mitatu na kuongeza wateja hadi kufikia 1.22 milioni kiwango kilichowafanya imiliki soko kwa asilimia tatu wakati TTCL ikibakiwa na asilimia moja ileile.

Pamoja na kwamba Halotel ni kampuni changa tayari imezidi kujiimarisha na hadi Juni mwaka huu tayari ilikuwa na asilimia saba ya watumiaji wa simu nchini na kupunguza soko la mitandao mingine mikongwe ikiwemo Zantel na Smart. Kiwango hicho hakijafikiwa na TTCL kwa miaka zaidi ya mitano.

Tofauti na kampuni nyingine za simu, TTCL inamiliki miundombinu mingi ya mawasiliano hususan ya intaneti kama mkongo wa taifa inayofanya iwe na nguvu kubwa kibiashara.

Ni dhahiri kuwa TTCL ilikuwa ikipitia wakati mgumu wa kifedha na kimenejimenti kama yalivyokuwa mashirika mengine ya umma yaliyokuwa yakiendeshwa kwa ubia na wawekezaji. Lakini kadhia hizo zimeanza kutatuliwa.

Juni mwaka huu, Serikali ilirudisha asilimia 35 ya hisa zilizokuwa zinamilikiwa na Bharti Airtel na kuifanya kuwa shirika la umma kwa asilimia 100. Pia, Rais Magufuli amemteua Kindamba kuanzisha safari hiyo mpya.

Pamoja na hayo, kuna baadhi ya namba ambazo hazipo wazi. Taarifa za kifedha. Wengi tungetamani tuone Kindamba anaanzaje kifedha na kufahamu kiasi kinachoingizwa na mauzo ya intaneti.

Tungependa pia kufahamu mustakabali wa biashara hiyo upoje hasa baada ya kuanzisha huduma ya intaneti ya kasi ya kizazi cha nne (4G) chini ya kampeni iitwayo kizazi T?

Ni shauku yetu kufahamu uelekeo wa kuendelea na biashara ya sauti hususan simu za mkononi na mpango wa kuanzisha huduma za kifedha kupitia simu za mkononi kama unaweza kuiinua kampuni hiyo.

Kindamba huenda ameshasoma namba zake tayari lakini kazi iliyopo mbele yake siyo ndogo na wengi tunatarajia uzoefu wake kibiashara utasaidia kubadili kampuni hiyo kwa kuongeza wateja na kufanikisha kupunguza mwanya wa huduma za intaneti nchini.

Hata hivyo, tofauti na watangulizi wake anaingia kipindi ambacho watu wanahitaji uwazi na uwajibikaji kuliko vyote.

Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru tayari ameshatangaza kuwa Serikali ina mpango wa kuyataka mashirika yote ya umma kuchapisha taarifa za fedha kila mwisho wa mwaka ili wananchi wajionee nani anapata hasara na nani anaendesha vyema shirika lake.

Kindamba anaweza kuyashinda haya iwapo ataongoza mabadiliko chanya ambayo nayaona yatapaa kwa kasi miaka ijayo kama TTCL itaingia Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) na kuuza asilimia 49 kwa wananchi.

Bado kuna fursa ya kutumia vyema soko la intaneti linalokua kwa kasi. Kila siku mahitaji ya intaneti yanaongezeka huku zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania wakiwa hawafikiwi na intaneti ya uhakika.

Tofauti na miaka ya nyuma, Watanzania hawanunui huduma au bidhaa kwa dhana ya uzalendo kwa mashirika ya umma. Wengi tunataka huduma bora. Kila la kheri Kindamba katika safari ya kuifanya Tanzania kuwa ya dijitali.