Katiba ni tunda la utii wa kizazi na nyakati

Muktasari:

  • Tume ile ilipomaliza kazi yake ikaleta majibu, asilimia 20 ya Watanzania walitaka vyama vingi, Wengine walio wengi, asilimia 80, walikataa vyama vingi, walitaka kibaki chama kimoja.

Hivi karibuni kumekuwa na mjadala mkubwa kuhusu mahitaji ya Katiba mpya. Mjadala huu umechochewa zaidi na kauli za viongozi mbalimbali wakiwemo maaskofu, wachungaji, mashehe, viongozi wa kijamii, kisiasa na taasisi nyingine zikiwemo zile ambazo zimethubutu hata kufanya utafiti kwa wananchi ili kujiridhisha wanaihitaji Katiba mpya kwa kiasi gani na yapi ni mambo muhimu yanayowasukuma wananchi katika kiu hiyo.

Tafiti za sasa na miaka ya tisini

Tafiti za sasa juu ya Katiba mpya zinasadifu nyakati zile za miaka ya tisini ambapo kulikuwa na mahitaji makubwa ya kurejesha mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania. Juhudi za makundi mbalimbali zilisisitiza kuwa lazima Tanzania irejee kwenye mfumo wa vyama vingi na ilibidi Serikali itekeleze matakwa ya wananchi, ikaundwa Tume ya kukusanya maoni ili kujua kama wananchi wanataka vyama vingi.

Tume ile ilipomaliza kazi yake ikaleta majibu, asilimia 20 ya Watanzania walitaka vyama vingi, Wengine walio wengi, asilimia 80, walikataa vyama vingi, walitaka kibaki chama kimoja.

Kama Mwalimu Nyerere asingelikuwa na ushawishi mkubwa ndani ya CCM, Tanzania ingechelewa kurudi kwenye mfumo wa vyama vingi. Wakati CCM ikishangilia kuwa wananchi wamepiga kura za kukataa vyama vingi, mwalimu akawa mwiba kwa sherehe zile na akakishawishi chama chake kikubali nchi irejeshe mfumo wa vyama vingi kwa sababu hata kama wengi hawataki, lakini nyakati zinataka.

Nguvu ya nyakati

Nyakati ni kila kitu katika kila jambo na huwa hazimsubiri mtu. Binadamu hupaswa kuishi kwa kuangalia majira na nyakati na hupaswa kuishi kwa kujipambanua ndani ya mazingira yanayoandaliwa na nyakati.

Mwanadamu hajawahi kushindana na nyakati na majira, tangu enzi. Ni kanuni ya asili ya maisha ya mwanadamu tangu anazaliwa kwamba ataishi kulingana na nyakati na mabadiliko yaliyopo, binadamu anaposhindana na kanuni za asili hushindwa vibaya na huanguka anguko kuu.

Mwalimu Nyerere alipowaambia wana CCM kuwa lazima sasa turejee kwenye vyama vingi hata kama wengi wao hawataki na hata kama maoni ya Watanzania yanaunga mkono msimamo huo wa CCM, alikuwa anafanya kitu kimoja tu - kutopingana na kanuni ya asili ya mabadiliko ambayo mwalimu alijua itaiathiri sana nchi ikiwa tungelipambana na nyakati.

Kanuni ya asili ya nyakati iko kwenye kila kitu tangu mwanadamu anazaliwa hadi anakufa. Mtoto mdogo anapozaliwa, yako majira yatafika lazima aanze kukaa, kama akizuiwa kukaa basi atakuwa na ulemavu wa milele, na anapokaa huchukua muda mfupi majira yakitaka atambae, akizuiwa kutambaa basi atapata ulemavu wa kudumu na ikiwa atavuka hatua moja kati ya hizo bila kushiriki bado atapata madhara. Ni lazima binadamu apite kwenye nyakati na azifuate.

Nyakati na majira

Katiba mpya ya Tanzania ni suala la majira pia, ni suala la nyakati pia. Rais Kikwete alipokubali kuanzisha mchakato wa Katiba ni kwa sababu aliamini kuwa nyakati za sasa ni mpya kabisa na zinahitaji utaratibu mpya wa kujiongoza.

Na bila kumsemea JK tunaweza kuzitafakari sababu nyingi ambazo zilimsukuma kusimamia mchakato wa kusaka Katiba mpya, sababu kubwa ikiwa ni kizazi.

Katiba ya sasa ya Tanzania ilitungwa mwaka 1977 kwa kiasi kikubwa ikirithi mifumo ya kikoloni na mbinu za uendeshaji wa siasa, uchumi na jamii kwa tafsiri ya mkoloni.

Huo ni wakati ambao Tanzania haikuwa na wasomi wa kutosha kufikiri vizuri juu ya Katiba ya muda mrefu. Na ukichanganya na masuala ya siasa za ujamaa na kujitegemea na mambo kama hayo, taifa lilijikuta linakuwa na Katiba ambayo inaweza kuendesha mifumo fulani tu ya maisha ya kizazi cha wakati huo.

Mahitaji makubwa ya kizazi cha wakati huo yalikuwa ni uwezo wa kuishi wakati huo, wazazi wengi wa wakati huo hawakuwaza kuwa kuna maisha baada ya nguvu za ujana, wengi wao walifanya kazi tu ofisini bila kufanya na biashara moja au mbili, wengine walilima tu shambani bila kuanzisha ofisi ndogo ya ufundi ili wakusanye vipato na kuvitunza kwa ajili ya maisha ya uzeeni.

Kwa kiasi kikubwa, maisha ya wazazi wetu yalijishughulisha na kuishi wakati huo kuliko kuandaa maisha ya mbele.

