MBALAMWEZI YA KISWAHILI : Kauli ya Kikwete ZIFF izingatiwe na wasanii

Muktasari:

  • Tamasha hilo liliwahusisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi. Mgeni rasmi alikuwa Rais mstaafu wa Awamu ya nne, Jakaya Kikwete.

Hivi karibuni huko Mji Mkongwe, Zanzibar, kulifanyika tamasha la 20 la filamu za nchi za jahazi (ZIFF).

Tamasha hilo liliwahusisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi. Mgeni rasmi alikuwa Rais mstaafu wa Awamu ya nne, Jakaya Kikwete.

Tamasha hilo lilianzishwa miaka 20 iliyopita. Katika maadhimisho ya mwaka huu, Kikwete alitunukiwa tuzo ya ZIFF kutokana na mchango wake mkubwa wa kukuza sanaa nchini Tanzania katika kipindi alichokuwa Rais. Katika hotuba yake Kikwete, alipongeza jitihada zinazofanywa na asasi hiyo kwa kuwa filamu zipitazo katika tamasha lao zimekuwa zikifanya vizuri katika tuzo nyingine ikiwamo tuzo ya Hollywood. Hata hivyo, Kikwete aliwataka kupiga hatua mbele zaidi.

Mbalamwezi ya Kiswahili ‘ilikunwa’ na kauli ya Kikwete ya kukerwa na wasanii wa kiume wanaosuka nywele na kuvaa herini wakiiga tamaduni za wasanii wa kigeni.

Alisisitiza kuwa wasanii wanaoiga tamaduni hizo, wanaharibu utamaduni wa Tanzania.

“Mimi huwa nashangaa ninapomuona kijana wa kiume amesuka nywele au kuvaa herini; ni kinyume kabisa na utamaduni na maadili yetu.”

Akionyesha masikitiko hayo, aliwasihi wasanii wa Kitanzania kufanya mambo yanayoendana na utamaduni wa Kitanzania. Aliwataka kutumia lugha ya Kiswahili katika kazi zao.

Hii ni kwa sababu Kiswahili ni kipengele muhimu cha utamaduni wa Watanzania. “Badala ya kuiga tamaduni za kigeni ambazo ni kinyume na maadili ya utamaduni wetu, tumieni Kiswahili katika kazi zenu za kisanaa,” alisema na kuongeza:

“Kiswahili hiki ni tunu kwetu na kwa kukitumia huko, mtatangaza na kueneza utamaduni wa Kitanzania sehemu mbalimbali duniani kupitia kazi zenu…”

Kwa hakika kauli hii inapaswa kuchukuliwa kwa uzito na wasanii wa filamu na wanajamii kwa jumla. Kila jambo lifanywalo katika utamaduni fulani hubeba maana kulingana na utamaduni husika.

Suala la wasanii kusuka nywele na kuvaa herini si sehemu ya utamaduni wetu. Aidha, katika utamaduni wetu tafsiri ya tamaduni hizo ni kinyume na maadili yetu.

Baadhi ya wasanii wa filamu na muziki, wachezaji wa mpira na baadhi ya wanajamii; wamekuwa na tabia ya kuiga tamaduni za namna hiyo.

Kwa kuwa wanaoigwa, yaani watu wa mataifa ya kigeni hufanya hivyo kama sehemu ya tamaduni zao; badala ya kuiga tamaduni hizo nasi tuutangaze utamaduni wetu kupitia vipengele vyake mbalimbali.

Kupitia kazi anuwai za kisanaa, tunaweza kuutangaza vyema utamaduni wetu. Miongoni mwa vipengele tunavyoweza kuvitangaza kwa urahisi ni lugha yetu adhimu ya Kiswahili.

Wasanii wa Kitanzania huweza kujipambanua katika filamu zao kwa kutumia Kiswahili fasaha, chenye mvuto kiasi cha kuwafanya wageni wakavutika na kujifunza Kiswahili na utamaduni wetu.

Licha ya waigizaji kusuka nywele na kuvaa herini, filamu nyingi huigizwa kwa kutumia pia Kiingereza kibovu kiasi cha wahusika kujidhalilisha.

Filamu za kigeni hutumia lugha ngeni na bado hata kama hatuzijui lugha hizo tunashawishika kununua. Kwa nini nasi tusitumie Kiswahili chetu katika kuutangaza utamaduni wetu?

Tunapoiga tamaduni ambazo kimaadili ni potofu, tunatazamwa tofauti na jamii zetu. Halikadhalika, tunajidhalilisha mbele ya wenye tamaduni hizo na kujionyesha kwamba hatuna utamaduni wetu.

Wasanii wa filamu na wanajamii kwa jumla, tushikilie utamaduni wetu na tukitumie Kiswahili kujitangaza, badala ya kuiga tamaduni za kigeni zisizo na maana kwetu.