Tafsiri hiyo ya maisha ya wazazi wetu inaakisi bongo zilizokuwemo serikalini na kwingineko, na walifikiri sana kuhusu Serikali ya wakati huo na maendeleo yake. Serikali nyingi za zamani ziliishi zaidi wakati huo kuliko kutegemea mabadiliko ya nyakati yanayokuja kwa nguvu sana.

Katiba ya Tanzania nayo lazima iliakisi wakati huo, haikuwa inaangalia mbali sana na ndiyo maana kizazi kipya kilipokuja kimejiridhisha kuwa Katiba hiyo si ya sasa na haibebi matakwa ya taifa la kisasa na kwamba lazima ibadilishwe.

Katika mpya lazima

Kubadilisha Katiba ya nchi, au kutunga Katiba mpya ili kuendesha Taifa la kisasa, uchumi wa leo, siasa za nyakati hizi na jamii iliyopo si jambo la hiari ya watu au kikundi cha watu, wawe wengi au wachache.

Hitaji la Katiba mpya ni la nyakati na kizazi cha sasa na si hiari ya viongozi au kiongozi na kwa kweli si jambo la hiari hata kwa CCM yenyewe.

Na hata kama CCM inahitaji kutawala zaidi miaka ijayo, kulilinda taifa na kizazi cha sasa katiba ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele.

Na taifa hulindwa kwa kufuata matakwa ya nyakati ambapo kizazi husika kinaishi na kama chama chochote kinataka kutawala zaidi lazima kijinyumbulishe kwa uwazi na kwa nia njema katika nyakati hizo na kizazi hicho.

Ninapozungumzia kujiandaa kuenenda na wakati simaanishi kuwa ndiyo tiketi ya kutafuta namna ya kudhibiti wakati au majira. Nyakati - hazidhibitiki na hazijawahi kudhibitika, hiyo ni kanuni ya asili.

Mathalani, kizazi cha sasa na wakati tuliopo ni enzi za ukuaji mkubwa wa teknolojia na uhuru wa kutoa maoni duniani, ni wakati ambapo wananchi kwenye mataifa yote wanaelekea kwenye uhuru mkubwa wa mawazo na matumizi ya juu ya mitandao ya kijamii, taifa linalofuata kanuni ya asili ya kuheshimu vizazi, majira na nyakati, litawekeza nguvu kubwa katika kuwasaidia wananchi kuongeza matumizi ya teknolojia, kuongeza uhuru wa kutoa maoni na mawazo na kufanya matumizi zaidi ya mitandao kwa faida za kijamii na kiuchumi.

Inakuwa ni kichekesho kukuta leo baadhi ya mataifa ndio yanaamka na kung’ang’ana na njia nyingi na nguvu kubwa ili kudhibiti kizazi cha sasa, kudhibiti uhuru wa kutoa maoni, teknolojia na utumiaji ya mitandao ya kijamii. Taifa linalojaribu kupita njia ya namna hii linajipiga ngwala za kudumu lenyewe, maana kanuni ya asili inaonesha kuwa hakuna taifa linaloweza kupambana na vizazi na wakati na nyakati na majira.

Kizazi cha sasa, majira ya sasa, nyakati za sasa na Watanzania wa sasa unawaona kwa maneno, vitendo na viashiria, kwamba wanahitaji Katiba mpya.

Na wanaihitaji katiba kwa sababu za msingi za kiuchumi, kijamii na kisiasa na hawa nao hawafanyi hivi kwa kupenda, wanafanya hivi kwa sababu hawawezi kushindana na kanuni ya asili ya maisha, kanuni ya kuenenda kulingana na wakati na majira, kanuni ya kutii mahitaji ya kizazi cha sasa.

Kwa hiyo, presha za sasa za Watanzania, za kutaka mchakato wa Katiba urejelewe upya, hazina maana yoyote zaidi ya utii wa kanuni ya asili ya maisha ya mwanadamu.

Sauti hizi zikipuuzwa ati kwa sababu wapo watu wanajaribu kulinda vyeo vyao, watu hao wataangushwa kwa sababu kila aliyepingana na kanuni ya asili ya maisha ya mwanadamu, alianguka.

Nilimsikia Askofu mmoja akisema (sijui kama ni kwa niaba ya kanisa, ambalo na mimi ni muumini), kwamba kipaumbele cha nchi yetu si Katiba mpya. Askofu huyu hakuzungumza kwa niaba ya waumini wake, naye alizungumza kwa niaba yake mwenyewe.

Mwalimu Nyerere wakati ule aliposema wachache wasikilizwe, alizungumza kwa niaba ya vizazi na vizazi, Mwalimu angeliweza kusema “Vyama vingi si kipaumbele kwa sasa (wakati huo), badala yake tupeleke maji na afya vijijini,” lakini Mwalimu hakuwa na uelewa mdogo kiasi hicho wala hakuwa na ubinafsi uliopitiliza namna hiyo. Mwalimu ni mmoja wa watu waliokuwa na uwezo mkubwa sana na kuishi kulingana na nyakati, majira na vizazi. Wapo watu leo hii, pamoja na kuendeshwa na kanuni za asili za maisha, hawaamini katika kuzitii na watu hao huanguka bila kujua.

Hitaji la Katiba mpya Tanzania, ni takwa la kanuni ya asili ya maisha ya mwanadamu, ni hitaji la lazima la kizazi cha sasa, ni utii wa majira na wakati tuliopo, kudhani kuwa hitaji hili ni mjadala au hiari ni kujiandalia anguko kuu.

Julius Mtatiro ni Mfuatiliaji wa Utendaji wa Serikali barani Afrika, ni mchambuzi wa masuala ya kutaifa na kimataifa +255787536759,